Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 14Article 557377

Maoni of Tuesday, 14 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Mimi Mars afanye haya kusafisha nyota

Msanii wa Bongofleva, Mimi Mars Msanii wa Bongofleva, Mimi Mars

Mimi Mars ni mdogo wa aliyekuwa msanii wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee ‘Vee Money’. Hana umaarufu sana, lakini kwa wanaofuatilia muziki huo hawawezi kuwa na maswali juu yake.

Mbali na kufanya muziki na kuamua kuingia kwenye sanaa ya filamu baada ya kuonekana kwenye tamthilia ya Jua Kali, bado hajapata umaarufu mkubwa kama dada’ke, Vee Money.

Mwanadada huyo ambaye kwa sasa anafanya vizuri kwenye tamthilia hiyo kuna vitu anatakiwa kuvifanya ili awafanye Watanzania wamsahau Vee Money ambaye yupo Afrika Kusini.

Mimi Mars ndiye alikuwa msanii wa kwanza kusainishwa na Mdee Music na kuachia wimbo uitwao Sugar uliofanyika studio ya Barnaba, High Table Sound. Mdee Music tayari ina mafanikio ikiwa ni pamoja na kutoa albamu ya Vanessa ‘Money Mondays’ na EP ya Mimi Mars ‘The Road EP’.

Mwanaspoti inakuletea mambo matano yanayoweza kumsaidia Mimi Mars kufuata nyayo za dada’ke ambaye alikuwa ni miongoni mwa wasanii wa kike waliokuwa wanafanya vizuri ambao kwa sasa ni kama unashikiliwa na Nandy na Zuchu.

KOLABO KIMATAIFA

Hadi Vanessa anaacha muziki alikuwa amefanya kazi na wasanii wa kimataifa kama KO wa Afrika Kusini, Mr. P (P Square) wa Nigeria, Reekado Banks wa Nigeria na wengineo ambao waliweza kumtangaza kimataifa, lakini Mimi Mars hana kolabo yoyote ya kimataifa.

MATAMASHA

Vanessa alifanya shoo kubwa za kimataifa kama One Music Fest, lakini Mimi Mars hajawahi kufanya hata moja Tanzania na hata nchi ya karibu kama Kakamega, Kenya.

ALBAMU

Ikumbukwe kuwa Vanessa alijipigania na kutoa albamu ya kwanza Januari 15, 2018 iliyokwenda kwa jina la Money Mondays ikiwa na nyimbo 17.

Licha ya kushuhudia wasanii wengi wakitoa albamu kwa kipindi hicho, ni Vanessa pekee aliyeweka wazi mauzo ya albamu yake siku za mwanzo zilipotoka.

Wakati Vanessa anatangaza kukamilika kwa albamu yake ‘Money Mondys’, wiki mbili za mwanzo watu 1,500 walifanya ununuzi wa awali (pre order) wa albamu hiyo kwenye mtandao wa Boomplay Music.

NYIMBO KUMPA TUZO

Mwanadada huyo kutokana na ubora wake kwenye muziki wa ndani na nje alishinda tuzo kadhaa za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) wakati huo, hilo likampa fursa ya kushinda tuzo za All Africa Music Awards (AFRIMA) mara mbili.

Desemba 27, 2014 alishinda kama Best Female Artist in Eastern Africa. Pia Novemba 15, 2015 alishinda kipengele cha Best African Pop kupitia wimbo wake uitwao Hawajui.

Katika miaka yote ambayo Vanessa amechukua tuzo hizo alikuwa akishinda pamoja na Diamond Platnumz ambaye 2015 alishinda tatu vipengele vya Artist of the year, Best Male Artist in Eastern Africa na Best Song in Africa, lakini mdogo wake huyo hadi sasa hana tuzo hata moja licha ya kufanya muziki muda mrefu.

TOVUTI Vanessa alizindua tovuti inayofanya kazi ya kueleza kila kitu kuhusu maisha yake, huku ikitoa matukio ya kila ya kila siku ya staa huyo na ni mbunifu pia. Mwanzoni mwa 2018 alifungua programu ya Vee Money App ambayo ilitengenezwa Marekani. Mimi Mars hana hiyo kitu japo amejikita kwenye tamthilia.