Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 26Article 581161

Maoni of Sunday, 26 December 2021

Columnist: www.mwananchi.co.tz

Msongo wa mawazo, visasi chanzo ukatili wa watoto

Msongo wa mawazo, visasi chanzo ukatili wa watoto Msongo wa mawazo, visasi chanzo ukatili wa watoto

Kuna msemo wa wahenga unaosema uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Msemo huo umechukua sura tofauti baada ya kuripotiwa kwa matukio kadhaa ya ukatili dhidi ya watoto yaliyofanywa na mama zao wa kuwazaa.

Mfano wa matukio hayo ni pamoja na lile la Desemba 2, 2021 ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe aliripoti tukio la mwanamke aliyefahamika kama Veronica Gabriel (30), mkazi wa Kijiji cha Mwabagaru, Kata ya Buseresere, Wilaya ya Chato, mkoani Geita kuwanywesha sumu watoto wake watano kisha na yeye kunywa kwa madai ya ugumu wa maisha.

Tukio hilo lilisababisha vifo vya watoto wawili na waliobaki kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo mama huyo amenusurika kifo, licha ya kunywa sumu hiyo kwa madhumuni ya kujiua

Jeshi la Polisi mkoani Njombe, Septemba 15, 2021 lilitoa taarifa ya kumshikilia Vaileth Chaula (30), mkazi wa Kijiji cha Mkongomi Kata ya Kidugala wilayani Wanging’ombe kwa kosa la kumuua mtoto wake kwa kumkatakata na shoka kichwani ambapo taarifa hiyo ilisema kwa mujibu wa ndugu wa Vaileth, mwanamke huyo alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya akili.

Jeshi la Polisi mkoani Manyara Septemba 14, 2021 lilitoa taarifa ya kumshikilia Doto Vicent, mkazi wa Babati kwa tuhuma za kumchoma mtoto wa kike sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Desemba 7 mwaka 2020 mwanamke anayeitwa Regina Daniel (24), mkazi wa Louxmanda Manyara anatuhumiwa kuua watoto wake watatu kwa kuwalisha maembe yenye sumu inayodhaniwa kuwa ya panya.

Advertisement Akizungumzia athari za matukio hayo kufanywa na wanafamilia, mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya mahusiano na malezi kutoka Psychomotive Internation, Charles Kalungu alisema ukiachilia mbali matatizo ya afya ya akili, kuna sababu mbalimbali za kisaikolojia zinazoweza kumpelekea mzazi kumfanyia ukatili au mauaji mtoto wake. Alisema namna alivyompata mtoto huyo pia inahusika na ukatili anaokuja kumfanyia baadaye.

“Unaweza kukuta alipata ujauzito wa mtoto huyo kwa kubakwa, hiyo inaweza ikawa sababu ya kuwa na hasira kwa mtoto huyo, hivyo anapokosea humuadhibu hadi kuna muda hujikuta akipitiliza na kufanya ukatili,” alisema.

Alifafanua kuwa pia mzazi anaweza kufikia hatua hiyo kutokana na namna anavyotaabika katika malezi na ukuaji wa mtoto husika.

“Unakuta mama amepata taabu sana kumlea mtoto pengine bila hata msaada wa mtu yeyote katika kipindi hicho kigumu cha malezi, hivyo mtoto huyo anapofanya jambo ambalo labda amekuwa akilifanya mara kwa mara na kutomsikiliza mzazi wake pale anapomuonya, hupata hasira zinazojumuisha mahangaiko aliyopitia au anayopitia kumlea na kutaka akue katika maadili mema, hivyo kufanya kitu kibaya pengine asichokitarajia,” alisema.

Alisema pia jambo kama hili linaweza kusababishwa na visasi baada ya wazazi hao kuachana, kutokana na maumivu anayopitia akiunganisha na changamoto nyingine za kimaisha anaweza kumdhuru mtoto.

“Hali hii huweza kutokea kwa wanamume na wanawake,” alisema.

Kalungu alishauri kuwa ili matukio kama haya yapungue katika jamii ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha wanatatua migogoro yao binafsi au iliyopo baina yao ili kuepusha hali ya kuhamishia hasira kwa watoto.

“Wazazi hususan kina mama wanapaswa kuhakikisha kabla ya kuwaadhibu watoto wao wawape muda wa kuwasikiliza kwanza, ili kuepusha majuto baadaye,” alisema.

Pia, alisema ni muhimu kuwapo na dawati maalumu la wanasaikolojia kila kata ambapo kina mama watapatiwa huduma bure wanapofikwa na changamoto za kihisia au matatizo ya afya ya akili ili kuepusha madhara zaidi.

“Kuwe na semina za mtaa kwa mtaa ambapo kina mama pamoja na mabinti watashirikishwa vyema katika mafunzo rasmi ya malezi, kwani uwepo wa semina hizi utawapatia maarifa na majibu ya maswali ya kina wanayojiuliza kila siku bila majibu na kujikuta wanakuwa na hasra kali muda wote,” alisema.

Aliongezea kuwa elimu ya ziada inahitajika zaidi kwa kina mama, kwani wao ndio wanabebeshwa mzigo mkubwa, hasa katika upande wa malezi, ikiwemo kumlea mtoto na kumkuza, “Mama huyu akikosa msaada na kutelekezwa ni rahisi mno kuchanganyikiwa na kufanya maamuzi ya hovyo, maana wanawake wengi wana hisia za karibu, hususan za majonzi.

Kwa upande wa Mtaalamu wa Afya ya Akili, Dk Philimina Scarion kutoka Mental Health Tanzania, alisema matukio kama hayo husababishwa na na mhusika kuwa na matatizo ya akili (kuchanganyikiwa) au mrundikano wa msongo wa mawazo ndani ya kichwa chake bila mwenyewe kujua kama hayupo sawa.

“Watu wengi siku hizi wanasumbuliwa na msongo wa mawazo, hali inayosababisha kwa namna moja au nyingine kuwa na hasira kupindukia hata anapoudhiwa kwa kitu kitu kidogo,” alisema.

Alisema mtu akikosa mbinu sahihi za kukabiliana na msongo kitaalamu hujulikana kama ‘stress management’, hushindwa kuzuia hasira zake pale anapofanyiwa maudhi fulani na kujikuta amesababisha majeraha au kifo kwa mtu.

Aliongezea kuwa kwa mtu aliyepata tatizo la kuchanganyikiwa humsababishia kufanya matukio ya kikatili na kwa mujibu wa mtaalamu huyo, baadhi yao husukumwa na sauti wanazokuwa wakizisikia zikiwaamuru kufanya jambo fulani.

“Wakati wa matibabu kuna baadhi ya wagonjwa nikizungumza nao wananiambia kuna sauti zimekuwa zikiwashinikiza kufanya mambo fulani na kutokana na shinikizo la sauti hizo wanajikuta wamefanya hayo,” alisema.

Kwa upande wa matibabu, Dk Philimina alisema kuna aina mbili za matibabu ambayo hutolewa kulingana na hali ya mgonjwa.

“Matibabu hayo ni pamoja na mgonjwa kukutanishwa na mwanasaikolojia na kuzungumza naye, tiba hii kitaalamu hujulikana kama ‘stress and anger management’,” alisema.

Alisema matibabu ya pili ni dawa ambazo hutolewa na madaktari maalumu wa afya ya akili, kulingana na hali ya mgonjwa.