Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 11Article 542227

Maoni ya

Columnist: www.habarileo.co.tz

MAKALA MAALUMU Wizara na mwelekeo mpya katika sekta ya biashara

MAKALA MAALUMU    Wizara na mwelekeo mpya katika sekta ya biashara MAKALA MAALUMU Wizara na mwelekeo mpya katika sekta ya biashara

WIZARA ya Viwanda na Biashara imepania kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya biashara nchini katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 kwa kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara zinazofanywa na wananchi na shughuli zote za viwanda.

Akieleza kwa undani katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2021/2022 kuhusu mageuzi hayo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, anasema wizara imedhamiria kuendeleza jitihada za kujenga imani kwa wafanya biashara kupitia kuwepo kwa uwazi na kutabirika kwa mwelekeo wa kisera wa serikali kwa kuwa na mawasiliano chanya ya mara kwa mara.

Anaainisha mikakati na jitihada zinazofanywa na serikali na mafanikio mengi yaliyopatikana katika sekta ya viwanda nchini alipowasilisha Hotuba ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita. Bunge liliidhinisha bajeti hiyo ya Sh bilioni 105.67.

“Tunataka tunapokutana na wafanyabiashara, tufanye mazungumzo yenye tija ya kubadilisha mikakati ya kukuza biashara na masoko, badala mikutano hiyo kutumika tu kama jukwaa la kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara,” anasema.

Anasema wataendelea kuzipitia kanuni za mamlaka za udhibiti, zinazokwamisha biashara kila inapobidi na kwa kuzingatia matokeo ya kitafiti. Vilevile, wizara itachochea na kuhamasisha tabia ya kujali wateja miongoni mwa watendaji wa serikali wanaohudumia sekta mbalimbali za biashara.

Kitila anasema serikali inaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini, ikiwemo kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Anasema tayari ada na tozo 232 zilizokuwa kero na kikwazo kwa biashara nchini zimeshafutwa.

Serikali inaendelea kurekebisha sheria mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kisera na kisheria.

“Tutaweka mkazo na msisitizo wa pekee katika kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi, hususan nchi zenye fursa kubwa ya masoko kama Mashariki ya Kati, China, India, Japan, Umoja wa Ulaya (EU), Marekani, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),” anasema Kitila.

Hata hivyo anadokeza kuwa, limeibuka tatizo la mamlaka mbalimbali kufungia viwanda na biashara bila kushirikisha wizara hiyo yenye mamlaka juu ya viwanda na biashara.

Anasema adhabu ya kufungia kiwanda au biashara ni kubwa na ina athari kubwa kwa uchumi na shughuli za uchumi, mapato ya serikali na jamii.

“Tatizo hili ni kubwa zaidi katika ngazi za mamlaka za serikali za mitaa ambako viwanda na biashara hufanywa kinyume cha taratibu. Ninapenda kukumbusha, kuwaomba na kuagiza tena mamlaka zote kuacha mara moja mtindo huo,” anasema.

Anataka wahusika wazingatie taratibu, kwa kuwapa muda wahusika na kuwaelekeza taratibu za kurekebisha masuala yanayohusika, badala ya kuwatoza faini kubwa na kufungia shughuli husika.

Waziri anasema sekta ya biashara ina mchango mkubwa katika taifa na mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa kwa mwaka 2020 ulikuwa asilimia 8.7 ikilinganishwa na asilimia 8.8 mwaka 2019.

Sekta hiyo ilikua kwa kiwango cha asilimia 2.1 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 5.5 mwaka 2019. Upungufu huo umechangiwa na athari za ugonjwa wa corona.

Aidha, imewezesha uuzaji nje wa bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.06 kwa mwaka 2020 ukilinganisha na Dola za Marekani bilioni 5.00 kwa mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la Dola za Marekani bilioni 1.06.

Ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa uzalishaji nchini na kutumika kwa fursa mbalimbali za masoko.

Wizara hiyo inajitahidi kufuatilia bei za mazao, bidhaa na huduma mbalimbali na kwa jumla mwenendo wa bei za vitu hivyo umeendelea kuimarika.

Ugavi wa mazao ya chakula umeimarika kutokana na mavuno makubwa ya mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020, hivyo kufanya bei za mazao mbalimbali kuwa stahimilivu.

Bei ya gunia la kilo 100 la mahindi imeshuka kwa asilimia 34.7, maharage yameshuka kwa asilimia 7.2 na mchele umeshuka kwa asilimia 27.4.

Aidha, bei ya jumla ya sukari kwa wafanyabiashara na wasambazaji wakubwa ni kati ya Sh 2,300 na Sh 2,533 kwa kilo moja na bei ya rejareja katika maeneo mengi nchini ni kati ya Sh 2,500 na Sh 2,900 kwa kilo.

Bei ya bidhaa nyingine muhimu za viwandani mfano saruji, mabati, na nondo zimeendelea kuwa stahimilivu kutokana na uzalishaji wa kuridhisha katika viwanda vya ndani vya bidhaa hizo.

