Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 15Article 557548

Maoni of Wednesday, 15 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

MZEE WA UPUPU: Ratiba Ligi Kuu Bara imepwaya kimtindo

Kikosi cha Coast Union kikiwa mazoezini Kikosi cha Coast Union kikiwa mazoezini

Mara zote kumekuwa na mijadala mikubwa kuhusu mechi za saa nane mchana kila inapotoka ratiba ya Ligi Kuu. Yanga na Simba kutopangiwa ratiba ya mechi za saa nane mchana ni swali ambalo mara zote halina majibu yalinyooka.

Hata ratiba ya msimu huu ina shida hiyohiyo pia. Yanga na Simba hawana mechi za saa nane mchana, ilhali wengine wanazo.

Kucheza saa nane, hasa katika nchi ya kitropiki kama Tanzania ni mateso kwa wachezaji. Lakini mateso hayo yanapoepushwa kwa makusudi kwa wachezaji wengine, ndipo inapokuwa shida.

Yanga na Simba wanapata upendeleo kutoka mamlaka za soka, huku wengine wakionyeshwa wazi kwamba kazi yao ni kuhakikisha Yanga na Simba wanafanikiwa, siyo wao kujaribu kutamani kufanikiwa.

Kila unapoanza msimu mpya ukimuuliza Mtanzania yeyote kwamba nani atakuwa bingwa msimu huu, zitatajwa timu tatu kwanza mbili za Kariakoo (Simba na Yanga) na moja ya Chamazi (Azam FC).

Huo ndiyo unaoenda kuwa utamaduni wa Tanzania kwa timu hizi tatu kuwa kioo cha soka la nchi hii. Lakini ili hiyo iwe na maana, ni lazima hizi klabu tatu zipate haki sawa. Kama hiyo haki sawa haiwezekani kwa klabu zote.

Kama Yanga, Simba na Azam ndizo zinazowania ubingwa, basi zipewe haki sawa. Sasa ukiacha suala la mechi za saa nane na hata Yanga na Simba kutoenda baadhi ya viwanja. Kuna jambo lingine ambalo pia haliko sawa kwa Azam FC kwenye hii ratiba ambalo linapaswa kufanyiwa kazi siku za usoni.

Hili ni suala la Azam FC kupangiwa mechi nyingi za usiku na katikati ya wiki inapokuwa katika uwanja wa nyumbani. Ratiba mpya ya msimu wa 2021/22 inaonyesha katika mechi 15 za nyumbani za Azam FC, ni mechi moja tu siku ya mwisho ya msimu ndiyo itachezwa saa kumi jioni. Na hii ni kwa sababu siku hiyo timu zote zitacheza wakati mmoja!

Mechi zingine zote za nyumbani za Azam FC zitachezwa usiku saa moja na saa mbili na nusu. Na pia katika mechi 15 za nyumbani, Azam FC itakuwa na mechi nne tu za mwisho wa wiki. Mechi zingine zote za nyumbani za Azam FC zitafanyika katikati ya wiki.

Hii siyo sawa kwa mkakati wa kibiashara na ukuzaji wa jina chapa la klabu yoyote ile. Uwanja wa nyumbani ndiyo sehemu ambayo timu huitegemea kupata pesa za viingilio, lakini pia kujenga utamaduni wa watu kwenda viwanjani.

Mechi nyingi zinapofanyika usiku wa katikati ya wiki ina maana kwamba watu wengi hawatafika uwanjani. Miundombinu ya usafiri wa nchi yetu hasa Dar es Salaam na zaidi Chamazi hufanya kwenda uwanjani kuwa shughuli ngumu.

Mechi inayoanza saa moja usiku itaisha saa tatu usiku. Kutoka Chamazi saa tatu usiku kwa miundombinu yetu utafika nyumbani saa tano au sita. Kumbuka hiyo ni katikati ya wiki, ikiwa na maana kwamba siku inayofuata mtu anatakiwa kuwahi kazini. Haiwezekani!

Jibu rahisi kwa mtu huyo ni kutoenda uwanjani, na asipoenda maana yake klabu imekosa mapato. Lakini pili, mechi za nyumbani ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga kizazi cha kesho cha wanaokwenda viwanjani, yaani watoto wa sasa ambao ni wakubwa wa kesho.

Mechi inapofanyika usiku, mzazi gani atamruhusu mwanaye aende uwanjani? Kiusalama siyo sawa na hata kimasomo siyo sawa. Huyu mtoto anatakiwa aende shuleni kesho.

Kwa hiyo ratiba inawanyima mapato ya leo na ya kesho. Wakubwa wa sasa hawaji uwanjani na wakubwa wa kesho ambao wangejengewa mazingira kuanzia sasa na wanapeperushwa.

Hatukosoi uwepo wa mechi za usiku wala za katikati ya wiki, lakini ziwe na uwiano mzuri. Kuipangia timu moja mechi zote za usiku nyumbani tena katikati ya wiki siyo sawa.

Kuna siku Azam FC wakishtuka kwamba wanaponzwa na taa zao wanaweza kuzitoa ili wasipangiwe mechi za usiku. Nyumbani wacheze usiku tu. Ugenini saa nane mchana. Siyo sawa.

NYUMBANI AZAM FC 2021/22.

Jumanne Oktoba 19, 2021 vs Namungo FC - saa moja usiku.

Jumanne Novemba 2, 2021 vs Geita Gold - saa mbili na nusu usiku.

Jumanne Novemba 30, 2021 vs Mtibwa - saa moja usiku.

Alhamisi Desemba 9, 2021 vs Kagera Sugar - saa moja usiku.

Jumamosi Desemba 18, 2021 vs Mbeya City - saa mbili na nusu usiku.

Jumamosi Desemba 23 vs Ruvu Shooting - saa moja usiku

Ijumaa Februari 4, 2022 vs Dodoma Jiji - saa moja usiku.

Alhamisi Machi 3, 2022 vs Coastal Union - saa mbili na nusu usiku.

Jumapili Machi 6, 2022 vs Polisi Tanzania - saa mbili na nusu usiku.

Jumatano Aprili 6, 2022 vs Yanga - saa moja usiku.

Aidha, mechi ya raundi ya 22 dhidi ya KMC ambayo itakuwa mwezi wa tano, haijapangiwa tarehe lakini ratiba inaonyesha itachezwa saa moja usiku.

Jumanne Mei 31, 2022 vs Simba - saa moja usiku.

Jumanne Juni 7, 2022 vs Mbeya Kwanza - saa moja usiku.

Jumatatu Juni 13, 2022 vs Tanzania Prisons- saa moja usiku.

Jumapili Juni 19, 2022 vs Biashara United - saa kumi jioni.

Ni matarajio yangu kwamba msimu ujao kuona ratiba itakayokuwa bora zaidi ya hii.