Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2019 11 27Article 489187

Maoni of Wednesday, 27 November 2019

Columnist: mwananchi.co.tz

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Lumumba akamatwa baada ya kutoroka, ateswa-8

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Lumumba akamatwa baada ya kutoroka, ateswa-8

Alhamisi ya Desemba mosi, 1960, Patrice Lumumba, alikamatwa na majeshi ya serikali ya Congo baada ya kutoroka. Alikamatiwa eneo la Mweka, Jimbo la Kasai alipokuwa akielekea Stanleyville (sasa Kisangani) baada ya kutoroka Leopoldville (sasa Kinshasa) alikokuwa chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa (UN), lakini akilindwa na majeshi ya Mobutu.

Ingawa msafara wao ulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakitoroka naye, ni Christophe Gbenye, Anicet Kashamura (aliyekuwa Waziri wa Habari) na Pierre Mulele (Waziri wa Elimu) tu walifanikiwa kumaliza safari yao.

Lumumba, Maurice Mpolo (aliyekuwa Waziri wa Vijana na Michezo) na Joseph Akito (makamu rais wa Baraza la Seneti) walikamatwa na kurejeshwa Kinshasa, lakini Joseph Mbuyi na Barthelemy Mujanay (aliyekuwa Gavana wa Benki Kuuo) waliuawa katika Jimbo la Charlesville.

Siku iliyofuata, wanajeshi 40 walimtoa Lumumba kutoka eneo walilomkamata la Lodi-Mweka na kumsafirisha kwa njia ya barabara hadi uwanja mdogo wa ndege wa Port Francqui ambako alisafirishwa kwa ndege kurudishwa Kinshasa ambapo waliwasili saa 11:00 jioni. Muda wote wakiwa angani, Lumumba na wenzake walikuwa katika mateso makubwa hadi ndege ilipotua na wao kuteremshwa na kupakiwa kwenye lori.

Lumumba alitoroka Kinshasa kwa kutumia gari aina ya Peugeot 403, mali ya mtu aliyeitwa Kamitatu Cleophas na ilikuwa ikiendeshwa na Mungul Diaka.

Johannes Fabian, mwandishi wa kitabu cha “Remembering the Present: Painting and Popular History in Zaire (uk 115)”, anasimulia kuwa Lumumba alikuwa katika gari hiyo ya rangi nyeusi, ingawa mwandishi mwingine, Anna Purna, katika ukurasa wa 285 wa kitabu “Dr. Lumumba’s Dream of Incest”, anasema gari hilo ni Peugeot lakini la rangi nyeupe.

Sehemu ya simulizi ya tukio hilo inasema baada ya kuvuka Mto Sankuru, alirudi kumchukua mkewe Pauline Opango Lumumba, na mtoto wao wa mwisho, Roland, waliokuwa ng’ambo ya mto, na ndipo alipokamatwa.

Wenzake, akiwamo Pierre Mulele, waliovuka mto na Lumumba, walifanikiwa kufika salama Port Francqui Desemba mosi.

Ijumaa, Desemba 2, 1960, muda mfupi kabla ya saa 11:00 jioni, ndege ya Congo DC-3 ilitua uwanja wa ndege wa Ndjili mjini Kinshasa. Ndani yake alikuwamo ofisa usalama wa Congo, Gilbert-Pierre Pongo, Lumumba na wanajeshi.

Pongo ni mmoja wa maofisa usalama wa serikali ya Congo waliomfuatilia Lumumba hadi kumkamata.

Umati wa watu uwanjani hapo ulikuwa ukisubiri kuona wanaoshuka kwenye ndege hiyo. Miongoni mwa waliokuwa kwenye umati huo ni waandishi wa habari, wapigapicha, maofisa wa serikali na wa jeshi la ANC.

Lumumba alikuwa wa pili kushuka, akiwa nyuma ya Pongo ambaye sasa alionekana kama shujaa kwa kuwezesha kukamatwa kwa Lumumba. Mikono ya Lumumba ilifungwa nyuma kwa kamba. Picha zilizopigwa siku hiyo zinamuonyesha alikuwa amevaa shati jeupe.

Lumumba na mateka wengine wawili walisukumwa kuingia kwenye lori kusubiri safari nyingine. Mwandishi wa kitabu cha “The Assassination of Lumumba”, Ludo de Witte anaandika kuwa kwa faida ya wapigapicha, mwanajeshi mmoja alimkamata Lumumba na kunyanyua kichwa chake juu ili apigwe picha.

Kwa mujibu wa kitabu hicho, mwangalizi mmoja wa UN aliyekuwa uwanjani hapo, alisema Lumumba alipoteza miwani yake na shati lake lilitapakaa damu, na kulikuwa na damu iliyovia kwenye shavu lake la kushoto.

