Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 27Article 544468

Maoni of Sunday, 27 June 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

NYUMA YA PAZIA: Nawakumbusha tu Enzo Zidane ana miaka 26

NYUMA YA PAZIA: Nawakumbusha tu Enzo Zidane ana miaka 26 NYUMA YA PAZIA: Nawakumbusha tu Enzo Zidane ana miaka 26

YALE maisha ya mtaani kwako uswahilini. Unaamka asubuhi unaenda kwa mama muuza chapati au maandazi. Kando yake ana mtoto wa kiume anayehangaika kufanya kazi hii na ile kumsaidia mama yake. Baadaye anaaga kwenda kucheza soka na wenzake. Anaruhusiwa.

Ghafla anaitwa tena na mama yake kwa ajili ya kwenda kununua mchele kwa maandalizi ya chakula cha mchana cha wateja. Jasho linamtoka. Anakwenda katika duka la Mangi huku akihema. Anarudi kumsaidia mama kisha anachomoka tena kwenda kucheza.

Unayakumbuka maisha yale? Tuliishi nayo. Mtoto unaonekana kuwa na kipaji kikubwa na baadaye watu wazima wanakupitia ili ukachezee timu zao. bila ya wewe hawashindi mechi. Wanakununulia viatu na jezi. Wanakuja kukuombea ruhusa kwa mama na kuna wakati wanampa pesa ili kumlainisha akuruhusu. Ghafla anajikuta mtoto anatoka ngazi moja kwenda nyingine na mwishowe anaishia kuwa staa mkubwa. Anaweza kuishia kuwa Mbwana Samatta au Diamond Platinumz. Mastaa wengi wakubwa Afrika wametoka katika mkondo huu wa maisha. Hawatoki familia za mambo safi.

Hata Ulaya mastaa wengi wametoka katika maisha ya kati. Nadra kutoka kuwa katika mtoto wa tajiri. Ni kama Zinedine Zidane alivyohangaika baada ya kujikuta katika familia ya wahamiaji wa Algeria pale Marseille, Ufaransa. Akajihangaikia na kuwa staa mkubwa. Lakini mwanaye Enzo Zidane hakuwahi kupata mkosi huo. Yeye amezaliwa katika familia ya kitajiri. Kama Zidane alikuwa mtoto wa wahamiaji, yeye alikuwa mtoto wa tajiri Zidane. Baba yake amekusanya pesa nyingi kwa kucheza Juventus, Boardeaux na Real Madrid. Baba yake ni bilionea. Enzo aliingia katika soka kuna watu wakiamini kwamba angekuja kuwa kama baba yake. Wananchi walimpokea wakidhani mtoto wa Zidane angekuwa kama Zidane. Ni kosa kubwa kusubiri watoto wa namna hii. Sio lazima wawe kama baba zao.

Ukweli ni kwamba baba zao ndio ambao walihangaika katika mazingira magumu lakini sio lazima wao wahangaike katika mazingira magumu. Hapo ndipo unapokuta wanakosa moyo wa kupambana. Wao wanaamka huku nje kuna magari ya kifahari, uhakika mkubwa wa chakula mezani, lakini pia uhakika wa kwenda likizo na wazee katika sehemu nzuri ya uso wa duniani popote pale duniani.

Lakini pia wengine wanajikuta wanaigiza kazi ya baba. Wanacheza soka kwa kutamani kuwa kama baba na wanapata sapoti kubwa kwa sababu ‘ni mtoto wa Zidane’. Yule mtoto wa muuza chapati wakati mwingine anakosa fursa kwa sababu ya kuzibiwa na ‘mtoto wa Zidane’. Hata hivyo bahati mbaya mtoto wa Zidane anajikuta hana kipaji lakini anapelekwapelekwa tu. Na ndio maana tunampata mtu kama Enzo. Wakati ule akiingia katika soka watu walikuwa wamehadaika huenda akawa na kipaji kikubwa na akatamba kwa sababu ni mtoto wa Zidane.

