Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2020 03 26Article 498898

Maoni of Thursday, 26 March 2020

Columnist: mwananchi.co.tz

Mambo ya kuzingatia unapofikiria kazi ya ziada

Mambo ya kuzingatia unapofikiria kazi ya ziada

Siku hizi si ajabu kusikia mfanyakazi ana kazi zaidi ya moja. Teknolojia, kwa mfano, imetengeneza majukwaa yanafanya iwe rahisi kwa watu kufanya kazi nyinginezo za kuwaongezea kipato nje ya ajira.

Mtu anaweza kuwa ameajiriwa kama mhasibu wa taasisi, lakini wakati huo huo ni mkaguzi wa mahesabu wa kampuni nyingine.

Mifano ipo mingi. Wapo wanaotumia muda wao wa ziada kufanya biashara, kutoa ushauri wa kitaalamu na kutoa huduma nyinginezo kwa malipo.

Je, kuna mambo gani ya kuzingatia mfanyakazi anapofikiria kujiingiza kwenye kazi hizi za ziada? Hapa ninakuletea maswali manne ya kujiuliza.

Kwa nini unahitaji kazi za ziada?

Watu hutofautiana malengo wanapofanya kazi za ziada nje ya ajira. Wengine hutafuta namna ya kujiongezea kipato. Hawa ni wale wanaoona kama ajira zao haziwapatii kipato kinachotosha kuendesha maisha yao.

Pia Soma

Advertisement
Lakini wakati mwingine watu hutafuta kazi za ziada kukabiliana na kutokutabirika kwa ajira.

Unapokuwa na shughuli ya kufanya nje ya ajira inakusaidia kujiandaa na maisha ya baada ya ajira na hivyo kukuondolea hofu pale inapotokea kazi imekoma pasipo matarajio.

Pia, wapo wanaofanya kazi hizi kwa minajili ya kujifunza ujuzi mpya unaowasaidia kuboresha utendaji wa kazi. Katika mazingira ambayo ajira kuu haikusaidii kukua kiujuzi, kazi unazofanya nje ya ajira zinaweza kukusaidia kukuza uwezo wako wa kiutendaji.

Katika kufikiri sababu za kuwa na kazi nje ya ajira, ni muhimu kuangalia mazingira ya ajira yako kwa jicho la kazi unayotaka kuifanya. Je, unachotaka kukifanya kinaweza kukupa muda wa kuendelea na majukumu yako ya msingi kazini? Kazi ya ziada inapoingilia ajira yako, kazi hiyo inaweza kukuleta hasara badala ya faida.

Unajengaje kazi yako ya ziada?

Baada ya kuchagua aina ya kazi ya ziada unayoweza kufanya, kinachofuatia ni kufikiri namna bora ya kuifanya.

Kuna kazi ambazo kwa jinsi zilivyo ni rahisi kuzifanya na kuziendeleza. Mfano kuendesha teksi au bodaboda baada ya saa za kazi, inaweza kuwa rahisi madam una chombo cha usafiri na muda unao.

Lakini unapoanzisha biashara ya kuuza bidhaa au ujuzi (usadi), ni wazi utahitaji muda wa kujenga uhusiano na wateja. Ili ufike kiwango cha kuona tija yake utalazimika kutumia muda mwingi kukidhi mahitaji ya wateja.

Wakati mwingine kazi hizi huambatana na makataa (deadline) yanayoweza kukunyima amani. Kazi kama hizi zitadai umahiri katika kupangilia majukumu yako na nidhamu kubwa ya muda.

Unawezaje kuigeuza kuwa kazi kuu?

Ndoto ya wengi wanaoanzisha kazi za ziada ni pamoja na kukuza kazi hizo kuwa kazi wanazoweza kuzitegemea baadae. Ili hili liwezekane, tafiti zinaonyesha ni muhimu kazi hiyo iwe kweli unaipenda, inaendana na vipawa vyako, ujuzi wako kuliko ajira yako kuu.

Hata hivyo, changamoto ni kwamba taasisi na kampuni nyingi zinaweza kuwa na sera zinazowazuia wafanyakazi wake kufanya kazi za ziada zinazoleta mgongano wa kimasilahi, kuchukua muda zaidi wa mfanyakazi hali inayoweza kutafsiriwa kama kwenda kinyume na mkataba. Muhimu kujiridhisha kuwa unachokifanya hakivunji mkataba ulionao na mwajiri wako.

Hata katika mazingira ambayo kazi ya ziada haiendi kinyume na mkataba wa ajira, mara nyingi kuweka wazi kazi hizo kwa wafanyakazi wenzao na viongozi wao wa kazi inaweza kukuingiza kwenye matatizo yasiyo ya lazima.

Unapofanya uamuzi wa kusema au kunyamaza ni muhimu kutathmini mazingira yako ya kazi kuona kama ni salama kuweka wazi ‘mapambano’ yako ya nje ya ajira.

Mahali pa kuanzia ni kujiuliza, je unawajua wafanyakazi wengine walioweka wazi shughuli zao? Uhusiano wako na msimamizi wako, mkuu wa idara ukoje? Je, wanaweza kuendelea kukuamini wakijua kuna kazi nyingine za ziada unazozifanya wakati mwingine zikifanana na majukumu ya ajira yako ya sasa.

Unakabiliana vipi na changamoto?

Pamoja na faida nyingi unazoweza kuzipata kwa kuwa na kazi za nje ya ajira, ni muhimu kujiandaa na changamoto kadhaa.

Kwanza, ni namna unavyoweza kuendelea kuwa na ufanisi ule ule kazini. Fikiria mazingira ambayo unalazimika kufanya kazi za ziada usiku au siku za wikiendi. Je, unapata muda wa mapumziko?

Suala la pili ni namna gani kazi ya ziada inakuza ajira uliyonayo. Je, unachokifanya nje ya ajira kinakusaidia kuwa bora zaidi kazini? Mfano ofisa biashara anayefanya kazi ya kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wateja binafsi anapata ujuzi wa kuimarisha ajira yake?

Je, kipato kidogo unachopata nje ya ajira yako kinakuza kujiamini kwako kazini, au ndio kwanza kinakufanya usionekane kazini?

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya Simu: 0754870815Join our Newsletter