Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 24Article 559411

Maoni of Friday, 24 September 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Msiingize siasa chanjo dhidi ya Covid-19'

Msiingize siasa chanjo  dhidi ya Covid-19' Msiingize siasa chanjo dhidi ya Covid-19'

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, amewataka wataalamu wa afya kuacha kuingiza siasa katika kupeleka elimu ya kuhamasisha chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 kwa wananchi.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa kikao cha tathimini ya utoaji wa chanjo ya Covid-19 kwa wananchi wa mkoa huo. Alisema kuwa lengo la serikali ni kudhibiti maambukizi mapya hivyo chanjo hiyo ni vema walengwa wakaipata.

"Wataalamu wa afya kama mmeweza kuhamasisha wazazi kuna umuhimu wa kuchanja watoto wachanga, basi nendeni mkahamasishe watu umuhimu wa chanjo ili kuendelea kujikinga na ugonjwa wa Covid-19," alisema.

Aidha, aliwataka wanasiasa na viongozi wa dini kuendelea kutumia majukwaa yao kwa ajili ya kuelimisha wananchi kuona manufaa ya kuchanja ili kuendelea kujilinda na maambukizi mapya.

Akitoa takwimu za chanjo kwa mkoa huo, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Jonathan Budenu, alisema lengo ni kuchanja walengwa 390,000 lakini wameweza kufikia watu 10,939.

Alisema kuwa bado wanaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutoa chanjo katika maeneo yenye mikusanyiko kama shuleni, sokoni, kwenye misikiti, makanisa pamoja na vyombo vya usafiri.

Aidha, aliongeza kuwa ili kusogeza huduma ya chanjo ya Covid-19 kwa wananchi wameanza kutoa huduma hiyo katika ngazi ya msingi kwenye vituo vinavyotoa huduma ya chanjo nyingine.