Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2019 11 14Article 487552

Maoni of Thursday, 14 November 2019

Columnist: mwananchi.co.tz

Misuguano ya wasaidizi wa Rais humpa ugumu Magufuli

Misuguano ya wasaidizi wa Rais humpa ugumu Magufuli

Kuna siku ilibidi Rais John Magufuli aseme kazi ya kuteua na kutengua ni nzito mno, kiasi kwamba wakati mwingine hulazimika kulala na kuamka ili kutafakari na kufanya uamuzi.

Rais Magufuli alisema kuna siku alijadiliana na Katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi kuhusu jina la mtu wakakosa majibu. Akasema, aliaga kwenda kulala kupumzisha kichwa, aliporejea ofisini alikuta Kijazi naye aliondoka. Akauliza: “Sijui naye alienda kulala?”

Kauli hiyo ya Rais Magufuli inaweza kukupa tafsiri kuwa si kila ambaye yupo ofisini anamfurahisha, bali wengine wanapeta kwa sababu kazi ya kuwang’oa si ndogo. Huwaza jinsi ya kuwaondoa mpaka kichwa huuma.

Sasa basi, katika mazingira hayo kama ambavyo Rais mwenyewe aliyatamka, wasaidizi wake wanaingia kwenye malumbano ya mara kwa mara. Hapo bila shaka humwongezea uzito.

Mzani wa Serikali haupaswi kuonekana umelalia upande mmoja au kuyumbayumba. Watendaji hutakiwa kuonekana wanakwenda kama timu. Majibizano au malumbano ya wasaidizi wa Rais, huongeza uzani kwenye kitovu cha Serikali.

Wanafizikia wana kanuni ya kitovu cha uzani (principle of centre of mass), kwamba ili uzito ubebeke vizuri, inatakiwa kuuchukua kwenye makutano ya 0 kuelekea kila upande.

Katika mataifa mengine, kuna taasisi maalumu huundwa na kuitwa kitovu cha Serikali (CoG). Wajibu wa CoG huwa kumsaidia mkuu wa utawala kuiendesha Serikali.

CoG haifanyi kazi kama sehemu ya Serikali, bali majukumu yake ni kupitia utendaji wa mawaziri, makatibu wa wizara na watendaji wengine, kisha kumpa ushauri Rais namna ya kuwaongoza na kuiweka Serikali katika uzani sawa.

Ukweli ni kuwa mkuu wa utawala ndiye kitovu cha Serikali. CoG inakuwapo kuhakikisha Serikali inabebeka. Hivyo, Rais Magufuli ndiye kitovu cha Serikali.

Kwa vile ameshatamka kuwa kazi ya kutengua na kuteua ni ngumu, bila shaka ingetakiwa wasaidizi wake wawe watulivu, wafanye kazi kulingana na mwongozo waliopewa ili kitovu cha Serikali kisielemewe.

Kwa bahati mbaya kumekuwa hakuna utulivu miongoni mwa wasaidizi wake. Ukosefu huo wa utulivu unaweza kuutafsiri kuwa ni tendo la kukitesa kitovu cha Serikali ili kuufanya uongozi ubaki sawa bila kuelemea upande mmoja.

Yalishakuwapo malumbano kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Walishambuliana sana mitandaoni.

Hivi karibuni, Makonda aliagiza mchekeshaji maarufu Tanzania na mshindi wa Big Brother Africa 2015, Idris Sultan, aripoti kituo chochote cha polisi, Kigwangalla akatokeza na kuahidi kumwekea wanasheria Idris.

Hapo hakuna tafsiri nyingine zaidi ya Kigwangalla kumwonyesha Makonda kuwa alichokiamua hakikuwa sahihi. Wasaidizi wa Rais kuonyesha tofauti zao au misuguano hadharani ni kumpa wakati mgumu Rais ambaye ana kazi nyingi.

Siku zimepita kidogo, Makonda aliingia kwenye malumbano na naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mwita Waitara. Wanatumikia Serikali moja na tena wametokana na chama kimoja. Huwa hawaoni kama wanamwongezea uzito Rais kufanya uamuzi.

Makonda alipata kuingia kwenye msuguano na Waziri wa fedha na mipango, Philip Mpango. Hoja ilikuwa mgogoro wa kodi za samani zilizotajwa kuwa za msaada kwa walimu wa Dar es Salaam. Makonda alitaka ziruhusiwe kupita bila kutozwa kodi, Mpango alisisitiza zilipiwe.

Rais Magufuli akiwa mapumziko, Chato mwaka alilazimika kulitolea maelekezo suala hilo na kutaka samani hizo zilipiwe kodi. Tamko la Rais lilimaliza malumbano.

Yalishakuwapo malumbano mengine kati ya Kigwangalla na January Makamba, kipindi akiwa waziri wa muungano na mazingira katika ofisi ya makamu wa Rais.

Hoja ilihusu mpango wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha mradi wa magari ya nyaya kupanda Mlima Kilimanjaro.

January alimwambia Kigwangalla kuwa ingebidi mradi huo uthibitishwe na watu wa mazingira ofisini kwake. Hilo likaibua zogo mitandaoni baiana ya wawili hao.

Pamoja na Kigwangalla kutoa ufafanuzi mitandaoni kuwa yeye na January walimaliza tofauti zao, mshangao ulikuwa mkubwa.

Mawaziri kulumbana mitandaoni si jambo la afya kwa nchi. Unaweza kuhoji hawakutani vikaoni katika Baraza la Mawaziri?

Mawaziri, wakuu wa mikoa na watendaji wengine, wakiwamo wakuu wa wilaya na wakurugenzi wanatakiwa kuonyesha wao ni timu, malumbano ya hapa na pale ni ishara kwamba timu ina mgawanyiko. Na hiyo ni kumpa ugumu mkuu wa timu.

Watendaji wa Serikali wanapaswa kuonyesha wao ni timu na wanalo eneo la kuwasilisha tofauti zao na kupata ufumbuzi, badala ya kulumbana mitandaoni. Muhimu ni kuheshimiana.

Hata kama mwenzako kakosea, tumia njia sahihi ya kumfikishia makosa yake au kumripoti ngazi za juu. Kuna waziri mkuu, makamu wa rais kabla ya Rais.

Watendaji wa Serikali kulumbana mara kwa mara mitandaoni ni kukosa nidhamu kwa Serikali na mamlaka za juu. Ni kukifanya kitovu cha Serikali kuyumba kwa uzito kuelemea upande mmoja.