Leo nawakumbusha tu kwamba Enzo ana miaka 26 na hana mwelekeo wowote katika soka. Hayo yanatokea wakati kumbuka kina Kylian Mbappe, Cesc Fabregas, Wayne Rooney, Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na wengineo walianza kutamba na miaka mingapi. Wengi tuliwasikia wakianza kutamba wakati wana miaka 17 tu.

Enzo ana miaka 26 na haumsikii. Bado anajiita mchezaji. Majuzi nimemsikia akicheza katika klabu ya Rodez ya Daraja la Pili Ufaransa. Umri huo baba yake alikuwa akikaribia kuvunja rekodi ya uhamisho wa dunia kutoka Juventus kwenda Real Madrid. Kuna wachezaji wachache waliofanikiwa kutoboa wakitokea katika familia za kitajiri. Hawa ni kina Ricardo Kaka. Lakini wapo pia watoto wa wachezaji mastaa ambao walifanikiwa kupenya na kufanya mambo makubwa.

Mfano ni huyu Erling Haaland. Baba yake, Alf Inge Haaland alikuwa staa mkubwa Leeds United, Manchester City na timu ya taifa ya Norway lakini kesi hizo sio nyingi kuliko wale ambao wamefeli. Kesi za waliofeli zipo katika hesabu za vidoleni.

Kwa mfano, watoto wote wa David Beckham wanaonekana wamefeli. Waliongozwa na kaka yao mkubwa, Brooklyn Beckham ambaye Waingereza walijaribu kumsukumia katika soka mpaka wakachoka. Yeye mwenyewe alipata nafasi kubwa ya kufanya mazoezi katika timu kubwa kama Arsenal lakini ikagundulika kwamba alikuwa anapoteza muda tu.

Baadaye aliamua kwenda katika kazi nyingine ambayo aliona inamfaa. Kwa sasa ni mpigapicha tu. wadogo zake nao hatuwasikii sana lakini sidhani kama wana vipaji vikubwa kwa sababu katika umri wa miaka 17 walipaswa kuanza kuwika katika baadhi ya timu.

Soka ni mchezo unaochezwa na watoto wa maskini huku ukiongozwa na matajiri. Kuna mahala ambapo unaumia zaidi na hauwezi kusonga mbele kama hauna hasira za kimaskini. Hasira ambazo mtoto wa tajiri hawezi kuzifikia.

Kwa mfano, Ronaldo de Lima alijikita zaidi katika soka kwa sababu alichukizwa na kazi ya mama yake, Sonia ambaye alikuwa akiuza pombe baa. Walevi walikuwa wakimshika mama yake ovyo ovyo mbele ya macho yake na alitia nia ya kumuondoa mama yake katika kazi hiyo ya fedhea.

Alipambana kwa kiasi kikubwa kuiondoa familia katika umaskini. Tatizo kina Enzo hawana hasira hizo. Na hata mtoto wa De Lima hawezi kuwa na hasira hizo kwa sababu ameangukia baba yake kuwa tajiri. Enzo leo alipaswa kuwa mmoja kati ya wachezaji ambao wanacheza michuano ya Euro akiwa katika ubora. Kuonyesha kwamba hakuwa na kipaji kikubwa, alicheza mechi moja tu ya Ufaransa chini ya umri wa miaka 15. Kumbuka kwamba baba yake ni shujaa wa taifa hilo na aliwapa ubingwa wa dunia mwaka 1998 pale Paris.

Baadaye Enzo aliamua kuhamia katika uraia wa mama yake Hispania lakini alicheza mechi mbili tu za kikosi cha chini ya umri wa miaka 17. Hii inaonekana ni namna gani hakuwa na kipaji kikubwa. Ni kwa sababu tu alikuwa ni mtoto wa Zidane ndio maana alipata nafasi.

Hata hivyo tofauti ya Enzo na wengineo ni kwamba bado ana uhakika wa kwenda likizo na rafiki yake wa kike popote anapotaka. Baba yake ni tajiri.