Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 08Article 556150

Maoni of Wednesday, 8 September 2021

Columnist: TanzaniaWeb

Nabi katika mtihani uliomshinda Mwinyi Zahera

Kocha Mkuu wa Yanga,  Nasreddine Nabi Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi

Novemba 13, mwaka 2019 kwenye Uwanja wa 30, June pale Cairo nchini Misri, Yanga chini ya kocha Mwinyi Zahera ilishiriki kwa mara ya mwisho michuano ya Afrika ambapo kikosi hicho kwa bahati mbaya kilipokea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Pyramid FC na kumaliza matumaini ya mashabiki wao kuona klabu yao inafika mbali Kimataifa.

Kipigo hicho cha mabao 3-0 ilikuwa ni matokeo ya mchezo wa mkondo wa pili, ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Oktoba 27, mwaka huo Yanga wakiwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza walishindwa kufua dafu na kukubali kipigo cha mabao 2-1, hivyo kuondoshwa kwa matokeo ya jumla ‘Aggregate’ ya mabao 5-1.

Tangu mwezi Novemba mwaka 2019 mpaka sasa ni takribani miaka mitatu imepita tangu Yanga washiriki michuano ya Afrika kwa mara ya mwisho, nafasi ambayo kwa msimu uliopita Klabu za Simba na Namungo zilishiriki.

Ukame huu wa ushiriki kimataifa ni wazi umewafanya mashabiki wengi wa Yanga watarajie mambo makubwa kutoka kwenye klabu yao katika ushiriki wa michuano hiyo kwa msimu ujao wa 2021/22.

Nadhani Uongozi wa Yanga unastahili pongezi kubwa kwa kupambana, na kuirejesha timu hiyo katika michuano hii mikubwa Afrika.

Lakini pia pongezi kubwa kwao ni juu ya namna ambavyo Kamati ya usajili ya Yanga, Uongozi wa klabu hiyo pamoja na wadhamini wao kampuni ya GSM kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika dirisha kubwa la usajili ambalo lilifungwa Agosti 31, mwaka huu.

Kila mtu atakubaliana nami kuwa kikosi cha Yanga cha msimu ujao kinatarajiwa kuwa bora zaidi kulinganisha na msimu uliopita, hasa kwa kuangalia kushiba kwa wasifu ‘CV’ za mchezaji mmoja mmoja ambaye amemwaga wino na kuwa kwenye jukumu la kuwatumikia Wananchi kwa msimu ujao.

Ni wazi kwa usajili uliofanyika kuna mengi ya kuyatarajia kutoka kwa chama la Wananchi kwa msimu ujao, kuanzia kwenye michuano ya ndani na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa kwa maneno na hata vitendo kuwa msimu huu hawataki kushiriki pekee, bali shabaha yao kubwa ni kushindana na kufanya vizuri.

Yanga wanatarajia kuanza kibarua chao cha Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Klabu ya Rivers United kutokea nchini Nigeria, ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam Septemba 12, mwaka huu yaani hapa tunazungumzia siku nne tu zimesalia kuelekea mchezo huo. Mchezo wa mkondo wa pili utapigwa Nigeria Septemba 19, mwaka huu nchini Nigeria.

Swali gumu kwa Yanga hususani kwa Uongozi wa klabu hiyo na kocha wao Mkuu, Nasreddine Nabi ni Je, kwa kiasi gani wapo tayri kwa mchezo huo? Tukumbuke kuwa licha ya usajili bora ambao wameufanya kuelekea msimu ujao, lakini ni jambo lililowazi kuwa Yanga wanakabiliana na changamoto kubwa ya kutafuta muunganiko wa timu yao kuelekea mchezo dhidi ya Rivers.

Changamoto hii inatokana na uhalisia kwamba Yanga ina idadi kubwa ya wachezaji wapya ambao wanaingia moja kwa moja ndani ya kikosi, hivyo kama hakutakuwa na maandalizi mazuri jambo hili linaweza kuwa na athari kubwa kwao.

Ikumbukwe kuwa Yanga wanaanzia katika Uwanja wa nyumbani ambao kwa hesabu za mpira ni jambo la lazima kuhakikisha unapata matokeo mazuri, hususani ushindi mkubwa ili kujiweka salama kuelekea mchezo wa marudiano.

Hivyo siyo tu kwamba ni muhimu, lakini ni jambo la lazima kwa Yanga kupambana na kusaka ushindi mkubwa kwenye mchezo wa Jumapili pale kwenye Uwanja wa Mkapa, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ushindi huo kwenye mchezo utakaopigwa Nigeria na kukamilisha malengo yao ya kufuzu hatua ya kwanza ya michuano hiyo.

Binafsi ninaamini kuwa Yanga ina kila sababu za kufanya vizuri kwa sasa, kwa kuwa wana kikosi bora, na wamejitahidi sana kupata michezo mingi ya kirafiki licha ya kukumbana na changamoto ya kambi yao kule Morocco ambapo walilazimika kuivunja kambi hiyo.

Kila la kheri Yanga, Azam na Biashara kwenye michezo yenu ya awali.