Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 03Article 561025

Maoni of Sunday, 3 October 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

NYUMA YA PAZIA: Erling Haaland anacheka ndani na ya uwanja

Erling Brut Haaland Erling Brut Haaland

Mino Raiola anaongea lugha saba. Kiitaliano, Kiingereza, Kijerumani, Kispaniola, Kifaransa, Kireno na Kidachi. Sijui atakuwa anaongea lugha gani kwa sasa na mteja wake anayeitwa Erling Brut Haaland ambaye ni raia wa Norway aliyezaliwa Leeds - Uingereza.

Wana dili ya maisha yao mezani. Haaland, nadhani unamjua. Jina lake kwa sasa linamaanisha mabao. Kuna tofauti ndogo ya kutofautisha jina lake na mabao. Ukisema mabao unamaanisha Haaland. Ukisema Haaland unamaanisha mabao.

Wapo kina Harry Kane, Roberto Lewandoski, Luis Suarez na wengineo. Lakini katika umri mdogo Haaland anashangaza kidogo. Inatokea mara chache chezaji kukomaa akiwa katika umri mdogo.

Msimu huu tayari ana mabao 13 katika mechi 10 tu alizovaa jezi za Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Norway. Haaland ana moto. Ana balaa. Huko Norway akiwa na umri wa miaka 21 tu amefunga mabao mengi kuliko mechi alizocheza. Katika mechi 10 ana mabao 13. Mabao huwa yanazidi mechi zake. Tunaomjua hatushangai.

Turudi mezani katika mazungumzo yao. Yeye na Raiola. Sijui mazungumzo yao yatafanyika wapi kati ya Dortmund au Miami ambako Raiola anamiliki jumba lenye thamani ya Pauni 8 milioni alilonunua mwaka 2016. Popote walipo watakuwa wanacheka kujadili biashara tamu iliyo mezani kwao.

Katika dirisha hili lililofungwa hivi majuzi, Haaland angeweza kuondoka kwa dau kubwa kwenda katika klabu yoyote kubwa Ulaya. Kulikuwa na kipengele cha majadiliano ya bei kati ya Dortmund na klabu ambayo ingemtaka. Kufikia Septemba mwakani, namaanisha Septemba 2022, Haaland ana kipengele ambacho kinamruhusu kuondoka Dortmund kwa dau la Euro 75 milioni tu.

Nimeweka neno ‘tu’ kwa sababu dau hilo ni dogo kwa mchezaji kama Haaland. Ni dau Arsenal wanamudu kulipa, Everton wanamudu kulipa hata Leicester City wanamudu kulipa. Kuna swali la kwanza linajitokeza kama tukienda kando ya topiki. Kwanini Dortmund waliruhusu waingie katika mwaka ambao Haaland anaruhusiwa kuondoka kwa dau dogo? Nilidhani kwamba ilikuwa lazima kwa Dortmund kumuuza katika dirisha la mwaka huu kwa sababu wangemuuza kwa bei wanayojisikia kuliko bei ambayo ipo katika mkataba ifikapo mwakani.

Labda wanataka Haaland awasaidie kutimiza malengo fulani. Labda ni malengo ambayo yatawapa pesa nyingi kuliko dau ambalo wangemuuza katika dirisha lililopita. Vyovyote ilivyo Dortmund wana akili timamu na wanajua watakachopata.

Na sasa maamuzi yao yanawapa faida Haaland na Raiola. Vikao vyao vitakuwa na vicheko vingi. Klabu yoyote ambayo itamtaka Haaland italazimika kumlipa mshahara mkubwa pamoja na kifuta jasho kizuri kwa sababu itakuwa wamempata Haaland kwa bei ya chini.

Wataambiwa kwa lugha nyepesi tu na Raiola. “Sikilizeni katika bei halisi ya sokoni kwa sasa Haaland anaweza kupatikana kwa dau la Pauni 160 milioni. Ana miaka 21 tu. Nyie mnampata kwa Euro 75 milioni tu. kingine kilichobaki tupeni sisi wenyewe.”

Kauli hii inamaanisha kwamba kufidia pesa ambazo klabu ingegharamika, basi ni bora pesa hiyo iende katika mshahara wa Haaland pamoja na kitita ambacho Raiola atataka. Kama hautaki basi. Ni kama tu inavyokuwa kwa wachezaji ambao wanaondoka bure baada ya kumaliza mikataba yao.

Mpaka sasa Raiola na Haaland wana turufu hii. Na unapokumbushwa kwamba dau la Harry Kane mwenye miaka 28 lilizidi Pauni 100 milioni na Tottenham Hotspurs wakagoma kumuuza kwenda Man City, inampa nguvu Raiola kudai mshahara mkubwa pamoja na pesa yake ya mfukoni kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 21 tu ambaye ni mfungaji hatari Ulaya.

Sio wawili hao, kumbuka kwamba kando yao kuna baba yake Haaland, Alf Inge Haaland ambaye amekuwa akijihusisha na dili za mwanaye kwa karibu. Baba mtu alikuwa staa wa zamani wa Leeds United na Manchester City. Anajua biashara ya soka ilivyo.

Kama ilivyo kwa baba wa Neymar, Neymar Senior au mama yake Adrien Rabiot, Veronika, Alf Inge ameacha kazi zake na kujishughulisha kumlinda mwanaye katika biashara ya soka. Hapana shaka atakuwa kando ya Haaland na Raiola katika biashara hii kubwa inayokuja.

Nani anaweza kumlipa Haaland mshahara mkubwa? Hili ndio swali kubwa. Dau la kumnunua wengi wanaweza kama nilivyosema hapo awali. Suala ni nani anaweza kumlipa mshahara mkubwa. Kwa dau hili wapo wengi wanaoweza kumlipa.

Sioni Chelsea wakiendelea kujishughulisha tena na Haaland kwa sababu tayari wameshampata Romelu Lukaku ambaye amekuwa akifunga vyema. Hauwezi kuwa na Lukaku na Haaland kwa wakati mmoja. Ukimpata mmoja unamuachia mwingine.

Manchester City? Inawezekana kwa kiasi kikubwa. Hawajaziba pengo la Sergio Aguero tangu aondoke. Wanatumia zaidi viungo kufunga mabao. Walimkosa Harry Kane katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto. Hata hivyo Pep Guardiola inabidi aamue jambo moja. Anaweza kuamua kurudi kwa Kane au kumfuata Haaland. Akienda kwa Kane basi ataachana na Haaland. Akienda kwa Haaland basi ataachana na Kane. Ni hali halisi ambayo inabidi waifuate. Labda kama unaweza kuwa na jambo la kumshauri Pep amchukue nani kati ya watu hawa wawili.

Kuna uwezekano pia Haaland akanaswa na dola nyingine za mafuta za PSG. Kule Kylian Mbappe amegoma kusaini mkataba mpya. kama Mbappe akiondoka kwenda Real Madrid kuna uwezekano mkubwa Haaland akaingia katika utatu wa yeye, Neymar na Lionel Messi. Real Madrid pia wanamtaka Haaland. Inaweza kunishangaza kidogo kama watawachukua Mbappe na Haaland kwa wakati mmoja. Labda kwa sababu Mbappe watampata bure. Hata hivyo watalazimika kulipa mishahara mikubwa kwa wakati mmoja ya Mbappe na Haaland.