Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2019 12 02Article 489817

Maoni of Monday, 2 December 2019

Columnist: mwananchi.co.tz

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Mwili wa Lumumba wafukuliwa, wayeyushwa kwa tindikali-14

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Mwili wa Lumumba wafukuliwa, wayeyushwa kwa tindikali-14 MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Mwili wa Lumumba wafukuliwa, wayeyushwa kwa tindikali-14

Siku moja baada ya mauaji ya Lumumba na wenzake, habari zilianza kusambaa kuwa wameuawa. Habari zilipoanza kusambaa, maofisa wa Katanga walipanga kwenda kufukua miili hiyo na kwenda kuizika kwingine mbali ambako waliona ni vigumu kufikiwa.

Jioni ya Januari 18, Kamishna wa Polisi wa Ubelgiji, Gerard Soete, Kamishna wa Polisi, Frans Verscheure na Kapteni Julien Gat waliamua kuwa lazima miili hiyo ifukuliwe, iondolewe eneo hilo na kwenda kufukiwa kwingineko ili kupoteza ushahidi wa mauaji hayo.

Kwa mujibu wa kitabu ‘The Assassination of Lumumba’, jioni ya Januari 21 Wazungu wawili wakiwa katika sare na Waafrika wachache waliondoka mjini kuelekea Kasenga ilikokuwa imefukiwa miili hiyo. Watu hao walikuwa katika lori la serikali ya Katanga lililokuwa limebeba alama za barabarani na mapipa mawili yenye tindikali.

Walipofika Kasenga waliifukua miili hiyo, wakaifunga kwenye turubai na kuitupa nyuma kwenye lori. Soete na wenzake walianza tena safari ya kiasi cha maili 150 kuelekea karibu na mpaka wa Congo na Rhodesia (Zimbabwe). Waliingia katika msitu ulioko karibu na mpaka wa nchi hizo.

Safari hii walichimba mashimo marefu zaidi, kiasi cha futi sita kwenda chini. Waliishusha miili ya Lumumba, Okito na Mpolo kwenye mashimo hayo na kuifukia. Hii ilikuwa ni mara ya pili kuifukia.

Baada ya kumaliza kazi ya kuwafukia, Soete na wenzake waliamua kutorudi Elisabethville. Safari ya kurudi ilianza kesho yake alfajiri, Januari 22 saa 11:30. Hata hivyo, inaelekea kuwa kifo cha Lumumba kiliendelea kuwatesa maofisa wa serikali ya Katanga.

Pamoja na kwamba maiti hizo sasa zilikuwa zimefukiwa ardhini mbali na mjini, maofisa hao hawakuacha kuzifikiria. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Katanga, Godefroid Munongo, aliona amepata wazo la kuondokana na maiti hizo.

Aliona njia pekee ni kuhakikisha wanapoteza ushahidi wowote ambao ungeweza kuunganisha mauaji hayo na serikali ya Katanga. Katika kikao chao kimoja ilionekana kuwa kaburi lolote atakalozikwa Lumumba huenda likagundulika na kuzua matatizo.

Alhamisi ya Januari 26, 1961, Munongo aliwatuma tena Soete na timu yake kwenda kuifukua tena miili ya Lumumba, Okito na Mpolo kwa mara ya pili. Safari hii walitaka kuhakikisha miili hiyo inatoweka kabisa.

Munongo alimwagiza Kamishna Verscheure aandae mapipa mawili ya tindikali ya betri za magari iliyokuwa ikitengenezwa na kampuni ya Union Miniere. Nia ya kuandaa mapipa hayo ni kuiyeyusha miili ya Lumumba, Okito na Mpolo ili kupoteza ushahidi wowote.

Siku ya 10 baada ya kuuawa, Lumumba, Mpolo na Okito walifukuliwa kwa mara nyingine. Soete ndiye aliyeongoza wengine kufanya kazi hiyo. Safari hii walikuwa na visu na misumeno waliyoitumia kukatakata viungo vya miili ya marehemu hao vipande vipande.

Alama za barabarani walizobeba kwenye lori waliziweka barabarani kuwafanya watu waamini kuwa kuna kazi ya barabara iliyokuwa ikiendelea eneo hilo. Mapipa yenye tindikali nayo yaliwekwa barabarani. Watu waliopita eneo hilo walihisi kuwa hao ni wahandisi wa barabara wakiendelea na ujenzi wa barabara.

Vipande vya miili ya akina Lumumba vilivyokatakatwa vilitupwa kwenye mapipa ya tindikali ili viyeyuke. Hata hivyo hakukuwa na tindikali ya kutosha kuyeyusha miili ya wote watatu. Sehemu za mwili ambazo hazikuyeyuka zilichomwa moto. Lakini Soete alibaki na meno mawili ya Lumumba kama kumbukumbu yake.

Kazi hiyo ya kuikatakata miili hiyo ilichukua siku mbili, usiku na mchana hadi ilipomalizika Jumatano ya Februari 1.

Ili kuficha ukweli kuhusu mauaji ya Lumumba na wenzake wawili, wanajeshi watatu wa Katanga waliojifanya kuwa ni Lumumba na wenzake waliouawa, walipakiwa kwenye magari yaliyokuwa kwenye msafara wakijifanya wanapelekwa gerezani.

Katika vituo kadhaa vya barabarani magari hayo yalisimama na wananchi walielezwa kuwa waliokuwa wamebebwa kwenye magari hayo ni Lumumba na wenzake na walikuwa wakipelekwa gerezani. Ilidaiwa walikuwa wanapelekwa gereza la Kasai.

