Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 26Article 553798

Maoni of Thursday, 26 August 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Mwisho wa ubishi, huku Diarra huku Manula

Mwisho wa ubishi, huku Diarra huku Manula Mwisho wa ubishi, huku Diarra huku Manula

KWA ubora wa makipa hawa sasa ni mwisho wa ubishi. Ndio kauli za mashabiki wengi wa Simba na Yanga wakati timu hizo zenye upinzani wa jadi zikijiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. Simba wanaamini baada ya kutwaa mataji ya Ligi ujio wa kipa mpya wa Yanga, Diarra Djigui utaongeza ushindani kwa kipa wa Simba, Aishi Manula ambaye amekuwa bora kwa takribani misimu mitano mfululizo.

Manula amekuwa bora kuanzia alipokuwa akiichezea Azam FC na hata alipojiunga Simba bado alihakikisha lango lake haliruhusu mabao mengi na kushikilia rekodi ya kipa ambaye hafungwi mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara.

Ujio wa Diara unaonyesha kabisa ni kipa mwenye uzoefu kutokana na kupita timu zote za Taifa pia kucheza mashindano makubwa ndani ya Afrika akiwa na timu ya Taifa ya Mali.

Mwaka 2015 kipa huyo alichaguliwa kikosi cha Mali chini ya miaka 20 kwenye mashindano yake, lakini alivunjika mkono katika mechi ya Ligi Mabingwa dhidi ya AS GNN na kujikuta akikosa mashindano hayo.

Mei 2015 alijumuishwa kwenye kikosi cha Mali chini ya miaka 20 kilichocheza fainali za Kombe la Dunia U-20 nchini New Zealand, pia akiwa nahodha katika mchezo dhidi ya Ujerumani walishinda kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Kipa huyo mwenye uwezo wa kudaka penalti akiwa na kikosi cha Mali walitolewa na Serbia hatua ya nusu fainali, lakini walimaliza nafasi ya tatu kwa kuifunga Senegal.

Amecheza mechi tatu akiwa na timu ya umri chini ya miaka 23 katika fainali za Mataifa Afrika.

TIMU KUBWA

Kipa huyo upande wa timu ya Taifa ya Mali aliitwa kikosi kilichocheza mechi ya kufuzu fainali za Mataifa Afrika 2016, katika raundi ya awali alicheza mchezo wake wa kwanza Julai 5, 2015 dhidi ya 3-1 wakiifunga Guinea-Bissau.

Pia alicheza mchezo dhidi ya Mauritania Oktoba 2018 wakishinda 2-1 na ushindi huo ukaifanya Mali kufuzu kwenye Fainali za Mataifa Afrika zilizofanyika nchini Rwanda.

Diarra hakuachwa kwenye kikosi cha wachezaji 23 na kuweka rekodi ya kucheza mechi tatu kwenye mechi sita, huku Mali wakifika fainali na kupoteza mbele ya DR Congo 3-0.

Mali licha ya kushindwa kuchukua kombe hilo, Diara alikuwa katika kikosi bora cha mashindano cha wachezaji 11 akiwa upande wa wachezaji wa akiba.

Pia alikuwa mchezaji bora wa mwaka kwenye Ligi Kuu ya Mali akiwa na kikosi cha Stade Malien msimu wa 2014-2015.

Kwa upande wa Manula amekuwa na misimu minne bora akichukua tuzo ya kipa bora wa msimu mara zote, mara tatu akiwa na Simba na mara moja akiwa kwenye kikosi cha Azam FC.

Manula pia alikuwa sehemu ya mafanikio kwenye kikosi cha Simba baada ya kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia tangu ajiunge Simba 2017 amechukua ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo huku akiwa ndiye kipa namba moja kwenye kikosi hicho na kujenga imani kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Manula alikuwa katika kikosi cha Taifa Stars kilichocheza fainali za Mataifa Afrika 2019 nchini Misri akicheza mechi mbili na timu ya Tanzania ilitolewa katika hatua ya makundi.

Manula alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioipa Simba mafanikio ya kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018/19, msimu wa 2019/20 waliishia raundi ya awali wakitolewa na UD Songo ile yaLuis Miquissone kabla ya msimu wa 2020/21 kurejea makali yao na kufika tena robo fainali.

WASIKIE WADAU

Kocha wa makipa wa zamani wa Yanga, Juma Podamali alisema; “Sijamuona udakaji wake huyo Diarra, ligi ikiianza hadi akicheza mechi tatu ndiyo itajulikana ubora wake. Hata kwenye mechi ya Simba na Yanga kama itakuwa ni mechi yake ya kwanza tusijaji, ila baada ya mechi tatu hawezi kutuongopea.”

“Kwa hapa nchini Manula hana mpinzani, yeye ndiye Tanzania One wetu kwa sasa na hilo halina ubishi,”alisema Pondamali.

Kipa gwiji, Mosses Mkandawile alisisitiza; “Manula ana uzoefu, uwezo na amecheza mechi nyingi za kimataifa ambazo zimemjenga, huyu wa Yanga, pamoja na kwamba ana CV nzuri, lakini hata kina Sarpong walikuja na CV bora.”