Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 21Article 538885

xxxxxxxxxxx of Friday, 21 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

MIAKA 25 AJALI YA MV BUKOBA Akumbuka mengi yaliyojiri baada ya ajali

DAUDI Yusuph alisikia sauti ikimwita na kumwamuru kuondoka alipokua ameketi wakati meli ya MV Bukoba ikianza kuzama asubuhi ya tarehe 21, Mei, 1996.

Ilimuita mara ya kwanza na ya pili akakaa kimya, ya tatu akaitika na kutii amri ya kutoka chumba cha kuongozea meli ambako alikwenda kwa mazungumzo na wafanyakazi wenzake.

Alitii amri licha ya kwamba hakumwona wala kujua aliyemuita, akaenda moja kwa moja sehemu ya chakula (buffet) ambako ndiko ilikua eneo lake la kazi kwani ndiye alikua mpishi mkuu wa MV Bukoba.

“Kwa asilimia zote naamini aliyeniita ni malaika aliyetumwa na Mungu kunikoa,” anasimulia.

Alipofika sehemu ya chakula alichungulia dirishani na kugundua tayari meli ilianza kuzama upande wa kushoto wa meli.

Alirudi juu zinapohifadhiwa boti za uokoaji lakini kabla ya kufanya chochote MV Bukoba ilipinduka, chini juu, juu chini na kumfanya yeye kwenda chini zaidi kwenye maji.

Anasema alienda chini na kurudi juu mara kadhaa, ndipo mara ya mwisho akafanikiwa kuona kile anachokiita ‘propeller' na ‘usukuni' wa meli, akashika na kuning'inia kwa saa kadhaa bila kukanyaga popote japo kwa dakika moja.

Wakati akikaribia kukata tamaa na kuwaza kuachia ajitupe tena kwenye maji kutokana na kuchoka mikono, ndipo akaona boya (life jacket) likining’inia mbele yake, akalidaka na kulivaa.

“Na ilikua bahati sana kwangu kuliona kwani baada ya meli kupinduka tenki la mafuta lilipasuka na kasambaa kote. Maji hayo machafu yalikua yakinipiga machoni na kuniwasha, nikawa muda mwingi nayafumba (macho).

“Nilipolazimisha kuyafumbua ili kutafuta namna zaidi ya kujiokoa, ndio nikaona boya licha ya uono wangu kuwa hafifu,” anasimulia zaidi.

Anasema boya lilivutwa kwenda juu na kumfikisha kwenye kipande kidogo cha mgongo wa MV Bukoba kilichokua bado kimesalia maana meli ilikua ikiendelea kuzama ikiwa imepinduka vilevile (juu chini, chini huu).

Anasema aliwakuta baadhi ya watu ambao ndio walivua mashati yao, wakayafunga kwa pamoja ili kupata kamba ndefu ya kufunga kwenye boya na kuwarushia wenzao waliokua chini ya maji.

Kipande kile cha mgogo wa meli kikiwa kimebakia sehemu ndogo sana kutokana na MV Bukoba kuendelea kuzama kilimfanya Yusuph na wenzake kukata tamaa ya kupona. Wakiwa katika hofu na taharuki, ndipo wakaona boti ya uokoaji ya polisi ikielekea walipo.

Anasema waliokolewa na kuungana na wenzao kwenye meli ya MV Butiama na kisha kupelekwa katika Hospitali ya Bugando.

Anasema waliokua na hali mbaya walilazwa na wengine walichunguzwa afya, kutibiwa na kuruhusiwa siku hiyo hiyo, akiwemo yeye Yusuph baada ya kuhojiwa na kuthibitisha kwamba hakuwa na tatizo lolote la kiafya.

Maisha yake baada ya ajali

Takribani siku nne baada ya Yusuph kuungana na familia yake alirudishwa Hospitalini Bugando akiwa hajitambui baada ya kupatwa na tatizo la akili, na madaktari wakathibitisha hilo.

Anasema muda wote picha ya ajali, mpaka anaokolewa na kukanyaga nchi kavu ilikua ikimrudia, akawa anashindwa kuamini kilichotokea, na hivyo kushindwa kulala na hatimaye kuchanganyikiwa.

Kwa kumbukumbu zake kwenye meli walikuwemo jumla ya wafanyakazi wapatao 20 lakini 13 wote waliangamia, hali iliyomfanya Yusuph kuchanganyikiwa zaidi kila alipokumbuka wenazake.

Mbali na tatizo la akili Yusuph pia alikua akisumbuliwa na macho pamoja na masikio, huku madaktari wakimueleza kuwa ni kutokana na kukaa muda mrefu katika maji yaliyochanganyikana na vitu vingine hatarishi, hasa mafuta yaliyosambaa baada ya tenki la meli kupasuka.

