Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 29Article 581947

Maoni of Wednesday, 29 December 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

MZEE WA UPUPU: Derby Mzizima katika taswira ya Merseyside

Simba na Azam zinakutana Januari mosi, 2022 Simba na Azam zinakutana Januari mosi, 2022

Januari Mosi 2022, Tanzania itaukaribisha mwaka mpya kwa mechi ya kukata na shoka baina ya Simba SC na Azam FC.

Watu wengi wanajua kwamba Simba na Azam FC zina aina fulani ya uhusiano wa kihistoria, lakini hawajui kiundani na wanautafsiri vibaya.

Katika mpira, kila timu ina historia yake na mara nyingi historia hiyo huanzia kwenye timu nyingine, lakini historia hubaki kuwa historia na uhalisia wa wakati husika huchukua nafasi.

Hivi ndivyo ilivyo kwa Liverpool FC na Everton FC - timu za kutoka kitongoji cha Merseyside kwenye mji wa Liverpool nchini England.

Klabu mama ni Everton ambayo ilikuwa ikidhaminiwa na tajiri John Houlding ambaye alikuwa mwenyekiti na mfadhili wa Everton FC huku akimiliki Uwanja wa Anfield.

Baadaye ukatokea mgogoro ndani ya klabu na yeye kujitenga na kuanzisha klabu nyingine ya Liverpool ili iutumie ule uwanja.

Kwa hiyo bwana Houlding akawa amehusika na historia ya klabu zote mbili na kusababisha mechi baina ya klabu hizi kuwa na msisimko mkubwa. Ndiyo ilivyo kwa mechi ya Simba SC na Azam FC.

Timu hizi mbili kihistoria zinaunganishwa na tajiri mmoja wa kuitwa Said Salim Bakhresa. Mzee huyu alikuwa mfadhili wa Simba SC ukatokea mgogoro akajiondoa na baadaye kuanzisha klabu yake, Azam FC.

Ofisi kuu za kampuni zake zote ziko Mzizima, mahali ambapo Azam FC ilipoanzishiwa na ambapo yeye mwenyewe alipatumia kuifadhili Simba SC.

Kwa maana rahisi, Simba SC na Azam FC zinaunganishwa na Mzizima - makao makuu ya kampuni za Bakhresa, ndiyo maana inaitwa Msimamo Derby au Dabi ya Mzizima.

Kama ambayo Liverpool na Everton zina uhusiano wa kihistoria ambao hauna uhusiano wowote na maisha yao ya sasa, ndivyo Simba SC na Azam FC zilivyo.

Licha ya kuunganishwa kihistoria na Mzizima, lakini hazina muunganiko mwingine wowote zaidi ya huo na mechi baina yao ni kama vita.

Hii inathibitishwa na matukio ndani ya mechi au yanayofuata baada ya mechi - tangu mechi yao ya kwanza. Mara ya kwanza zilikutana Oktoba 4, 2008 katika Uwanja wa Uhuru na Simba kufungwa 2-0.

Baada ya mechi, mashabiki wa Simba waliandamana kutoka uwanjani hadi nyumbani kwa mwenyekiti wao Hassan Dalali, Magomeni Makanya na kumtaka ajiuzulu.

Naye akajiuzulu kweli, lakini siku mbili baadaye akarudi kwenye nafasi yake baada ya mashabiki wengine kwenda kumuomba atengue uamuzi wake.

Aliporudi madarakani, akachukua hatua nzito za kuwasimamisha wachezaji wanne; Mussa Hassan Mgosi, Henry Joseph Shindika, Edwin Mukenya na Amani Simba kwamba walihujumu timu.

Pia kocha msaidizi Jamhuri Kihwelu na kocha wa makipa Iddy Pazzy wakafukuzwa kazi. Baadaye Mgosi na Shindika wakasamehewa lakini Amani Simba na Edwin Mukenya wakafukuzwa kabisa.

Jinamizi likahamia Azam FC katika mechi ya mzunguko wa pili msimu huohuo iliyofanyika Aprili 29, 2009 na kuvunjika kutokana na mvua na kurudiwa Aprili 30.

Baada ya mchezo huo ulioisha kwa Simba kushinda 3-0, Azam FC ikamfukuza kocha Neider Dos Santos ambaye hapo zamani alikuwa kocha wa Simba.

Maisha ya timuatimua baada ya mechi hizi yaliendelea ambapo Oktoba 27, 2012 Azam FC ilimfukuza kocha wake Boris Bunjak baada ya kipigo cha 3-1 kutoka Simba.

Pia wachezaji wanne kina Deogratius Munishi Dida, Aggrey Moris, Erasto Nyoni na Said Morad wakasimamishwa kupisha uchunguzi wakituhumiwa kuhujumu timu. Hivi inaonyesha ni namna gani timu hizi hazipendi kufungwa na mmojawapo.

Ni sawa tu na Merseyside Derby ambayo inaongoza kwa kuzalisha kadi nyekundu nchini England na Derby hii inaongoza kwa kufukuzisha makocha. Hans van der Pluijm, kocha mwenye heshima kutoka Uholanzi alifukuzwa na Azam FC baada ya kichapo cha 3-1 kutoka Simba Februari 22, 2019.

Siku ya mwaka mpya zitakutana katika mchezo wa 27 wa Ligi Kuu Bara.

Katika michezo 26 iliyotangulia, Azam FC imenyanyasika sana na ndiyo maana inaongoza kutimua makocha baada ya mchezo. Imefungwa mara 12 yenyewe ikishinda mara saba. Imefungwa mabao 37 yenyewe ikifunga mabao 27. Mechi saba ziliisha kwa sare.