Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2019 12 16Article 491029

Maoni of Monday, 16 December 2019

Columnist: mwananchi.co.tz

Namna ya kumsaidia mtoto anayekojoa kitandani

Namna ya kumsaidia mtoto anayekojoa kitandani

Si jambo geni kusikia mtoto akiitwa kikojozi, hata akiwa sekondari. Mara nyingi, tabia hii inajengwa tangu mtoto akiwa mdogo.

Wataalamu wameeleza kuwa kitendo cha mtoto wa miaka chini ya mitano au zaidi kutokwa na mkojo bila kujitambua hasa usiku usingizini ni cha kawaida katika ukuaji na mzazi hapaswi kuogopa.

Upo ushahidi wa tafiti zinazoonyesha kuwa tatizo hili huweza kuwa la kurithi.

Pili tatizo linaweza kuwa usingizi mnono. Mtoto akilala hapati hisia ashiria kutoka kwenye kibofu kumkumbusha muda wa kukojoa. Tatu ni kibofu kidogo. Mkojo unaozalishwa usiku unaweza kuwa mwingi kuzidi uwezo wa kibofu hivyo kukosa mlinganyo sawa wa uzani katika uzalishaji kemikali iitwayo Antidiuretic Hormone (ADH) inayosaidia kujua kiwango stahiki cha maji mwilini.

Pia, zipo sababu za kiafya, mfano maradhi ya kisukari na maambukizi katika njia ya mkojo UTI (Urinary Tract Infection) na kumuacha mtoto kwenye mkojo muda mrefu bila kumbadili nepi hadi kumfanya kuzoea unyevu kama hali ya kawaida.

Nini suluhisho? Kwanza mtengenezee mtoto ratiba ya kukojoa kila baada ya muda fulani ili ubongo uzoee na kumtaarifu anapohisi kukojoa.

Pili, mbadilishie mtoto muda wa kunywa vimiminika na usimwache na kiu muda mrefu (hasa usiku), anaweza kunywa asubuhi hadi alasiri ili apate muda wa kukojoa kabla ya usiku hivyo kulala bila kujikojolea. Tatu, punguza kumlisha vichocheo vya kuzalisha mkojo hasa vyenye madini ya caffeine ikiwemo chokoleti, maziwa na kokoa.

Nne, mchunguze mtoto kama ana tatizo la kukosa au kupata choo kwa shida, hii inaweza kusababisha matatizo ya kibofu na hivyo tatizo la kutodhibiti mkojo.

Mwisho unashauriwa usimuamshe mtoto usiku kukojoa, haisaidii kuondoa tatizo bali kulizidisha kwa kuleta usingizi wa fofofo pale anaporudi usingizini baada ya kukatishwa. Hii inamkosesha fursa ya kujenga tabia ya kudhibiti na kupambana na tatizo hili wakati wa mchana.

Kamwe usimuadhibu kama kumchapa, kumpaka upupu au kumuimbia ‘kindumbwendubwe’, kwani kitaalamu imethibitika kutosaidia bali kumuaibisha mtoto na kumuumiza. Tumekuwa tukishuhudia ndoa, mahusiano kuvunjika inapotokea mwenza mmojawapo anakojoa kitandani, vijana wakubwa na wadogo shule za msingi, sekondari wakizomewa wanapogundulika na tatizo hili.

Ukweli ni kwamba tatizo hili linamkosesha amani mtoto zaidi kuliko mzazi, maana mzazi anateseka kipindi mtoto akiwa mdogo lakini mwenye tatizo huendelea kuteseka nalo muda mrefu.

Tatizo hili huweza kumsababishia mtoto madhara kama kukosa uwezo wa kujiamini, kujitenga na wenzake na kukosa marafiki, kufeli masomo, matatizo ya kitabia, mara nyingi hujisikia aibu na fedheha mbele ya wenzake na wakati mwingine kuwa mkorofi na mshari kwa yeyote atakayemtania.

Pia hujenga wasiwasi unaopelekea kushindwa kusikiliza kwa umakini awapo darasani au nyumbani, huogopa kutembelewa na wageni au kutembea na kulala nje ya nyumbani (sleep-overs). Ili kumsaidia na kuepuka fedheha ya utu uzima, shirikiana naye katika kutafuta suluhu.

Mtie moyo kwa kusifia hatua za maendeleo na jitihada anazozifanya katika kupunguza tatizo, msaidie ajione hana hatia na mfanye afurahie jitihada zake.