Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 24Article 565312

Maoni of Sunday, 24 October 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

NYUMA YA PAZIA: Tajiri atazidi nguvu ya wanafiki wa Solskjaer Trafford?

Kocha wa Man U, Ole Gunner Solkjaer Kocha wa Man U, Ole Gunner Solkjaer

Nililitazama bao la Mo Salah dhidi ya Manchester City nikamkumbuka Michael Jordan. Nitakwambia kwanini. Nikalitazama bao la Mo Salah dhidi ya Watford nikamkumbuka Michael Jordan tena na tena.

Jordan achana na kipaji chake cha wakati ule, aliwahi kusema “katika uwekezaji wowote unaoufanya inabidi ufurahie unavyoendelea, na pia upate pesa”. Kwa sasa Jordan ni bilionea hasa. Amewekeza katika nembo yake ya Air. Anafurahia watu wanavyovaa. Viatu vinawapendeza. Lakini pia anapata pesa. Labda ndivyo ambavyo tajiri wa Liverpool alivyokuwa anamtazama Salah katika hizi mechi.

Jinsi alivyowageuza mabeki wa Man City na Watford kuwa koni za mazoezini na kisha kufunga. Ilimpa raha tajiri wa Liverpool lakini pia alikuwa anajua kwamba mabao hayo yanampa pesa.

Matajiri wa Manchester United walikuwa wanawaza nini wakati Leicester City walipofunga bao la nne kupitia kwa Mzambia Paston Daka wikiendi iliyopita? Subiri kwanza. Pesa wanapata. Manchester United wanaendelea kupata pesa nyingi. Vipi raha wanapata? Hakuna raha. Na sasa unafunguka miongoni mwa mijadala mizito kuwahi kuibuka Manchester United. Kocha Ole Gunnar Solskjaer afukuzwe au? Kuna mgawanyiko wa hisia ulioletwa pale Old Trafford. Moyoni tajiri atakuwa anataka Ole aondoke. Tatizo tajiri hasikii kelele za kutosha kutoka kwa watu walewale ambao waliwahi kumshinikiza awafukuze David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho.

Kelele zipi? Kuna kelele za aina mbili. Kelele za mashabiki wa mtaani na kelele za watu wazito. Bahati mbaya watu wazito wenyewe ni wazito hasa na hawapigi kelele. Hawa ni wachezaji wa zamani. Kina Paul Scholes, Roy Keane, Rio Ferdinand, Gary Neville na wengineo.

Mtaani tunapiga kelele lakini hawa hawapigi kelele. Ole ni mwenzao. Wamecheza naye kwa muda mrefu tena kwa mafanikio. Nadhani wapo katika kundi moja la WhatsApp na wanampa mawazo ya nini kifanyike. Anafanya kila awezalo lakini United imekuwa kama ilivyo sasa. Hakuna kitu cha maana inachofanya.

Haujui ubora wa United uko wapi. Kwamba wanajihami vyema, hapana. Kama wanamiliki mpira vyema, hapana. Kama wanashambulia vyema, hapana. Hauwezi kujua ubora wa Manchester United hii uko wapi. Watu wanaufahamu ubora wa Liverpool, ubora wa Manchester City, ubora wa Bayern Munich, lakini hawaufahamu ubora wa moja kati ya klabu maarufu zaidi duniani, Manchester United. Haikuwa hivi hapo zamani kidogo wakati kina Scholes wanacheza. Hata hivyo wamefunga mdomo kwa sababu kinachofanyika kwa sasa kinafanyika chini ya mwenzao. Wanachofanya kwa sasa ni kuhamisha lawama kwa wachezaji kila siku.

Enzi za kina Mourinho waliokuwa wanalaumiwa ni makocha. Kina Keane walikuwa wanakesha katika migongo ya kina Van Gaal huku wakiwa wamekaa katika sofa za Skysport wakichambua. Maisha hayapo tena hivyo. Kwa sasa ni wachezaji na sio kocha.

Kinachochekesha zaidi ni kwamba hata Sir Alex Ferguson amekaa kimya. Hakosekani katika kila mechi ya United, hasa nyumbani. Sidhani kama anaiona Manchester yake anayoita lakini hata hivyo amekaa kimya. Sijasikia anachosema juu ya ubora wa City na Liverpool.

