Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 26Article 539944

Maoni of Wednesday, 26 May 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Manufaa ya kiuchumi ufyekaji mimea vamizi Hifadhi ya Ngorongoro

Manufaa ya kiuchumi ufyekaji mimea vamizi Hifadhi ya Ngorongoro Manufaa ya kiuchumi ufyekaji mimea vamizi Hifadhi ya Ngorongoro

“TUMEKUSANYIKA hapa kwa sababu moja ambayo ni kuunganisha nguvu si tu kuokoa mazingira yetu, bali kuokoa uchumi wa nchi yetu; janga hili si la sekta moja; kama tulifanya makosa huko nyuma kushughulikia jambo hili tuache, sekta na taasisi zote zifanye kazi kwa pamoja kwa kupeana taarifa na mikakati ya kukabiliana na changamoto hii ya viumbe vamizi ambayo sasa ni janga la kitaifa.

Ndivyo alivyosema aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sasa ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Septemba 28, 2018, katika uzinduzi wa kikosi kazi cha kutatua changamoto za viumbe vamizi.

Kikosi kazi hicho kililenga kuchambua kwa kina utafiti na miradi mbalimbali ili kupata ufumbuzi wa tatizo la kuwepo kwa viumbe wageni nchini ikiwamo mimea hiyo kunakoathiri sekta za kiuchumi zikiwamo utalii, usafirishaji, kilimo, mifugo na nishati itokanayo na maji na uvuvi.

Akiwa Makamu wa Rais wakati huo, Samia alitaka hatua za makusudi zichukuliwe kukabiliana na janga hilo ili kuokoa mazingira na uchumi wa nchi.

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakati huo, January Makamba, alisema kuundwa kwa kikosi hicho kulitokana na mapendekezo ya mkutano uliofanyika Arusha Septemba 4, 2018 likiwa ni agizo la Makamu wa Rais.

Katika kikao hicho Makamba anasema, ilibainika kuwa, moja ya malalamiko ya wafugaji, wakulima na wavuvi ni kuwepo kwa baadhi ya mimea vamizi katika maeneo yao.

“Tishio kubwa la Hifadhi ya Ngorongoro ni kuwepo kwa mimea ambayo wanyama hawawezi kuila na si hapo tu, bali hata katika Hifadhi za Serengeti na Saadan hali iko hivyo pia,” akasema Makamba.

Kutokana na kuwapo kwa mimea vamizi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, hivi karibuni, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk Freddy Manongi, aliwaongoza watumishi wa mamlaka hiyo kufanya operesheni maalumu ya kufyeka mimea vamizi ambayo imeathiri maeneo mbalimbali ya eneo la hifadhi.

Katika Operesheni hiyo, Dk Manongi anasema mimea vamizi ya aina mbalimbali imeathiri maeneo ya ndani ya hifadhi hususan maeneo ya Ndutu, Olduvai na eneo la Kreta ya Ngorongoro ambalo takribani hekta 5000 sawa na asilimia 22 ya eneo lote la Kreta, limeathiriwa na mimea hiyo.

Dk Manongi anasema pamoja na kazi hiyo kuwa imekuwa ikifanyika miaka yote, bado mimea hiyo imekuwa ikiongezeka kutokana na kuwapo kwa mvua nyingi hasa za mwaka jana (2020).

Kwa mujibu wa Kamishna Manongi, ofisi yake imeamua kushirikisha wadau mbalimbali wa uhifadhi ili kukabiliana na changamoto hiyo haraka zaidi.

“Tumeamua ofisi ihamie hapa kwa muda ili watumishi wote washiriki kazi hii maalumu; utaona kuwa karibu asilimia 22 ya eneo lote la Kreta ya Ngorongoro limepata athari ya mimea hii ambayo imeongezeka sana kutokana na mvua nyingi na za muda mrefu za mwaka jana,” anasema Dk Manongi.

Anaongeza: “Tutaweka kambi hapa kwa zaidi ya wiki mbili ili kuhakikisha tunapunguza ama kumaliza kabisa tatizo hili.”

Kamishina huyo wa NCAA anasema kampeni hiyo inashirikisha watu zaidi ya 700 wakiwamo watumishi zaidi ya 250 wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, wakufunzi na wanafunzi 320 kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapri (MWEKA).

Wengine wanaoshirika katika kazi hiyo muhimu ni askari wa mafunzo zaidi ya 30 kutoka Shirika la Palm Foundation, vibarua 115 kutoka Wilaya ya Karatu pamoja na wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi.

Kaimu Kamishina Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Idara ya Wanyamapori na Nyanda za Malisho, Vicktoria Shayo, anasema uwepo wa mimea vamizi katika Eneo la Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro unasababishwa na mambo mbalimbali.

Anayataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, vifaa vya ujenzi, mazao kama mahindi na mifugo inayoingia ndani ya hifadhi.

“Vitu hivi na vingine kwa pamoja, huchangia uwepo wa mimea vamizi katika hifadhi,” anasema Vicktoria.

Anaitaja mimea vamizi iliyopo katika eneo hilo kuwa ni pamoja na ‘Bidens schimperi’, ‘gutenbergia cordifolia’, ‘Datura’, ‘stramonium’ na ‘argemone Mexicana.’

Kwa mujibu wa Vicktoria, njia za kitaalamu zinazotumika kuangamiza mimea hiyo ni pamoja na kufyeka na kuichoma.

Anaongeza kuwa katika maeneo ambayo mimea hiyo imefyekwa takribani wiki 3 zilizopita zimeonekana kuwa na matumaini kwa kuwa tayari wanyama mbalimbali wakiwamo swala, pundamilia na pofu wameanza kurejea katika maeneo hayo kwa kuwa nyasi sasa zinaonekana na zinawavutia wanyama kuziona na kuzila.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamishina Msaidizi Mwandamizi huyo, tangu operesheni ya kukata mimea vamizi ianze katika eneo la Kreta ya Ngorongoro takriban wiki mbili zilizopita, tayari zimefyekwa hekta zaidi ya 163 sawa na ekari 407.5 zikiwa ni sehemu ya ekari 5000 zinazohitaji kufanyiwa kazi ambapo kazi hiyo bado inaendelea kwa kasi.

Uchunguzi wa mwandishi wa makala haya umebaini kuwa, NCAA sasa inapanga kuongeza mashine maalumu za kusaidia kufyeka mimea hiyo ili kazi hiyo ikamilike kabla ya mimea vamizi hiyo haijakomaa na kudondosha mbegu.

NCAA imepanga kuendeleza juhudi hizo bila kuchoka kwani uwepo wa mimea vamizi katika hifadhi hiyo, unaweza kuathiri mipango endelevu ya uhifadhi, hivyo kuigharimu mamlaka fedha nyingi kurejesha hali ya kawaida.

Hii ni kwa kuwa kuathirika kwa mipango hiyo endelevu ya uhifadhi katika eneo hilo ni hatari kwa sekta ya utalii, mapato ya hifadhi na uchumi wa nchi kwa jumla.

Ikumbukwe kuwa, mimea vamizi hufunika nyasi hivyo kulazimisha wanyamapori kuhama kwa kuwa wanashindwa kuona nyasi na kuzila.

Hali hiyo, inaweza kusababisha ugumu katika upatikanaji wa wanyamapori katika eneo moja ambao ni kivutio cha utalii ndio maana NCAA imeamua kuendesha operesheni hiyo maalumu ili kurudisha maeneo yaliyoathirika katika uoto wa asili.

Mwandishi wa makala haya ni Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro (NCAA). Anapatikana kwa 0622629486.

Join our Newsletter