Mateka hao walipelekwa kambi ya jeshi ya Binza karibu na makazi ya Mobutu. Waandishi waliokuwa kambini hapo wakati Lumumba anawasili, walisema alikamatwa na kuonyeshwa kwa wapigapicha ili apigwe picha. Wakati huo Mobutu naye alikuwa akiangalia.

Baadaye alitupwa ardhini huku akipigwa na wanajeshi waliomzunguka. Kisha Pongo akapaza sauti kuwataka wanajeshi hao wazidi kumpiga.

Baada ya kumkamata Lumumba, Pongo alipandishwa cheo na kuwa kapteni. Alitumwa kwenda Bukavu, lakini huko alikamatwa.

Januari mosi, 1961, siku 16 kabla Lumumba hajauawa, Pongo alitumwa na Mobutu kuongoza shambulio kwenye mji wa mpakani wa Bukavu, ikiwa ni jaribio la kulirejesha eneo hilo kwenye himaya ya Mobutu. Hata hivyo, alikamatwa na kuwekwa mahabusu katika mji wa Kisangani na mahabusu wengine ambako maofisa walitoa sharti la kumuachia kama Lumumba naye angeachiwa. Lumumba hakuachiwa na hivyo Pongo naye hakuachiwa.

Februari 20, 1961, ikiwa ni siku tatu baada ya Lumumba kuuawa, Pongo na wenzake 14 waliuawa na wafuasi wa Lumumba.

Wakati wakiwa bado wanamshikilia na kumtesa Lumumba, mwanajeshi mmoja alisoma ujumbe ulioandikwa kwenye karatasi ukidaiwa kuwa uliandikwa na Lumumba mwenyewe akidai kuwa yeye ndiye kiongozi halali wa serikali ya Congo.

Baada ya kuusoma ujumbe huo, mwanajeshi mmoja aliichukua karatasi hiyo, akaikunjakunja na kuisukumiza mdomoni mwa Lumumba. Baada ya hapo Lumumba alipelekwa chumba kingine ambako mateso dhidi yake yaliendelea.

Siku hiyo usiku, mkuu wa Idara ya Usalama ya Congo, Victor Nendaka, alimpeleka Lumumba mahabusu. Kwa mujibu wa Alfred Cahen, mwanadiplomasia kijana aliyewasili Congo muda mfupi baada ya Lumumba kushushwa kwenye ndege na ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Nendaka, alisema baadaye Nendaka alimwambia kuwa alimfungia Lumumba kwenye gereji ya aliyekuwa mkuu wa ujasusi katika serikali ya kikoloni, Kanali Frederic Vandewall.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Pierre Wigny, alikaririwa akisema Desemba 3 alipokea telegramu kutoka ubalozi wa Ubelgiji mjini Brazzaville.

“Alitendwa kikatili sana usiku wa tarehe 2 kuamkia 3 na makomando waliochoma hata ndevu zake,” unasema ujumbe huo.

Bomboko aliingilia kati kutuliza hasira, lakini hakufaulu. Kwa mujibu wa walioshuhudia, “waliomtesa Lumumba ni watu wakatili sana”.

Justin Marie Bomboko Lokumba ni mwanasiasa wa Congo ambaye hakuaminiwa na Lumumba. Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo, alishiriki katika kukamatwa kwa Lumumba.

Ujumbe huo kwa njia ya telegramu ulitumwa na Robert Rithschild akiwa ubalozi wa Ubelgiji mjini Kinshasa. Katika ujumbe mwingine alioutuma Brussels siku hiyo, Rothschild alisema: “Hatua muhimu zinachukuliwa kuhakikisha kuwa Kasavubu anawadhibiti mahabusu.”

Vyombo vya habari vya kimataifa vilipiga picha wakati Lumumba akiadhibiwa na askari wa Congo katika uwanja wa ndege wa Ndjili na kisha kwenye kambi ya Binza.

Balozi wa Marekani nchini Congo, Clare Hayes Timberlake, alituma telegramu kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Christian Archibald Herter, akimsihi ajitahidi kuzuia kusambaa picha za mateso ya Lumumba kwa sababu “zinaweza kutengeneza bomu la atomiki”.

Picha hizo zilianza kutia simanzi na hasira maeneo mengi ya dunia ambako zilionekana kwenye vyombo vya habari.

Wanasiasa kadhaa walianza kutilia shaka uwezo wa UN, wakihoji wanawezaje kuwalinda Wabelgiji walioko Congo lakini wanashindwa kumlinda Lumumba anayekubaliwa na Bunge na wabunge wa nchi yake.

Nchi kadhaa za Afrika zilitishia hata kuondoa wanajeshi wao katika jeshi la UN lililokuwa Congo, UNOC.

Hata hivyo UN haikushinikiza Lumumba aachiwe, pamoja na kukiri alikuwa na kinga ya Bunge.

Majeshi ya UN hayakufanya chochote zaidi ya kutazama hali ilivyokuwa inakwenda nchini Congo kuhusu Lumumba.

Itaendelea kesho…