Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 22Article 580342

Maoni of Wednesday, 22 December 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

MZEE WA UPUPU: Azam FC inakosa watu wa mpira

Sehemu ya Kikosi cha Azam FC Sehemu ya Kikosi cha Azam FC

Bandari ya Dar es Salam ni ya kipekee sana. Nahodha wa meli hata awe mzoefu kiasi gani duniani, lakini akifika pale lazima akutane na wataalamu wamuongoze.

Tatizo ni kwamba kutoka eneo la karibu na soko la samaki la Kivukoni kupita eneo ambalo vivuko vya kwenda Kigamboni hupita kuna kina kifupi kuweza kuhimili meli kubwa.

Hivyo Mamlaka ya Bandari (TPA) iliipa kazi kampuni ya ukandarasi kuchimba njia ya meli kutokea eneo lile hadi kufika bandarini kabisa. Na ndiyo maana meli zikija zikishafika karibu na soko la samaki lazima zipate nahodha wa bandari ili aziongoze kupita pale, la sivyo zitakwama.

Hao manahodha wa Mamlaka ya Bandari ni wataalamu wa ile njia. Wanaijua kiasi kwamba hata uwaamshe usiku wa manano wanakupitisha bila shaka. Watu wa aina hiyo wapo kila sehemu na kwenye mpira ndiyo huitwa watu wa mpira.

Watu wa mpira ni wataalamu wa siasa za mpira, fitna za mpira, sayansi ya mpira, figisu za mpira na ustaarabu wa mpira. Hawa ni watu wanaojua usiku na mchana wa mpira. Hawa ni watu wanaozijua njia za mpira kama wale manahodha wa Mamlaka ya Bandari wanavyojua ile njia ya kuchongwa na mkandarasi.

Sasa hawa ndiyo watu ambao Azam FC inakosa kiasi cha kujikuta ikikwama kila uchao na kuacha maswali lukuki kwa watu waliokuwa na matarajio nao. Endapo wangekuwepo watu hawa, wangewashauri wamiliki wa klabu hiyo kuelewa soka kwa mapana yake.

Ni bahati mbaya sana kwamba wamiliki wa Azam FC wanajua sana kuhusu soka, na wana mapenzi makubwa na mchezo huo mzuri, lakini wanajua kitu kimoja tu - sayansi ya mpira! Hawajui kama kuna siasa za mpira, fitna za mpira, figisu za mpira na kadhalika.

Mpira ni mchezo wa dakika 90 zinazoandaliwa kwa zaidi ya dakika 800 na kuchezwa ndani na nje ya uwanja. Bahati mbaya sana sayansi ya mpira haizungumzii kabisa kuucheza mpira nje ya uwanja.

Lakini kwa zaidi ya asilimia 60 mpira, hasa wa Tanzania huchezwa nje ya uwanja. Sasa kwa kuwa sayansi haisemi chochote juu ya hilo, ndiyo maana wamiliki wa Azam FC hawajui. Lakini kimsingi kabisa Azam FC inakwama katika kuucheza mpira nje ya uwanja. Dakika 90 za uwanjani ni mwendelezo tu wa kazi nzuri ya nje ya uwanja na wanaoijua kazi hiyo ni watu wa mpira. Azam FC inakosa hawa watu. Wangekuwepo wangesaidia sana kuwafahamisha wenye mali namna bora ya kuimarisha timu yao. Unaweza kusajili wachezaji wazuri sana, lakini wakashindwa kukupatia unachokitaka kwa sababu kuna mtego wametegewa bila wao kujua. Wanaoweza kuutegua ni watu wa mpira. Kuna vitu vinaendelea kwenye mpira unaweza ukavichukulia vya kawaida, lakini hapana, vimepangwa.

Wanaoweza kuvibaini na kuvipatia suluhu ni watu wa mpira. Unapoongoza ligi inabidi kulinda uongozi wako na kuulinda kwenyewe ni kuhakikisha aliyeko nyuma yako hakufikii. Watu wa mpira wanajua kuifanya kazi hiyo. Unapokuwa nyuma ya timu fulani inabidi kumzuia wa chini yako asikufikie na kumsimamisha wa juu yako. Watu wa mpira wanaijua kazi hiyo. Na hii kazi haifanywi kwa sayansi ya mpira ya ndani ya uwanja, bali ni kazi ya fitna, siasa na figisu za nje ya uwanja...watu wa mpira!

Viongozi wa Azam FC ni watu wazuri sana kwa majukumu yao, lakini siyo watu wa mpira. Wamiliki wa timu wanawaamini kwa sababu wana weledi mkubwa, lakini bado timu inakwama. Hizi timu zinazotawala soka la hapa nyumbani zina utitiri wa makundi ya watu wa mpira, kila mmoja akitimiza majukumu yake. Ukiambiwa ‘kamati ya mashindano’ ujue wamejaa watu wa mpira kuhakikisha taarifa zote ‘nyeupe na nyeusi’ za mashindano fulani zinafika mezani kwao.

Viongozi wa Azam FC wote ni watu wastaarabu ambao hawavijui vijiwe vya watu wa mpira vya mjini. Huwakuti kwa yule fundi viatu mtaa wa Samora wala kwenye pilau la Shaurimoyo - Ilala.Wamiliki wa Azam FC wanatakiwa kuunda timu ya watu wa mpira kuizunguka timu yao, watafanikiwa tu. Nenda pale mnara wa askari ukaone kundi la watu wa mpira wanaoshinda pale. Wale wote wapo kuhakikisha mambo yanaenda upande ule.

Shuka chini kidogo mtaa wa Bustani, kundi la watu wa mpira wanashinda pale miaka na mikaka. Mpira una watu wake ambao hawana kazi nyingine zaidi ya hiyo. Ukitaka kufanya kila kitu wewe mwenyewe au ukitaka kufanya kazi na wenye digrii tu, wao watakuangalia tu lakini hutafanikiwa kamwe. Azam FC tafuteni wafu wa mpira.