Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 02Article 555103

Maoni of Thursday, 2 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Mshahara wa Ronaldo, Sancho, Varane unalipa timu kibao za England

Mshahara wa Ronaldo, Sancho, Varane unalipa timu kibao za England Mshahara wa Ronaldo, Sancho, Varane unalipa timu kibao za England

MANCHESTER United ni chama kubwa. Kwenye dirisha la majira ya kiangazi lililofungwa juzi Jumanne, miamba hiyo ya Old Trafford imefanya kufuru kubwa kwenye usajili.

 Na sasa mashabiki wa timu hiyo ni kicheko tu, wakiamini timu yao ina kikosi cha kibabe kitakachokuwa na uwezo wa kushindania ubingwa kwenye Ligi Kuu England.

Uhamisho wa Jadon Sancho na Raphael Varane wenyewe tu tayari uliibua mzuka mkubwa kwa mashabiki huko Old Trafford kabla ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kuwapagawisha kabisa kwa kumleta mshindi mara tano wa Ballon d’Or, Cristiano Ronaldo.

Mastaa hao watatu wanakuja kuongeza mzuka kwa wachezaji wengine kwenye kikosi hicho na Solskjaer amewaaminisha mashabiki kwamba sasa kazi imeanza kwenye kumaliza ukame wa mataji.

Man United haijabeba taji lolote tangu iliponyakua Europa League mwaka 2017, huku mara ya mwisho walipobeba ubingwa wa Ligi Kuu England ni miaka minane iliyopita, kipindi hicho walipokuwa chini ya Sir Alex Ferguson.

Kuna mastaa wenye vipaji vya juu ambao kwao imekuwa kawaida kunasa mataji si kitu unachoweza kukipata kwa gharama nafuu, ambapo kwa usajili wote wa wakali hao Sancho, Varane na Ronaldo waliogharimu ada ya jumla ya Pauni 135 milioni. Hiyo nje ya mshahara watakaolipwa wakali hao.

Supastaa wa zamani wa Real Madrid na Juventus, Ronaldo ndiye atakayekuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi huko Old Trafford, akiripotiwa kwamba mshahara wake utakuwa Pauni 510,000 kwa wiki, wakati mchezaji mwenzake wa zamani wa huko Los Blancos, Varane analipwa Pauni 340,000 kwa wiki.

Sancho yupo katikati yao, akilipwa mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki, ikiwa ni pesa nyingi tofauti na alivyokuwa akilipwa Borussia Dortmund. Mshahara wa Sancho uliibua mjadala kama anastahili kulipwa kiasi kikubwa hivyo.

 

Lakini, kwa kuzingatia takwimu za supastaa huyo wa England kwa alichokifanya huko kwenye Bundesliga – akifunga mabao 50 na kuasisti mara 64 katika mechi 137 alizoitumikia BVB, anastahili.

Kwa kujumlisha mkwanja wote wanaolipwa mastaa hao wote watatu kwa mwaka, Man United inatoa Pauni 62.4 milioni kwa mshahara wa Sancho, Ronaldo na Varane peke yao.

Kwa ukubwa wa pesa hiyo, yani mshahara wa wachezaji hao watatu tu, unazidi mishahara ya vikosi vizima vya timu 13 nyingine kwenye Ligi Kuu England kwa bili yao ya mishahara kwa mwaka.

Mabingwa wa Kombe la FA, Leicester City bili yao ya mishahara kwa kikosi kizima kwa mwaka ni Pauni 58.5 milioni, wakati West Ham United, bili yao ni Pauni 57 milioni. Hii ina maana, mshahara wa Sancho, Ronaldo na Varane kwa mwaka, unalipa kikosi kizima cha Leicester na chenji inabaki.

 

Man United mshahara inayowalipa mastaa hao watatu pekee kwa mwaka, unaweza kuilipa Brentford, iliyoichapa Arsenal kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu England kwa miaka mitano.

Bili ya mishahara ya Brentford ambayo imepanda daraja msimu huu, kwa mwaka wanalipa mishahara ya Pauni 12.8 milioni kwenye kikosi chao cha wachezaji 25.