Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 05Article 536566

Maoni of Wednesday, 5 May 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

MZEE WA UPUPU: Tusione aibu, tuanzie tuhuma za Asukile

MZEE WA UPUPU: Tusione aibu, tuanzie tuhuma za Asukile MZEE WA UPUPU: Tusione aibu, tuanzie tuhuma za Asukile

IJUMAA ya Aprili 30, 2021, nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile alitoa tuhuma nzito kwa wapinzani wao katika mchezo wa 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports, Yanga.

Akizungumza baada ya kipigo cha bao 1-0, Asukile alimlalamkia mwamuzi wa mchezo husika na kusema Yanga waliwatafuta wachezaji wa Prisons wawahonge Sh40 milioni. Asukile ni mchezaji mwandamizi ambaye amedumu na timu yake kwa zaidi ya miaka 10.

Anapotoka hadharani na kusema anayoyasema, ukilinganisha na mafunzo ya nidhamu ya kijeshi aliyonayo, ni lazima tuyape umuhimu malalamiko yake. Hii ni kwa sababu Tanzania tumekuwa na tabia ya kufunika kombe mwanaharamu apite kila zinapokuja tuhuma kubwa kama hizi.

Miaka ya mwanzoni wa 2000, Prisons iliwafukuza kwenye timu wachezaji wake watatu kwa tuhuma za kupanga matokeo dhidi ya moja ya timu kubwa hapa nchini. Kipa Amani Simba, mlinzi Lameck Sichula na kiungo Wolalf Mwamlima.

Lakini hili liliishia ndani ya klabu na Jeshi la Magereza, halikutoka nje.

Amani ambaye hakuwa askari, akaachwa aendelee na maisha yake. Sichula na Mwamlima ambao walikuwa maaskari wakarudishwa lindoni. Sichula akagoma na kuondoka zake, lakini Mwamlima akatii na kurudi lindoni, akapelekwa Tanga.

Miaka miwili baadaye, Mwamlima akasamehewa baada ya kuomba sana, akarudi kwenye timu. Bahati mbaya ni kwamba nahodha wa wakati ule, Seka Bgoya, hakuwa jasiri kama Asukile. Lakini sasa amepatikana nahodha jasiri ambaye amejitoa mhanga kusema kile ambacho nahodha mwenzake alikiogopa, tuanzie hapo!

Malalamiko kama haya yamekuwa yakitolewa na wachezaji wengi katika nyakati tofauti, lakini mamlaka zetu zimekuwa kimya.

Kisingizio mara zote kinakuwa ‘hakuna ushahidi’ hata pale wanaojitoa mhanga kufichua uchafu kama huu wanaposisitiza wanao.

Januari 27, 2020, kipa wa Yanga, Ramadhan Kabwili, alisema ‘live’ kwenye kipindi cha michezo cha East Africa Radio kwamba viongozi wa Simba walitaka kumhonga gari katika harakati za upangaji matokeo. Sasa ni zaidi ya mwaka hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Mwaka 2014, mchezaji wa zamani wa Azam FC, Moro United na Yanga, Nsa Job, akizungumza na Millard Ayo wa Clouds FC kwenye kipindi cha Amplifier alisema kuna klabu iliwahi kuwahonga na wachezaji wenzake ili wacheze chini ya kiwango. Lakini wakakaza na kushinda huo mchezo, ile klabu ikaja kudai fedha zao.

Job alitakiwa awe shahidi katika upelelezi kwenye sakata hilo, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa. Safari hii hili sakata lisipite kimyakimya.

Kwa kuwa Asukile amesema yalifanyika mawasiliano ya simu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) itusaidie kwenye hili.

Simu za watu kadhaa Yanga zikaguliwe kwa kina.

Siyo kwamba nawafundisha kazi Takukuru na mamlaka zingine, bali najaribu kuwasaidia ili kazi yao iwe rahisi kwa sababu hawa ndio watu wanaotaka sana katika masakata ya aina hii.

Kukalia nafasi za uongozi kwenye klabu za soka kuna presha kubwa mno inayoletwa na mashabiki na kuwafanya viongozi wautafute ushindi kwa gharama yoyote, ikiwemo michezo michafu kama hii.

Katika hali ya kushangaza, unaweza kukuta Asukile anahukumiwa yeye, tena hata bila kusikilizwa kwa kutoa kauli chonganishi au ya uzushi.

Yaani badala ya kumuona Asukile ni shujaa na tumtumie katika vita dhidi ya uovu, atageuka kuwa adui na mharibifu na kupewa jina baya ili ashughulikiwe. Kila mtu hapendi upangaji matokeo, lakini hayupo ambaye yuko tayari kupambana nao.

Niliwahi kuandika kwenye ukurasa huu mwaka jana chini ya kichwa cha habari, ‘VPL NA HARUFU YA MKASA WA ITALIA 2006’. Nilirejea mkasa wa Calciopoli au kashfa ya Calcio, yaani kashfa ya soka (kwa lugha ya Kitaliano, soka huitwa Calcio), ambao ulitokea 2006 baada ya kubainika Juventus ilikuwa ikihonga waamuzi na wachezaji wa timu pinzani.

Tuhuma za Juventus zilianza chinichini kama hivi, baadaye watu wakaanza kuweka wazi kidogokidogo na kufikia 2006 ukafanyika uchunguzi wa kina na kubainika kuwa ni kweli. Juventus wakavuliwa ubingwa wa msimu huo na msimu wa nyuma yake, na kushushwa daraja kabisa. Wenzetu waliona na wakachukua hatua, na kwa sasa hali inawezekana kuwa ni nzuri. Tuhuma kama hizi siyo za kuziacha zipite tu hivihivi. Baada ya malalamiko ya miaka nenda rudi, sasa tuache kufanya kimazoea, tuchunguze kwa kina na uchunguzi uwe mpana. Siyo tu kwa Tanzania Prisons dhidi ya Yanga, uchunguzwe mpira wote.

Hakika tutabaini mengi na makubwa zaidi ya haya kwa sababu watu wameshajenga himaya kubwa sana kutokana na kuhisi wapo katika dunia yao isiyo na mamlaka. Tuchunguze...tuchunguze...tuchunguze!

Join our Newsletter