Majuma mawili baadaye, Ijumaa ya Februari 10, Redio Katanga ilitangaza kuwa ‘mateka’ hao wametoroka gerezani. Redio hiyo ilidai kuwa ‘mateka’ hao walivunja ukuta wa gereza, wakaiba gari na kutoroka, lakini gari lilipokwama walilazimika kukimbia kwa miguu.

Serikali ya Katanga ikatangaza kuwa wanawatafuta ‘mateka’ waliotoroka. Wakaenda mbali zaidi kwa kusema wametoa ‘donge nono’ kwa yeyote atakayewezesha kukamatwa kwao.

Hatimaye Waziri wa Mambo ya Ndani wa Katanga, Godefroid Munongo, akatangaza kwamba watatu hao walikamatwa na wakulima na kisha wakauawa. Hata hivyo hakuonyesha ni wapi walikamatwa na waliuawa na nani. Ingawa alionyesha hata vyeti vya vifo vya watu hao, hakuweza kuonyesha hao waliokamatwa na miili yao iliwekwa au kuzikwa wapi.

Waandishi Leo Zeilig, David Renton na David Seddon waliandika kitabu wakakiita ‘The Congo: Plunder and Resistance’. Kuhusu tangazo hilo la redio, waandishi hao wameandika: “Wakati tangazo la kifo cha Patrice Lumumba lilipotolewa redioni kwamba aliuawa na wanakijiji waliokuwa na hasira. Hakuna aliyeamini. Hili tangazo lilikuwa ni fedheha. Hakukuwa na maziko. Miili ya Lumumba na wenzake iliharibiwa.”

Baada ya kumalizika kwa sherehe na shamrashamra nyingine za kuapishwa kwa Rais mpya wa Marekani, John F. Kennedy, Mkuu wa Operesheni ya Umoja wa Mataifa nchini Congo na ambaye ofisi zake zilikuwa mjini Leopoldville, Rajeshwar Dayal, alimtaka Moise Tshombe kutoa mabaki ya miili ya Lumumba na wezake ili ipelekwe Leopoldville kwa maziko.

Lakini Tshombe alikataa. Kitabu ‘Death in the Congo’ kinamkariri Tshombe akisema, “Kulingana na mila zetu ni marufuku kufukua mwili uliozikwa...”

Karibu miaka 40 baada ya tukio hilo, mshiriki mkuu wa utekelezaji wa mauaji hayo, uchunguzi mpya juu ya mauaji hayo ulianza kufanyika. Aliyekuwa Kamishna wa Polisi wa Congo wakati wa kukamatwa na kuuawa kwa Patrice Lumumba ni Verscheure.

Mwaka 2000 alikuwa tayari amerudi kwao Ubelgiji. Alihojiwa mara mbili na tume iliyokuwa inafanya uchunguzi wa mauaji ya Lumumba. Wakati huu Verscheure alikuwa amezeeka na alikuwa ameshakuwa kipofu. Verscheure alisema aliamua kutoa ushuhuda wake ili angalau jambo hilo limtoke kifuani mwake kwa sababu lilikuwa linaitesa sana dhamira yake kwa miaka 40.

Alisema baada ya kuwafikisha mahabusu hao eneo ambalo waliuawa, yeye Verscheure aliwatoa kwenye gari mmoja baada ya mwingine. Kwanza alianza kumtoa Okito, kisha Mpolo na mwisho Lumumba.

“Walipompiga Okito risasi,” anasimulia Verscheure, “niligeuka na kuwaangalia wale wengine wawili (Lumumba na Mpolo) kupitia kwenye kioo cha gari na kuwaambia ‘punde tu kazi hii itakwisha.’ Niliwaambia wasali sala yao ya mwisho. Kisha akamtoa Mpolo, ambaye alionyesha ishara ya msalaba, kisha akapiga magoti.

Mpolo alianza kusali na wakati akiwa katikati ya sala ndipo akamiminiwa risasi na wanaume wanne waliokuwa na silaha. Sasa alikuwa amebaki Lumumba peke yake baada ya wenzake wawili kuuawa.

“Nilimwambia Lumumba, sali sasa ... Lumumba hakujibu kitu. Hakujibu chochote. Alikuwa mkimya kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Sikumwona kabisa akibabaika.”

Katika mahojiano aliyofanyiwa Oktoba 2, 2000, Verscheure alisema walipokuwa gizani kutekeleza mauaji hayo alihisi kutetemeka.

Alisema milio ya risasi zilizofyatuliwa kuwalenga Lumumba na wenzake na vishindo vyao vya kuanguka kwenye mashimo waliyochimbiwa kama makaburi kulimfanya ahisi kuwa na homa.

Baada ya kazi ya mauaji hayo, Verscheure na dereva wake walirudi moja kwa moja kuelekea nyumbani kwa Rais Tshombe. Wapokezi walimwelekeza akasubiri kwenye chumba cha wageni.

Nyumbani kwa Rais Tshombe aliwakuta maofisa wengine wawili wa serikali ya Katanga, Fernand Kazadi na Jonas Mukamba.

“Walinihoji sana. Waliniuliza maswali mengi. Sikumbuki nilikuwa nawajibu nini, lakini waliendelea kuniuliza kama vile mimi ni Mungu. Walitaka tu kujua kama (Lumumba) amekufa. Kisha Tshombe akaingia ukumbini akitokea kwenye chumba cha ofisi yake. Akazungumza nami kwa muda fulani. Alikuwa kwenye taharuki.”