Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 07Article 555937

Maoni of Tuesday, 7 September 2021

Columnist: TanzaniaWeb

Mfahamu Jean Pierre Adams, Mwanasoka wa Ufaransa aliyepoteza fahamu kwa miaka 39

Jean-Pierre Adams Jean-Pierre Adams

Baada ya kupoteza fahamu kwa miaka 39, mwanasoka wa zamani wa Ufaransa, Jean-Pierre Adams, amefariki dunia akiwa na miaka 73.

Adams alizaliwa Machi 10, 1948 mjini Dakar Senegal, na akiwa na miaka 10 akahamia Ufaransa alikoenda kuishi na bibi yake aliyemchukua ili akamsomeshe dini ya ukatoliki.

Baadaye akaasiliwa na familia ya kizungu na kuwa raia wa Ufaransa.

Akaanza kucheza soka mtaani kwake na mwaka 1967 na akastaafu 1981 baada ya kuchezea vilabu kadhaa pamoja na timu ya taifa ya Ufaransa

Baada ya kustaafu akaanza kusomea ukocha mjini Dijon katika siku yake ya tatu ya kambi ya mafunzo, akapata majeraha ya kifundo cha mguu.

Akaenda mjini Lyon kwenye hospitali Édouard Herriot kuonana na daktari aliyefahamiana naye vizuri, kwa ajili ya matibabu.

Vipimo vikaonesha hayakuwa majeraha makubwa lakini katika mazungumzo na daktari huyo, akashauriwa afanyie upasuaji mdogo.

Akapangiwa kufanyiwa upasuaji Machi 17, 1982. Bahati mbaya kwake ni kwamba wakati huo kulikuwa na mgomo wa wafanyakazi kwenye hospitali hiyo, na kusababisha uhaba wa wahudumu.

"Mhudumu mmoja alihudumia wagojwa nane wa upasuaji", alikumbuka Bernadette katika moja ya mahojiano yake.

"Ni bora hata wangeniomba ushauri tuahirishe upasuaji kwa sababu haukuwa wa lazima, hakuwa katika hali mbaya". Alieleza Bernadette.

Jean-Pierre Adams akahudumiwa na daktari mwanafunzi ambaye alifeli mwaka mmoja uliopita na alikuwa anarudia mwaka.

Daktari huyu mwanafunzi aliyefeli na mhudumu aliyekuwa akihudumia wagonjwa nane kwa mkupuo, ndiyo waliomsababishia matatizo.

Mrija wa hewa kumsaidia kupumua wakati wa nusu kaputi, uliwekwa vibaya na kuziba njia ya hewa kwenye mapafu.

Akaishiwa hewa ya oksijeni kupatwa na shambuio la moyo.

Akapoteza fahamu na kulazwa hospitali miezi 15 mfululizo,

Serikali ya mji wa Lyon ikashauri aondelewe hospitali na kupelekwa kwenye kituo cha kulelea wazee.

Mkewe, Bernadette, akakataa na kumpeleka nyumbani alikoishi naye hadi umauti ulipomkuta Septemba 6 Mwaka huu.

Adams alianza safari ya soka katika klabu ya Entente BFN mwaka 1967, alidumu hapo hadi 1970 alipojiunga na Nîmes kisha Nice 1973, Mwaka 1977 akajiunga na PSG hadi 1979 alipohamia Mulhouse. Alidumu hapo hadi alipojiunga na Chalon alipostaafu soka.