Kuhusu leseni, anasema kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 leseni 336 za nembo ya ubora ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) sawa na asilimia 67.2 ya lengo la kutoa leseni 500 kwa mwaka 2020/2021 zilitolewa.

Miongoni mwa leseni hizo, 197 zilitolewa kwa wajasiriamali wadogo wanaozalisha mafuta ya kupaka, chaki, mchele, korosho, unga wa mahindi, sabuni za aina mbalimbali, viungo, mafuta ya nazi, keki, juisi, pombe za nafaka, mkate, pombe isiyotokana na nafaka, pombe kali, mvinyo, nyama za kuku, na nyama za kusindika.

Wizara imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wadau mbalimbali katika dhana ya kuzingatia mifumo ya ubora ili kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika.

Mintarafu vipimo, wizara hiyo kupitia Wakala wa Vipimo imeendelea kufanya udhibiti wa bidhaa zilizofungashwa mipakani kupitia vituo vya ukaguzi vya Sirari mkoani Mara, Mtukula (Kagera), Namanga (Arusha), Holili (Kilimanjaro), Tunduma (Songwe), Tarakea (Kilimanjaro), Horohoro (Tanga), Kasumulu (Mbeya) na Kasesya mkoani Rukwa.

Baadhi ya bidhaa zilizoingia nchini na kukaguliwa ni mafuta ya petroli na mafuta ya kula.

Aidha, Wakala wa Vipimo imeendelea kukagua bidhaa zilizofungashwa zinazozalishwa na viwanda vya ndani ili kuhakiki usahihi wa kiasi kilichotamkwa. Baadhi ya bidhaa zilizokaguliwa ni vyakula, vilainishi, saruji, rangi, mitumba, mabati na nondo.

Kuhusu Maonesho ya Sabasaba, Waziri Kitila anasema Wizara kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) iliratibu na kuandaa Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania ambapo kwa mwaka 2020 wadau 596 wa viwanda walishiriki, ikilinganishwa na wadau 542 mwaka 2019.

Washiriki hao ni viwanda vidogo, vya kati na vikubwa na taasisi za serikali zilizotangaza bidhaa na teknolojia wanazozalisha na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda nchini; na kujadili changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya viwanda na biashara.

“Lengo la uratibu wa maonesho hayo ni kuongeza uelewa wa Watanzania kuhusu bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania na kuongeza hamasa ya kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini. Kupitia maonesho hayo, watembeleaji waliona bidhaa hizo na kutambua thamani na ubora wake ili kuzitumia,” anasema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, David Kihenzile, anasema wizara hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotakiwa kutatuliwa haraka.

Alisema hayo wakati akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu hotuba ya bajeti ya wizara hiyo iliyosomwa na Profesa Kitila.

Kihenzile anapongeza hatua zinazochukuliwa na serikali, lakini bado kuna malalamiko kutoka kwa wawekezaji kuhusu mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.

Anasema baadhi ya wawekezaji wanalalamikia uwepo wa changamoto kadhaa. Mfano, mamlaka nyingi za udhibiti, urasimu katika upatikanaji wa vibali vya uhamiaji na mlolongo wa kupata vibali vya uwekezaji.

Kihenzile anaishauri serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa “Blueprint” ili kuondoa changamoto mbalimbali zinaowakabili wawekezaji na wafanyabiashara nchini.

“Kamati inaishauri serikali kukamilisha haraka mchakato wa kuandaa muswada ili uwasilishwe bungeni kwa ajili ya kutatua changamoto hizi,” anasema.

Wabunge kadhaa wanaeleza mengi kuhusu jinsi ya kuboresha uwekezaji na biashara nchini wakati wakichangia hotuba hiyo bungeni.

Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM), anashauri wizara hiyo kupanua wigo wa soko la korosho kwa kutafuta masoko ya Vietnam na Japan, badala ya kutegemea soko la India pekee.

Naye Mbunge wa Solwa, Ahmed Salim (CCM), anasema Wizara ina mipango mizuri, lakini haitafanikiwa kama mpango wa “Blue Print” kwa maana ya kuondoa vikwazo vya biashara nchini hautatekelezwa.

Anamwambia Kitila: “Kama hutafanya hivi utaongea sera nyingi sana, lakini huwezi kufanikiwa. Chukua hii Blue Print lete hapa bungeni, tufute kero zote zinazowasumbua wawekezaji na wafanyabiashara.”

Anasema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndio mamlaka pekee nchini ya kukusanya kodi, hivyo taasisi nyingine zinatakiwa kusaidia kuweka mazingira bora kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini.

Mbunge wa Viti Maalum, Subira Mgalu (CCM), anasema wawekezaji nchini wanalalamikia kuhusu utitiri wa kodi na kuitaka wizara hiyo kutatua haraka suala hilo.

Subira anasema, iwapo mpango wa Blue Print utatekelezwa, kazi ya kuondoa changamoto zilizobakia katika sekta ya biashara nchini itakuwa rahisi.

Anasema TRA, Baraza la Hifadhi wa Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Idara ya Uhamiaji, zina mchango mkubwa kuwezesha mazingira mazuri ya biashara nchini.

Join our Newsletter