Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 03Article 567808

Maoni of Wednesday, 3 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

MZEE WA UPUPU: Lwandamina amefika mwisho wa uwezo wake

MZEE WA UPUPU: Lwandamina amefika mwisho wa uwezo wake MZEE WA UPUPU: Lwandamina amefika mwisho wa uwezo wake

KIPIGO cha 2-0 kutoka Yanga ilichopata Azam FC Jumamosi Oktoba 30, hakitoi picha halisi ya namna timu hiyo ilivyo hoi kimbinu na uwezo.

Azam FC haikuwa na uwezo wa kufikisha hata angalau pasi tano mbele. Pasi pekee ambazo zinaweza kuwa zilifikia idadi hiyo ni zile za nyuma. Kigonya amuanzie Amoah naye ampe Mballa halafu kwa Manyama, kwa Bajana na kurudi tena kwa Lusajo. Mabingwa hao wa 2013/14 walicheza kama wanafunzi wanaoshiriki Umisseta...aibu sana!

Timu inapofikia hatua hiyo, hakuna mtu yeyote wa kubeba lawama na dhamana zaidi ya kocha. Na kwa hapa ilipofikia Azam FC, George Lwandamina anatakiwa afungashiwe virago na arudi kwao Zambia...hana jipya tena. Zifuatazo ni sababu kuu za kuharakisha safari yake ya Ndola ambako amechagua kuwe makazi yake kutoka kwao Mufurila.

1. AMEFIKIA MWISHO

Mwaka 2016 Lwandamina aliisaidia Zesco United kufika nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu yake ilitolewa na Mamelodi Sundowns ambao hatimaye wakawa mabingwa. Zesco United ilishinda 2-1 jijini Ndola - Zambia na kupoteza 2-0 ugenini Afrika Kusini. Hapo utaona ni namna gani Zesco United ya Lwandamina ilikaribia kufika fainali.

Lakini 2016 hadi sasa ni zaidi ya miaka mitano - mpira umebadilika sana. Yeye bado anatumia mbinu zilezile ilhali makocha wenzake wanahangaika kila iitwayo siku kuja na mbinu mpya za kurahisisha ushindi. Aina ya uchezaji ya kutegemea mshambuliaji mmoja huku timu ikisubiri mipira ya kutengwa ipate nafasi ya kufunga, haitaifikisha Azam FC mahali popote.

Msimu huu hadi sasa Azam FC imefunga mabao tatu tu - yote yametokana na mipira ya kutenga. Timu yenye viungo wakubwa kama kina Kenneth Muguna inakosa ubunifu wa kupenya ngome ya timu ndogo kama Coastal Union, itapenya vipi kwa Pyramids au Yanga? Kwa sasa Lwandamina hana tena maarifa ya kuisaidia Azam FC kufika popote. Ameishiwa!

2. TIMU HAIELEWEKI

Ukiiangalia Azam FC ya Lwandamina inavyocheza huwezi kuelewa hasa inacheza kwa mpango upi? Muda wote timu inahangaika kujilinda kuliko kushambulia.

Iwe mechi dhidi ya timu kubwa au ndogo Azam FC itacheza na viungo wawili wa ukabaji halafu mshambuliaji mmoja. Bajana na Katema wa nini dhidi ya Namungo, tena Chamazi?

Toa mmoja halafu weka washambuliaji wawili ili uwanja uinamie kwao. Weka viungo wenye ubunifu kama Muguna na Tigere ili nafasi zitiririke kwa ajili ya mtu yeyote kufunga.

Lakini kwa namna ambavyo Lwandamina anaiweka timu haitakuja kutokea Azam FC ikatawala mchezo dhidi ya timu hata ya daraja la nne. Wanaweza wakashinda mechi kama hiyo kwa sababu ya uzoefu wa wachezaji, lakini siyo kwa mipango ya mwalimu.

Azam FC inacheza mpira wa wa kawaida sana kama timu za katikati ya msimamo wa ligi zinazopambana kukwepa kushuka.

3. REKODI MBAYA

Hadi sasa Azam FC imecheza mechi nne za LigiKkuu, ikishinda moja kupoteza mbili na sare moja.

Septemba 27, 2021

(Coastal Union 1-1 Azam FC), Okt. 2, 2021 (Polisi Tanzania 2-1 Azam FC). Oktoba 19, 2021 (Azam FC 1-0 Namungo) na Oktoba 30, 2021 (Yanga 1-0 Azam FC).

Haya ni matokeo mabaya zaidi namba mbili katika historia ya klabu hiyo. Matokeo mabaya zaidi kuliko haya ni yale ya mwanzoni mwa msimu wa 2010/11 ambapo walishinda mechi moja na kupoteza tatu katika nne za kwanza.

Agosti 21, 2010 (AFC 0-2 Azam FC),

Septemba 11, 2010 (Azam FC 1-2 Simba), Septemba 15, 2010 (Kagera Sugar 1-0 Azam FC) na Septemba 18, 2010 (Toto Africans 1-0 Azam FC)

Huu ulikuwa msimu wa tatu wa Azam FC kwenye Ligi Kuu, unaweza ukawapa utetezi wa ugeni kwenye ligi. Lakini sasa wakiwa kwenye msimu wa 14 wana uzoefu wa kutosha ikiwemo kuwa mabingwa. Hawana utetezi wowote zaidi ya kusema wamefelishwa na Lwandamina.

