Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 26Article 581167

Maoni of Sunday, 26 December 2021

Columnist: www.mwananchi.co.tz

MAONI: Ni wakati wa kuhusisha wamachinga upangaji miji

Ni wakati wa kuhusisha wamachinga upangaji miji Ni wakati wa kuhusisha wamachinga upangaji miji

Fikra na taswira zetu juu ya miji na majiji zimetawaliwa na mitazamo miwili kinzani. Mtazamo wa kwanza umejikita katika kutukuza vitu, ikiwemo mandhari, wingi na unadhifu wa majengo marefu pamoja miundombinu iliyomo jijini. Mtazamo huu unaotaka vitu hivi vilindwe na kuendelezwa kwa gharama yoyote ndio unaoongoza fikra, sheria, sera na mazoezi ya mipango miji.

Mtazamo wa pili huangalia zaidi watu, yaani wakazi na wafanyakazi wa miji, ambao wengi huangukia katika tabaka la wavuja jasho. Wavuja jasho ndio wanaoijenga, kuistawisha na kuilisha miji yetu, wakiwamo walinzi, bodaboda, wafagizi na wabeba zege.

Bila ya wavuja jasho, majiji yasingekuwepo au yangekuwa mfu, majengo yasiyo na watu na miundombinu isiyo na watumiaji. Bila ya wavuja jasho, uchumi wa majiji ungekufa kwa sababu wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa sehemu kubwa ya bidhaa zinazozalishwa au kusambazwa katika majiji ni wavuja jasho.

Licha ya kazi kubwa ambayo wavuja jasho huifanya katika kuistawisha miji, wao ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa upangaji wa miji.

Utaratibu wa mipango miji umo katika sera, sheria na hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa katika kupanga miji yetu.

Tangu nyakati za ukoloni hapa Tanzania Bara, miji yetu ilipangwa katika kanda tatu. Kulikuwa ukanda wa “uzunguni”, ambako waliishi walowezi kutoka Ulaya, ambao ndio walikuwa raia wa daraja la kwanza na wenye uwezo wa juu kiuchumi.

Ukanda wa pili uliitwa “uhindini” ambako waliishi watu wenye asili ya Asia ambao walikuwa raia wa daraja la pili na wenye uwezo wa kati wa kiuchumi kutokana na kupewa jukumu la kusimamia biashara. Ukanda wa tatu uliojulikana kama “uswahilini”, ulikuwa pembezoni na huko walijazana Waafrika, ambao hawakuwa na haki zozote za kiraia wala kiuchumi. Ukanda wa uswahilini ulipuuzwa, kudharauliwa na kunyimwa haki ya miundombinu na huduma za kijamii.

Watu wa tabaka la chini hawawezi kumudu kupanga katika maghorofa yaliyo katikati ya miji kwa ajili ya bishara na makazi. Njia pekee inayobakia kwa watu wa tabaka la chini kujipatia kipato katikati ya miji ni kwa kutembeza bidhaa au kuzipanga katika maeneo ya hifadhi ya barabara na mengine ya wazi yaliyo katika sehemu zenye mzunguko mkubwa wa watu.

Ukiachilia mbali ughali wa kodi za pango, kumekuwa na utaratibu kutimua wamachinga kutoka katikati ya jiji kwa visingizio mbalimbali kama ulinzi na usalama, usafi, unadhifu wa miji, kuongeza mapato ya Serikali n.k. Utaratibu huu wa timua timua ambao umekuwepo tangu ukoloni mpaka hivi sasa, ulisitishwa tu katika awamu ya tano baada ya kiongozi aliyekuwepo kuamua kubadili mwelekeo na kuwaruhusu wamachinga kufanya biashara katikati ya jiji bila kubughudhiwa.

Hivi sasa hatua hizi za “timua timua” zimerejea, japokuwa zimepewa jina la kuwapanga upya wamachinga.

Sehemu kubwa ya wamachinga wameondolewa kutoka maeneo ya katikati ya jiji na yenye mzunguko mkubwa wa watu na kupelekwa pembezoni, kusiko na wateja wala miundombinu ya kueleweka. Kwa ufupi, ni kama wamefungiwa katika hifadhi za watu maskini ili maeneo ya katikati ya jiji yabaki kuwa stahiki ya wafanyabishara wenye mtaji mkubwa.

Historia inatuonyesha kuwa hatua ya aina hii hufanikiwa tu kuharibu mali na vyanzo vya maisha vya watu wa tabaka la chini, na hivyo kuwaacha wakiwa hawana namna nyingine ya kuishi. Wamachinga wengi walioondolewa wameanza kurudi katika maeneo ya awali na kupanga bidhaa chini, lakini wamekuwa wakibughudhiwa na mgambo.

Tunapoadhimisha miaka 60 ya uhuru, ni vema tujiulize: Je, miji yetu inapangwa kwa kuzingatia manufaa na mahitaji ya nani? Ni vema sasa tukaanza mageuzi makubwa ya nadharia, sera, sheria na hatua zinazochukuliwa katika upangaji wa miji ili kutoa haki-jiji kwa wafanyabiashara wadogowadogo, wanaofahamika kama wamachinga. Kwa kuanzia, ujenzi wa miundombinu na upangaji wa miji uwe shirikishi, na uache nafasi ya wazi kila upande wa barabara na vituo vya daladala kwa ajili ya wamachinga. Pia, maeneo ya wazi pamoja na hifadhi ya barabara yawe ni miliki ya wote kwa ajili ya kutumiwa na wamachinga. Haki-jiji inawezekana!