Kwa City anaweza kusema kwamba wametumia pesa nyingi, lakini kwa Liverpool ukweli ni kwamba Jurgen Klopp ametumia uwezo mkubwa wa ukocha wake kuliko matumizi ya pesa. Ni ukweli ambao unapima akili ya Ole na makocha wengine wakubwa.

Kina Salah wamenunuliwa kwa bei rahisi kuliko kina Jadon Sancho. Ni ukweli ulio wazi. Kina Trent Alexander Arnold hawakununuliwa. Wamepandishwa katika kikosi cha kwanza wakitoka timu ya vijana. Lakini vipi kuhusu Aaron Wan Bissaka? Wameigharimu United pesa nyingi.

Vyovyote ilivyo rafiki zangu kina Keane yote haya wanayajua. Majuzi tu Jamie Carragher aliwapasulia ukweli kwamba wanakaa kimya kwa sababu wamecheza na Ole. Bahati mbaya kwa kina Roy ni kwamba visingizio vingi vimeisha. Kinachoweka maisha yawe magumu ni kwamba Ole mwenyewe anadai kwamba anajua anachofanya na yeye ndiye mtu sahihi wa kurekebisha kinachoendelea. Anakuwa mwanasiasa. Anajaribu kutatua tatizo ambalo amelitengeneza. Inachekesha kidogo.

Nimemshangaa Scholes ambaye pia amedai kwamba Ole apewe muda. Muda upi? Sawa apewe, lakini wakati akipewa huo muda inajulikana wazi kwamba kina Pep Guardiola wanazidi kuimarika baada ya kuwachukua kina Jack Grealish. Klopp naye amerudi moto. Na kabla mashabiki hawajaamka katika kile ambacho tunakiona kuna Waarabu wengine wamenunua Newcastle United. Ni matajiri zaidi kuliko matajiri wa Manchester City. United inabidi waamke wapige hatua za haraka kabla hawajakutwa weupe na Newcastle.

Mwisho wa siku naamini kwamba unafiki wa kina Keane huenda ukafika mwisho. Kama hautafika mwisho basi kuna uwezekano tajiri akaamua kufuata busara za Michael Jordan. Kwamba uwekezaji lazima uwe na raha ndani yake. Ni sawa tu na mmiliki wa baa anapoamua kufurahia baa yake ilivyokaa huku akiwa anapata kinywaji na rafiki zake. Mwisho wa siku aliyetia pesa atakuwa na kauli kubwa zaidi. Wafanyabiashara waliofanikiwa mara nyingi huwa wana maamuzi magumu na ndio maana wanafanikiwa. Wakongwe wa United huwa wanajidanganya kwamba mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha hayajawasaidia United. Wanayasema hayo kwa sababu kocha ni Ole.

Sidhani kama hilo litafanikiwa kwa sasa pindi familia ya Glazer itakapoona mapato yanaanza kupungua kwa sababu ya matokeo mabovu. Watachukua maamuzi magumu. Kina Keane wanaweza kusubiri kuanza kumkandia kocha ajaye lakini kwa huyu wamejikuta katika unafiki mwingi. Wachezaji hawahawa waliopo katika kikosi cha sasa cha United wanaweza kumpatia matokeo kocha yeyote mwenye uwezo mkubwa. Hakuna muda tena wa kumpa kocha. Paul Pogba alivunja rekodi ya uhamisho ya dunia.Harry Maguire alivunja rekodi ya uhamisho kwa mabeki. Cristiano Ronaldo ametwaa ubingwa wa Ulaya mara nne na sitaki kuhesabu mara ngapi amewahi kuwa mwanasoka bora wa dunia. Vipi kuhusu Bruno Fernandes na ubora wake? Vipi kuhusu Sancho? Vipi kuhusu bei ya Wan Bissaka? Nani mbovu pale United? Wapo wachache kuliko wengi. Bado wanafiki wanamtetea Ole. Na sasa tulio nje tunasubiri kuona. Tajiri atazidi nguvu ya wanafiki Old Trafford?