4. MASHABIKI ROHO JUU

Tangu aje Azam FC Novemba 2020, Lwandamina hajawahi kupata ushindi wenye utulivu. Yaani ushindi ambao utamfanya mtu anayekunywa chai asiunguzwe na kikombe.

Azam FC ya Lwandamina inapata ushindi kiduchu wa kutumia mabavu mengi hata dhidi ya timu ndogo. Yaani kama wewe ndo uko upande wa Azam FC siku hiyo utaishi roho juu hata kama timu inaongoza 2-0.

Rudi kwenye mchezo dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora robo fainali ya Azam Sports. Naam, Azam FC ilishinda 3-1, lakini kwa kwa jasho na damu.

Kimbinu, Rangers ambao kocha wao alikuwa mzawa Novatus Fulgence walikuwa bora kuliko Azam FC ila ni bahati mbaya tu walikutana na timu yenye wachezaji wazoefu. Dhidi ya timu kama Rangers hadi siku ya mechi hiyo tayari ilikuwa imeshuka daraja kutoka la kwanza hadi la pili, wachezaji wa kiwango cha Azam FC wanaweza wakashinda mechi kwa kutumia tu makosa binafsi ya wapinzani...na ndicho kilichotokea.

Azam FC walicheza bila mpango wowote zaidi tu ya kutegemea uwezo wa mchezaji mmojammoja.

Kwenye Ligi Kuu ushindi wake mkubwa ulikuwa wa 4-1 dhidi ya Gwambina ambayo ilikuwa inaelekea kaburini. Lakini hata hivyo, hadi mapumziko hali ilishakuwa tete. Ni vile tu kwamba makosa binafsi ya wachezaji wa Gwambina, hasa kipa wao yakawapa ahueni Azam FC, lakini siyo mpango wa kiufundi kutoka uwanja wa mazoezi.

Azam FC ya Lwandamina imekuwa nadra sana kutoka kwenye mchezo bila kuruhusu bao. Hadi sasa ukiwa ni mchezo wa nne hawajaruhusu bao kwenye mchezo mmoja tu. Msimu uliopita kuanzia pale aliposhika hatamu ni mechi 11 katika 20 alizocheza ndizo ametoka bila kuruhusu bao.

5. USAJILI WA HOVYO

George Lwandamina ameenda nchini kwake kuleta wachezaji watakaosaidia Azam FC. Rodgers Kola na Charles Zulu hawana cha kuipa Azam FC ili ifikie malengo yake. Kola ambaye Lwandamina alifanya naye kazi akiwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia chini ya miaka 20 iliyoshiriki Kombe la Dunia 2007 kule Canada, ameshachoka kimwili na akili, hana jipya.

Zulu ni aina ya wachezaji machachari wasio hatari hata kidogo. Ni afadhali Azam FC wangemrudisha kijana wao Adam Adam ambaye wamemlea wao wenyewe kuliko Zulu.

Paul Katema ni mchezaji mzuri, lakini kwa Idris Mbombo kunatia shaka kidogo. Japo ni mchezaji mwenye historia kubwa ambaye Lwandamina alifanya naye kazi Zesco United 2016 hadi kufika nusu fainali, lakini kwa sasa mchezaji huyo raia wa DR Congo ni kama amegota.

Mbombo ni aina ya wachezaji kama Francis Chirwa fulani hivi ambao silaha yao kubwa ni maguvu.

Wachezaji wa aina hii huchuja kadri umri unavyowatupa mkono kwa sababu yale maguvu waliyokuwa wakiyategemea hayatakuwepo tena.

6. HAJUI KUTUMIA WACHEZAJI

Lwandamina ni kama Simba aliyevamia zizi la ng’ombe na sasa hajui ale nyama palepale au abebe akalie mbele. Matokeo yake anaua ng’ombe wote halafu anatoka amechoka bila kula hata mmoja.

Rejea mechi ya mkondo wa pili dhidi ya Pyramids. Dakika 70 za mwisho Waarabu wale walikuwa wamechoka wakiombea mpira uishe. Badala ya kuongeza watu wenye kasi kama Ayoub Lyanga ili kuendelea kuwauliza maswali magumu, akamuingiza Frank Domayo kwenda kuupoozesha mchezo.

Halafu anachelewa sana kufanya mabadiliko kiasi kwamba hata mtu mwenye uelewa mdogo wa mpira anaona upungufu wa wachezaji.

Zulu alipaswa kutoka mapema sana dhidi ya Pyramids. Rodgers Kola alipaswa kutoka ndani ya dakika 30 za kwanza dhidi ya Yanga.

Halafu unacheza na Yanga, unaweka mshambuliaji mmoja anakuwa chini ya ulinzi wa wachezaji watatu - mshambuliaji mwenyewe Rodgers Kola. Hana hata mikimbio, labda angekuwa Dube.

Kwa maoni yangu, Lwandamina ataitoa Azam FC kwenye nafasi nne za juu zitakazoiwezesha kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao. Azam FC chukueni hatua sasa. Lwandamina amefika mwisho wa uwezo wake.