Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 13Article 537613

xxxxxxxxxxx of Thursday, 13 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Matumizi yasiofaa ya simu na mimba mashuleni

“KUIBUKA kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na vifaa vya mtandao vimegusa karibu kila nyanja ya maisha ya mwanadamu,” anasema Kenneth Simbaya, Mkurugenzi wa Shirika la YES-Tz linalotoa elimu ya afya kwa vijana kupitia michezo.

Simbaya anasema: “Simu za kiganjani (simumtelezo au simu janja) zimechukua nafasi ya kazi za kamera, kurekodi video, saa za dijiti na nyinginezo. Kwa mfano, inakuwa nadra sana kwa mtu kununua kamera ya dijiti kwa matumizi binafsi isipokuwa kwa sababu za kibiashara na wengine sasa hawanunui saa wala calculator.”

Anasema simu hizo ni kama kompyuta ndogo ya mfukoni na matumizi yake si tu ya kupiga na kupokea simu lakini zina vitu vya kushangaza kama vile kuvinjari matukio na taarifa mbalimbali, kuangalia michezo na habari, kutuma na kupokea barua pepe, kutazama video, kusikiliza muziki, kupiga na kusambaza picha na kupakua nyaraka mbalimbali zikiwemo za kitaaluma ambazo ni muhimu kwa wanafunzi.

Licha ya umuhimu wake kwa maisha ya sasa, Simbaya anasema simu za mkononi zinaweza pia kutumiwa katika tabia zisizofaa ikiwa ni pamoja na kuangalia picha na video zisizofaa zikiwemo za faragha na kuzisambaza kwa marafiki na watu wengine.

Anasema mara nyingi vijana hushindwa kutambua athari za muda mrefu za tabia zisizofaa.

Anasema simumtelezo zilipaswa kuwa nyenzo muhimu sana kwa wanafunzi kwa kuwawezesha kupakua masomo na kuwaunganisha wanafunzi wao kwa wao, kuwaunganisha na walimu pamoja watu wengine.

Hata hivyo anasema upande wa matumizi mabaya ya simu hizo umeleta changamoto kubwa katika jamii.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Rukwa, Abel Ntupwa anasema kilio kikubwa cha waalimu kuhusu simu za mkononi kwa wanafunzi ni kwamba huwasababishiausumbufu wakati wa masomo.

Anasema simu pia huwa kichocheo cha tabia zisizofaa ikiwemo ya kujiingiza katika vitendo vya ngono katika umri mdogo.

Anasema vitendo hivyo, siyo tu hukatisha ndoto zao masomo wanapoviendekeza au kupata mimba kwa wasichana, lakini baadhi yao kupata maambukizi ya magonjwa yatokanayona kujamiiana ukiwemo Ukimwi.

“Wanawake wanaopata ujauzito au kuanza kulea watoto katika umri mdogo wanapoteza fursa ya kuendelea na masomo na watoto wanaozaliwa na mama waliokosa elimu nao wanakuwa na nafasi ndogo ya kupata elimu. Hii ni changamoto kubwa sana,” anasema.

Anasema kwa mujibu wa takwimu, kipindi cha mwaka 2017 hadi 2019 wanafunzi wapatao 722 walipata mimba mkoani humo, matukio 171 yakihusisha wanafunzi katika shule za msingi na 551 katika shule za sekondari.

“Kwa kuwa tunaamini simu za mkononi huchangia madhara hayo kwa watoto wetu, tumepiga marufuku matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi wa shule zote mkoani Rukwa,” anasema.

Anasema marufuku hiyo inakwenda na adhabu kali kwa mwanafunzi atakayebainika kukutwa na simu ya mkononi, hivyo anawaomba wazazi nao ama wazuie matumizi ya simu hizo kwa vijana wao wawapo majumbani au wadhibiti matumizi yake.

“Utaratibu wetu wa kupima mimba wanafunzi wakati wa kufungua na kufunga shule umetupa somo kubwa sana. Uzoefu tulioupata unaonesha wanafunzi wengi hupata mimba wakati wa likizo. Hii inaashiria kuwepo kwa changamoto ya uwajibikaji wa wazazi na jamii katika malezi na ulinzi wa mtoto,” anasema.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo anasema kuendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ni moja ya mkakati wa miaka mitano (2020 hadi 2025) wa mkoa huo katika kukabiliana na mimba za utotoni.

Wangabo anasema takwimu za utafiti wa kidemografia za mwaka 2015 na 2016 zinaonesha kuwa asilimia 29 ya wanawake wenye miaka kati ya 15 na 19 mkoani humo ni wajawazito au wameshazaa. Kiwango hicho ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia 27.

Mbali na changamoto ya matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi, Mkuu wa Mkoa anataja sababu zingine zinazochangia mimba za utotoni mkoani mwake kuwa ni pamoja na elimu duni, hali ya umasikini kwa wananchi, kiwango cha juu cha uzazi na kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu.

Zingine ni mila, desturi na imani zinazomkandamiza mtoto wa kike, tabia ya ulevi kwa wazazi, malezi ya watoto na maadili ya jamii, uwajibikaji duni wa wazazi, jamii na viongozi, ukatili wa kijinsia, shinikizo rika, idadi ndogo ya shule za bweni na zinazotoa chakula na wanafunzi wa kike kupanga vyumba katika nyumba za watu binafsi na hosteli zisizo rasmi.

