Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 21Article 543586

Maoni of Monday, 21 June 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Mlioaminiwa uteuzi onesheni uwezo kiutendaji, uadilifu

Mlioaminiwa uteuzi onesheni uwezo kiutendaji, uadilifu Mlioaminiwa uteuzi onesheni uwezo kiutendaji, uadilifu

JUZI Rais Samia Suluhu alifanya uteuzi wa wakuu wa wilaya kwa kuteua wapya, kuhamisha na kuwaacha wengine waliokuwa katika nafasi hiyo.

Huu ni mwendelezo wa kazi ya kupanga timu ya watendaji, wasaidizi na wawakilishi wake anaoamini watamsaidia kwa dhati kuendesha gurudunu la maendeleo kwa Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inahitaji kukimbia kimaendeleo ili kufikia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Uteuzi wa wakuu wa wilaya ulitanguliwa na uteuzi wa mawaziri na naibu mawaziri, katibu wakuu na naibu katibu wakuu na wakuu wa mikoa achilia mbali wakurugenzi wa taasisi na mamlaka mbalimbali.

Sisi tunampongeza Rais Samia kwa kuendelea kupanga timu anayoamini ina uwezo na itamsaidia kwa dhati na hilo ndilo tunaloomba litokee.

Aidha, tunampongeza Rais kwa kufanya mchanganyiko mzuri wa wasaidizi wake akihusisha watu wa jinsia zote, umri tofautitofauti wakiwamo vijana na wazee na pia, watu wa vipaji na taaluma mbalilmbali. Hili ni jambo la kupongeza.

Wakati tukimongeza Rais kwa kuendelea kupanga timu yake sawia, tunawapongeza wote ambao Rais kwa ‘macho yake yote’ amewaona na kuwaamini kuwa wana uwezo na ni wazalendo kwa taifa hivyo, watachapa kazi si kwa manufaa yao, bali kwa maslahi ya taifa.

Ndiyo maana tunasema: “Hongera sana wateule wote wa Rais.” Hata hivyo, kuwakumbusha wateule wote kuwa, hawana budi kumshukuru Mungu kwa imani ya Rais kwao, miongoni mwa mamilioni ya Watanzania.

Tunasema hivyo tukiamini kwa dhati kuwa, imani na heshima hiyo kubwa aliyowapa Rais kwa kuwateua kumsaidia, ni ‘deni alilowakopesha’ akitegemea walilipe kupitia utendaji bora uliotukuka na unaozingatia watu na utu, maadili na weldi katika kazi.

Ndiyo maana tunasema, walioteuliwa na rais watende kazi kwa kujinyenyekeza kwanza kabisa kwa Mungu, pili kwa mamlaka ya uteuzi wao (Rais) na wasaidizi wa mamlaka hiyo na pia, watende kwa ufanisi huku wakijinyenyekeza kwa wananchi wanaowakilishwa na mkuu wa nchi (Rais).

Tunasema hivyo tukitoa mfano kuwa, Rais Samia na Watanzania kwa jumla hawatarajii kuona anakuwapo mteule anayejigeuza kuwa Mungu na kwenda kinyume cha miongozo, ilani na mipango, sera na sheria za nchi.

Rais na Watanzania wote hawatarajii kumuona kiongozi yeyote hata kama ni kijana au mzee, anajigeuza ‘mungumtu’ na kuwanyanyasa wananchi au kushiriki mambo yoyote kinyume na maadili ya kazi na jamii na pia, hatutajii kuona mteule yoyote wa rais anakengeuka na kufanya mambio akilenga kujinufaisha.

Tunasema, huo utakuwa ni usaliti kwa rais na kwa Watanzania.

Ndiyo maana tunasema, Mlioaminiwa na kuteuliwa na Rais Samia onesheni uwezo kiutendaji na kiuadilifu kwa kutimiza majukumu yenu kipasavyo na kwa weldi, bila kusubiri kazi zenu zifanywe na viongozi wa juu yenu.