Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 17Article 551899

Maoni of Tuesday, 17 August 2021

Columnist: Mwanaspoti

NYUMA YA PAZIA: Messi na tabasamu la pesa ndani ya Paris

Nyota mpya wa PSG, Lionel Messi Nyota mpya wa PSG, Lionel Messi

Uzunguni mwa Paris ataishi mgeni mpya kwa miaka miwili ijayo. Lionel Messi na familia yake. Mkewe Antonella Rocuzzo na watoto wake Thiago, Mateo na Ciro. Kwa sasa wapo hotelini, lakini baada ya muda mfupi watahamia uzunguni.

Ndipo ambapo Lionel Messi ameamua kwenda. Angekwenda wapi kwingine? Baada ya kutangaza kuondoka Barcelona wiki iliyopita alikuwa na miji miwili tu ya kuishi. Kati ya Paris au Jiji la Manchester ambalo mvua huwa haziishi. Miji hii miwili ndio ambayo ina pesa za Waarabu. Ilikuwa lazima Messi akacheze Paris au Manchester City kwa kocha wake wa zamani, Pep Guardiola. Nahisi kuna sababu ambazo zilimfanya asitamani kucheza City.

Inawezekana katika umri wa miaka wa miaka 34, Messi hakutaka kuingia katika mikiki ya soka la Kiingereza. Inawezekana katika umri huo hakuona sababu ya kujisumbua kuishi katika mji wenye mvua kama Manchester. Inawezekana pia Pep hakutaka kuwa na Messi, ingawa matajiri wake Waarabu lazima walimtaka. Tajiri gani, hasa mwarabu, hawezi kumtaka Messi?

Hatimaye ulikuwa uamuzi rahisi kwa Messi kwenda Paris. Jiji lenye kila kitu duniani. Mastaa wengi wanapenda kupita Paris. Maisha yanataka nini zaidi? Nadhani hata Antonella alivutika na jiji hilo huku Messi akivutika na kitita cha Pauni 650,000 kwa wiki ambacho kitakuwa kikiingia katika akaunti yake.

Ulikuwa uamuzi rahisi kwa Messi hasa ukizingatia kwamba kwanza ameondoka Barcelona bila ya lawama. Inadaiwa kwamba hakuna wa kulaumiwa kati ya Messi na Barcelona kufuatia kuondoka kwake. Ni kanuni tu za La Liga ndizo ambao zimewabana wote wawili. Walipambana sana kuhakikisha maisha yanaendelea kuwa kama yalivyo.

Ni katika upenyo huu Messi aliamua kwenda Paris na familia yake dakika chache baada ya kuangua kilio Camp Nou. Ghafla akapanda ndege akiwa na mkewe kisha wakatabasamu sana. Messi alikuwa na mengi nyuma ya tabasamu lake. Kwanza kabisa ni hizo Pauni 650,000 kwa wiki.

Wakati akiwa na Barcelona katika juhudi za kuokoa mpango wa kubaki alikubali kukatwa mshahara kufikia Pauni 250,000, lakini bado dili la kubaki lilishindikana. Kwa kwenda PSG bado mshahara wake umerudi kulekule kunakomfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi duniani.

Lile lilikuwa tabasamu la ushindi wa noti. Akiwa na Barcelona Messi alikuwa anafanya mambo mawili kwa wakati mmoja. Pesa na mapenzi. Hasa mapenzi. Aliwasili Camp Nou akiwa mtoto anayeupenda mpira. Kisha akaipenda sana Barcelona halafu pesa nyingi ikajileta yenyewe. Kwa sasa yuko PSG kwa sababu mbili.

Ya kwanza kabisa ni pesa. Messi hana mapenzi na PSG na wala hajatudanganya hivyo katika mkutano wake wa kwanza na vyombo vya habari. Hajazungumzia ule uongo kwamba “Nimekuwa nikiifuatilia klabu hii na kuipenda kwa muda mrefu.” Hajataka kutuambia uongo huu.

Sababu nyingine ambayo imemsukuma kwenda PSG ni ukweli kwamba miaka yake mitatu ya mwisho Barcelona alikuwa akicheza katika timu mbovu zaidi ya Barcelona tangu aanze kuvaa jezi ya kikosi cha kwanza klabuni hapo.