“Wasichana wengi wameingia katika masuala ya uzazi kabla ya muda stahiki kutokana na msukumo kutoka kwa watoto wa rika lao ambao wameanza mahusiano ya kimapenzi, matumizi ya pombe, dawa za kulevya huku simu za mkononi zikiwa ni moja ya kichocheo cha kuyafanya hayo yote,” anasema.

Pamoja na changamoto hiyo ya matumizi ya simu za mkononi, baadhi ya wanafunzi wa mkoa huo wanasema simu za mkononi zinawaongezea usalama kwani mbali na kuzitumia kupakua mambo mbalimbali ya kitaaluma, zinawawezesha kuwasiliana na watu wao wa jirani wakiwemo wazazi pale wanapokuwa na dharura.

“Ni kweli wapo baadhi ya wanafunzi wanaohitaji simu hizi kwa mambo yao binafsi yanayohusiana na masuala ya mapenzi hatua inayokatisha ndoto zao za elimu, lakini wengi wetu tunatumia kama moja ya kifaa kinachotuwezesha kujielimisha zaidi,” anasema mwanafunzi mmoja wa Shule ya Sekondari Matai wilayani Kalambo, Anna Mkemwa.

Anna anasema amekuwa akitumia simu ya mkononi anapokuwa nyumbani na kwamba inamwezesha kufanya majaribio mbalimbali ya masomo yake, kupata taarifa sahihi kwa wakati, kuongeza maarifa na uzoefu nje ya yale anayofundishwa darasani.

Anasema simu mtelezo ya wazazi wake imempunguzia gharama ya kununua kompyuta mpakato, na inamsaidia kuhifadhi taarifa zake mbalimbali na kuwasiliana na ndugu na jamaa.

Naye Jane Mwangoka anasema alianza kutumia simu ya mkononi akiwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Nkasi mwaka 2018.

Jane aliyekuwa akiishi katika nyumba ya kupanga, kilometa moja kutoka shuleni hapo anasema simu hiyo alikuwa akiitumia kwa kificho ikiwa ni pamoja na kucheza michezo mbalimbali ya kwenye simu na kufuatilia taarifa mbalimbali za mitandao ya kijamii.

“Hatua hiyo ilipunguza uwezo wangu wa darasani na wakati nikikaribia kumaliza kidato cha nne mwaka 2019 nilikuwa tayari nina ujauzito,” anasema na kushukuru Mungu kwamba alifanikiwa kufanya mitihani hiyo na kufaulu kwa kiwango cha daraja la nne.

Jane anasema baada ya kujifungua na kuanza kutaabika kumlea mtoto wake kwa msaada wa wazazi wake, hamu ya kurudi shule ili ajiendeleze kielimu imemrudia japokuwa hana msaada utakaomwezesha kutimiza ndoto hiyo.

Kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Norway (NORAD), Shirika la YES Tz kwa kushirikiana na asasi za PDF, RUSUDEO na Rafiki SDO kwa uratibu wa Plan International wameungana na wadau wengine kuusaidia mkoa wa Rukwa kutekeleza mkakati wa mkoa wa kukabiliana na mimba za utotoni.

Mratibu wa shirika hilo, Navina Mutabazi anasema wao kama YES Tz wamelenga kuwafikia vijana zaidi ya 32,000 wakiwemo wasichana zaidi ya 22,000 wenye miaka kati ya 10 na 20 ndani na nje ya shule za msingi na sekondari katika kata 36, vijiji 116 na shule 152 katika halmashauri za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga Vijijini.

Mutabazi anasema shirika lao linatambua pia kwamba nguvu ya teknolojia sasa hivi ipo sana kwenye mitandao ya kijamii ambayo hupatikana pia kupitia simu za mkononi.

“Kuna taarifa nyingi sana zinazorushwa kwenye hiyo mitandao ya kijamii zikiwemo za kuelimisha na zinazopotosha; vijana wenyewe wanalalamika kushindwa kuzichuja kujua zipi ni sahihi na zipi sio sahihi,” anasema.

Anasema katika mitandao hiyo ya kijamii, wazazi wanalamika kuwepo kwa taarifa za kupotosha zinazopokelewa vibaya na baadhi ya vijana; zikiwemo zile zinazofundisha aina na staili za kufanya mapenzi.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo Mutabuzi anasema wanafundisha elimu ya mawasiliano inayosaidia kuwawezesha vijana na makundi mengine katika jamii namna ya kupokea taarifa mbalimbali kupitia simu zao za mkononi na mawasiliano mengine na kuzifanyia kazi.

“Kwahiyo kwa kupitia kipengele hicho tunatarajia kuitatua changamoto hiyo kwa namna hiyo huku tukiwafundisha stadi mbalimbali za maisha, ubunifu na namna ya kuwa majasiri na wenye maaamuzi sahihi wanapopokea taarifa zinazoweza kuharibu maisha yako kupitia simu hizo,” anasema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Boniface Kasululu anasema mimba za utotoni ni miongoni mwa sababu zinazochangia vifo vitakanavyo na matatizo ya uzazi na vifo vya watoto wachanga na zina madhara mengine kiafya, kielimu, kiuchumi na kijamii.

Join our Newsletter