Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 28Article 566365

Maoni of Thursday, 28 October 2021

Columnist: Mwanaspoti

MZEE WA UPUPU: Kuna nini pale Msimbazi?

Mwekezaji katika Klabu ya Simba, Mo Dewji Mwekezaji katika Klabu ya Simba, Mo Dewji

Kuna wakati Arsenal walitaka kumsajili Luis Suarez alipokuwa Liverpool. Tena wakafika bei kabisa na Suarez mwenyewe akataka kulazimisha kuhama Liverpool.

Ni makosa madogo sana ya kutafsiri mkataba ndiyo yaliyokwamisha dili hili.

Mkataba wa Suarez na Liverpool ulikuwa na kipengele kinachomruhusu kuondoka Anfield endapo itakuja timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa ikiwa na kiasi cha zaidi ya Pauni 35 milioni. Arsenal wakaja na Pauni 35 milioni na kuzimwaga mezani kwa mbwembwe, wakaambiwa inatakiwa zaidi ya milioni 35.

Hapo kwenye zaidi ya Pauni 35 milioni ndipo walipofeli Arsenal. Wakaongeza Pauni moja. Naam Pauni moja halafu wakasema tupeni Suarez wetu.

Kumbe kile kipengele cha kwenye mkataba wa Suarez kilikuwa kinaendelea kwa kusema endapo ikitoa zaidi ya Pauni 35 milioni Liverpool wana hiari ya kugoma ila kama itatoa kuanzia milioni 40 Liverpool haina nafasi ya majadiliano zaidi ya kupokea ofa.

Mmiliki wa Liverpool akawashangaa sana Arsenal na kuhoji “hivi hawa huwa wanavuta nini pale Emirates? Nimeona niazime kauli hii kwa kuwashangaa viongozi wa Simba, hivi huwa wanavuta nini pale Msimbazi?

Dakika chache baada ya filimbi ya mwisho katika mchezo wa Simba na Jwaneng Galaxy, mwekezaji Mo Dewji akatoa ujumbe mkali kwa mwenyekiti wa bodi na bodi ya klabu hiyo “since my resignation, I am not in a position to make any decision in Simba, I can only advice the chairman and the board to take stern action on those that are responsible for today’s loss. This is unacceptable!”

“Kwa kuwa nilishajiuzulu, siko kwenye nafasi ya kufanya uamuzi wowote ndani ya Simba, ninachoweza ni kumshauri tu mwenyekiti na bodi kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaohusika na kipigo cha leo. Hii haikubaliki.”

Ukirejea katika taarifa yake ya kujiuzulu utaona Mo alisema amemteua Salim Abdallah ‘Try Again’ kuwa mwenyekiti.

Ukiyatafakari kwa kina utaona haya ni maelekezo au maagizo na siyo ushauri. Mo anatoa maelekezo kwa mtu aliyemteua. Wakati wananzengo tunatafakari kauli hii, mshauri wake Crescentius Magori naye akashuka na ujumbe mkali zaidi - “This is the darkest day in Simba history’ (usaliti ni kitu kibaya sana, hakivumiliki).” Hii ni siku mbaya zaidi katika historia ya Simba. Usaliti ni kitu kibaya sana, hakivumiliki! Mo na Magori kama viongozi waandamizi kwenye mpira hawakutakiwa kuwa na visingizo vyepesi namna hiyo baada ya kufungwa.

Hivi Mo na Magori wanaiona Simba imekua kubwa kiasi gani hadi isifungwe? Imefungwa Real Madrid na wale masharifu wa Moldova, tena Santiago Bernabeu. Real Madrid ndio klabu kubwa kuliko zote kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. FC Sheriff ndio klabu ndogo kuliko zote zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa msimu huu. Lakini wameenda Santiago Bernabeu na kuichapa Real Madrid.

Perez ambaye anafahamika kwa kutokuwa na subira, katulia tu kimya kwa sababu anajua huu ni mpira. TP Mazembe wametolewa na Amazulu - timu ndogo kutoka Afrika Kusini, tena nyumbani lakini Mose Katumbi yupo kimya kwa sababu anajua huu ni mpira. Mo na Magori wanaiona Simba kubwa kiasi gani?

Hivi haya ndo mambo ambayo Magori ambaye ni mshauri wa Mo, huwa ana mshauri?

Eti this is the darkest day in Simba history, kweli? Mwaka 1993 Simba walipofungwa hapa na Stella Abdjan ya Ivory Coast kuna wachezaji na viongozi walituhumiwa kufanya usaliti. Jina baya walilopewa bado linawaandama hadi leo. Miaka takribani 30 sasa, tuhuma bado zilezile kila wakati matokeo yakiwa mabaya kwa Simba.

Walipofungwa na Tanzania Prisons na Ruvu Shooting msimu uliopita, kuna watu walifukuzwa eti wamesaliti.Walitoa sare ya 1-1 na Yanga, kuwa wachezaji wakatuhumiwa kusaliti kwa kucheza chini ya kiwango. Haji Manara alifukuzwa kwa sababu alituhumiwa kusaliti.

Hii ni timu gani ambayo ikikosa matokeo inakimbilia kutuhumu watu kuwasaliti? Magori, ndivyo unavyomshauri Mo hivi. Hapana, hii siyo sawa. Ni dharau kwa wachezaji wao, dharau kwa wapinzani na dharau kwa mpira wenyewe kwa ujumla.

Simba kuifunga Al Ahly ambayo imetoka kushika nafasi ya tatu Klabu Bingwa ya Dunia, haikuwa sawa kimizania lakini uwanjani ilikuwa sawa. Na Al Ahly wala hawakutafuta wasaliti wakasonga mbele na kutwaa ubingwa. Lakini kwa Simba ni usaliti, kuna nini pale Msimbazi?