Ni katika miaka hiyo ndipo Messi alipokata tamaa. Kila alipojaribu kubaki na kudhani mambo yangebadilika nadhani amegundua kwamba alikuwa anajidaganya tu. Ni katika kipindi hiki ndipo ambapo Barcelona walifanya kama watoto na AS Roma na Liverpool. Tazama jinsi ambavyo matokeo ya Ligi ya Mabingwa yalipinduka kijinga dhidi yao. Messi akajikatia zake tamaa. Tayari kumbuka alitaka kuondoka msimu uliopita, lakini akatiliwa ngumu.

Nafasi hii ilipojitokeza akalia pale Nou Camp kisha akapanda ndege akicheka. Alikuwa kama ndege ambaye anatoroka. Anajua kwamba PSG ya sasa itampa unafuu mkubwa kuliko Barcelona. Kifupi ni kwamba PSG ni bora kuliko Barcelona kwa sasa.

Messi anakwenda kucheza na Kylian Mbappe, Neymar na Angel Di Maria. Wachezaji wa kariba hiyo hawapo Barcelona kwa sasa. Ghafla amejikuta katika timu ambayo inampa matumaini ya kutwaa Ligi ya Mabingwa kwa mara nyingine. Hii ni achilia mbali namna ambavyo maeneo mengine kuna Sergio Ramos, Gigi Donnarumma, Marco Verrati, Achraf Hakimi na wengineo. Ghafla Messi amejikuta katika kikosi cha mabingwa kwa mara nyingine na hili ni jambo ambalo amelichungulia.

Messi angeweza kuamua kwenda Falme za Kiarabu au Marekani kuliko kwenda kucheza Arsenal au Manchester United kwa sasa hata kama wangemudu mshahara wake. Ukweli ni kwamba kikosi chenyewe cha PSG kimemtamanisha achilia mbali pesa.

Waliosababisha kikosi hiki kimtamanishe ni Wahispaniola wenyewe. Mpaka sasa Real Madrid na wameshindwa kukivunja kikosi hiki kwa sababu hawana pesa. Neymar aliamua kusaini mkataba mpya PSG baada ya kuona Barcelona hawana tena pesa za kumrudisha ingawa wamekuwa wakitamani kufanya hivyo.

Mpaka sasa pia kumbuka kwamba Real Madrid licha ya kumtamani sana Mbappe, lakini hawana la kumfanya. Labda Mbappe atawasaidia kwa kuendelea kugoma kusaini mkataba mpya halafu mwakani ataenda Santiago Bernabeu akiwa mchezaji huru.

Vinginevyo Florentino Perez sio tena yule ambaye tunamjua kwa uhodari wake wa kukusanya Galacticos. Angeweza kumnyakua Mbappe kwa dau ambalo lingevunja rekodi za uhamisho duniani. Ameshindwa. Hana tena pesa hiyo na ndio maana alikuwa mmoja kati ya waasisi waliotaka kuanzisha ligi ya ajabu duniani.

Ni Perez huyuhuyu ndiye aliyesababisha Sergio Ramos akacheze na Messi PSG baada ya kushindwa kumpa ofa ya mkataba wa miaka miwili. PSG wamempa na sasa amejikuta akicheza katika timu moja na hasimu wake wa zamani, Messi. Wakubwa wa Hispania wamesababisha leo Messi awepo PSG huku ghafla akiwa katika timu kali.

Usishangae kuona Messi akitwaa ubingwa wa Ulaya akiwa na PSG. Wengi tumeanza kutabiri hivyo. Na hata kama Messi akishindwa kufanya hivyo, basi kuna nafasi kubwa kwa timu za Kiiingereza kufanya hivyo.

Kwa sasa tunachoweza kufanya ni kumtakia kila la heri Messi katika kikosi chake cha PSG. Tumeona historia ikiandikwa. Kuna wachezaji ambao hawakuwahi kuhama timu kama Francesco Totti au Paulo Maldini na tulidhani Messi angefuata mkondo huo. Hata hivyo mazingira yanayoeleweka yamesababisha ahame. Vile vile tumekosa fursa adimu ya kumuona Messi akiuzwa.