Alilazwa Bugando kwa zaidi ya wiki mbili na kuruhusiwa huku matatizo ya macho na masikio yakiwa yametibika kabisa lakini akaendelea kuhudhuria kliniki ya tatizo la akili.

Anasema si tu picha ya ajali iliyokua ikimuumiza akili bali pia alipokua anawaza ni jinsi gani mke wake angeweza kulea mimba peke yake kwani wakati huo mkewe alikuwa na ujauzito wake wa pili.

Aliwaza pia jinsi ambavyo mtoto wao angeweza kuyakosa mapenzi na malezi ya baba, na badala yake kupewa tu hadithi ya ajali mbaya ya MV Bukoba kumpoteza mzazi wake.

“Na mtoto aliyezaliwa ndiye alikua kitinda mimba wetu kwani hatukubahatika kupata mtoto mwingine. Ni hao wawili tu,” anasema.

Baada ya miezi kadhaa alirudi kazini. Utaratibu wa mwajiri wake, enzi hizo Shirika la Reli nchini (TRC), ilikua ni kumpangia kazi ya mapishi katika meli yoyote iliyokua na safari katika Ziwa Victoria.

Hata hivyo anasema alishindwa kustahamili kufanya kazi kwenye maji kwani picha ya ajali ya MV Bukoba ilianza kumrudia upya na kufufua tatizo lake la akili na hivyo kurudishwa Bugando mara kwa mara.

“Kichwa kilielemewa zaidi pale nilipokua nikifika eneo la ajali. Akili ilikua haikubali kwamba pale ndipo wenzangu walipopotezea maisha, lakini mimi nikapona,” anasema.

Kuacha kazi kwa manufaa ya umma

Kutokana na kusumbuliwa na tatizo la afya ya akili mara kwa mara, Yusuph aliomba kustaafu kwa hiari, akiamini kwamba akiacha shughuli za kumfanya kuwa kwenye maji muda mwingi atatengamaa.

Mbali na wazo la akili kutulia akiacha kufanya kazi kwenye maji, lakini pia hakuwa na uwezo wa kufanya chochote akiwa melini kutokana na msongo wa mawazo na hivyo kujiona hafai kuwepo kwenye nafasi ile.

“Kwa kweli nilihisi nakula mshahara wa bure, simtendei haki mwajiri wangu.”

Ombi lake lilikubaliwa na hatimaye akastaafu mwaka uliofuata, akapewa mafao yake kiasi cha Sh 300,000 na kidogo, akaanza maisha mengine na kwa sasa anauza bidhaa ndogondogo maarufu kama ‘genge'.

Yusuph mwenye umri wa miaka 73 sasa anasema wazo la kustaafu lilimsaidia kwani baada ya miezi kadhaa kichwa chake kilikaa sawa.

Maoni yake juu ya kinachoweza kuwa kisabishi cha ajali

Anasema haamini kama kweli MV Bukoba ilizidiwa uzito, ndio ikawa sababu ya kuzama kama weni wanavyoamini.

Anakiri kutokuwa na ujuzi wowote katika masuala ya usafirishaji wa melini lakini anajiuliza na kuuliza wengine kwamba: “MV Bukoba iliwezaje kusafiri mwendo wa takribani saa nane Kutoka Bukoba bila tatizo lolote kama uzito ndio ilikua sababu?”

Anasisitiza kwamba kama ni uzito uliopindukia, MV Buboba isingeweza kusafiri mwendo wote huo na kuja kuzama kilometa chache kabla ya kutia nanga katika bandari ya Mwanza.

Kwa mawazo yake, anasema kuna uwezekano mkubwa nahodha alishindwa kukata kona, meli ikalalia upande mmoja na ndio ikawa chanzo kama ilivyo kwa magari ambayo hupata ajali baada ya dereva kushindwa kukata kona.

“Kwa nilivyoona mimi ajali ilitokea kwenye kona na ndio maana ilianza kuzama upande wa kushoto. Nahisi nahodha hakujipanga vizuri au alipitiwa wakati wa kukata kona,” anasema.

Maoni yake juu ya kwa nini meli ilitoweka jumla

Anasema baada ya waokoaji kuitoboa kwa nia ya kuokoa wahanga, maji yaliingia kwa wingi na kuzidisha uzito, ikazidi kwenda chini.

Anakiri kwamba hata kama meli insingetobolewa si watu wote wangeokolewa lakini huenda idadi ingeongezeka.

“Au hata maiti huenda zingeokolewa zaidi, kwa mawazo yangu,” anasema huku akiwa ameshika gazeti lenye majina na idadi ya watu 90 walionusurika, alilolitunza kama kumbukumbu yake.

Join our Newsletter