Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 07Article 541438

xxxxxxxxxxx of Monday, 7 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ndoa na sababu za kuchokana - 2    

Takriban katika maisha ya wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao hupitia katika vipindi tofauti. Kama ulivyo umri wa Binadamu, ndoa hupitia katika kipindi cha utoto, ujana na uzee, na kila kipindi kina mambo yake na taratibu zake kama tulivyoona katika makala iliyopita ambazo kama wanandoa watashindwa kuzifuata basi huenda ndoa hiyo ikakumbwa na mtihani mkubwa, nao ni mtihani wa kuchokana.

Hivyo basi, sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa kunasababishwa na wanandoa na pengine mwanamke anaweza kuchangia zaidi hasa pale ambapo atashindwa kutumia nafasi yake na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa yao.

Katika makala iliyopita nilipigiwa simu na wasomaji kadhaa wakiona kama kwamba ninapendelea wanaume lakini niliyoyaandika yanatokana na maandiko matakatifu na hata uchunguzi wangu binafsi unaonesha hivyo. Hata hivyo, waliopiga simu niliwaambia waendelea kufuatilia ambapo leo, wanandoa wote, mume na mke wataguswa.

Wiki iliyopita tulianza kuangalia baadhi ya visababishi vinavyopelekea katika kuchokana kwa wanandoa na leo tutaendelea kuangalia na kuchambua visababishi vingine ambavyo ni muhimu kwa wanandoa kuvielewa.

Kutamka na kudhihirisha mapenzi

Ni muhimu sana kwa wanandoa ili kuyaimarisha mapenzi yao yasiote mvi, kutamkiana hisia zao za kupendana bila utangulizi wowote, kwa mume au mke kumwambia mwenzake NAKUPENDA kuna athari nzuri katika nafsi kuliko hata ungemletea zawadi ya kitu cha gharama.

Kwa Waislamu watakumbuka kwamba Mtume Muhammad (SAW) ametufundisha kwa kusema: “Atakapompenda mmoja wenu ndugu yake basi amfahamishe, kwani huzidisha maelewano na kuthibitisha mapenzi…” Hadithi Sahihi, Silsilatus Swahiyhah

Haya ni mafundisho watu hawayajali wakiwemo Waislamu na leo hii yanaonekana ni mila za kimagharibi, na huonekana kioja katika jamii mke kumwambia mumewe kuwa ‘Nakupenda’ na si ajabu mume mwenyewe au mke anayeambiwa hivyo na mwenzake akajibu kwa kejeli: “Ah hebu acha utani wako, sisi tumeishazeeka”.

Lakini wanandoa wengi hupenda kudhihirisha mabaya na mambo yanayowakera kuliko yale mazuri ya kufurahisha, jambo ambalo kwa kiwango kikubwa linachangia katika kuchokana haraka.

Kupeana zawadi

Zawadi ni njia nzuri ya kudhihirisha mapenzi yako na nafasi ya mwenzako katika maisha yako, na zawadi ambayo mtu huitoa kwa mwenzake bila ya utangulizi au mnasaba maalumu huleta athari njema na huimarisha mapenzi, kama na hili pia Mtume (SAW) pia amefundisha kupiyia Hadith aliyosimulia Abu Hurairah akisema: “Peaneni zawadi mtapendana.”

Na katika zoezi hili la kupeana zawadi, ni vema kila mmoja akaelewa anachokipenda mwengine ili zawadi iwe na athari inayotarajiwa, na iwe ni zawadi maalumu kwa mlengwa.

Nashauri isiwe zawadi ambayo mtoaji naye atafaidika na zawadi hiyo, kwa mfano, si vema kwa mwanaume kumletea mkewe zawadi ya sufuria, microwave, pazia, dinner set na mfano wa hivyo. Vitu vya aina hiyo havitaitwa zawadi bali vitu vya matumizi ya nyumbani lakini ni juu yake kumletea manukato ayapandayo, mavazi, hereni, bangili, mkufu au pete ya dhahabu, na vitu ambavyo ni maalumu kwa matumizi yake binafsi. Vivi hivyo yapaswa pia mke kumzawadia mumewe.

Kualikana vyakula

Inaweza kushangaza kuwa vipi wanandoa wataalikana chakula wakati wenyewe ni mume na mke, na ni lazima wale pamoja?! Ni vema ikaeleweka kuwa, kubadili mazingira na kufanya vitu mahsusi kwa kushtukizana, huwafanya wanandoa kutozoeana na kuchokana, kwani maisha yenye mtindo na mtiririko mmoja kila siku humfanya mtu kuyachoka.

Ni vema wanandoa kuwa wabunifu katika kuyapaka rangi mpya maisha yao kwa kubuni vitu vitakavyotia ladha mpya katika nyumba, njia mojawapo ni hiyo ya kumualika chakula maalumu mke au mume wakiwa peke yao, na hata kama itamlazimu mwanandoa kununua au kuagiza aina tofauti ya chakula basi afanye hivyo, na ampe mwaliko mwenziwe wa kutokosa kuhudhuria katika mnasaba huo.

Hebu unayesoma hapa jaribu, siku moja kumwalika mwenzi wako katika hoteli ya heshima mlo wa mchana au usiku na kupata nafasi ya kujikumbusha mambo mazuri yaliopita.

Kubadilisha mpangilio wa nyumba

Wanawake wengi huwalalamikia waume zao kwa kutopenda kukaa nyumbani na badala yake kumaliza muda wao kwenye migahawa na kwa marafiki zao. Mke mwerevu huwa anafanya kila juhudi za kumnasa mumewe apende kukaa nyumbani wakati wa nafasi yake kwa kumbadilishia mazingira ya nyumba.

Mazingira ya nyumba yanapokuwa ni yale yale tangu ndoa ilipofungwa hadi wanakuwa na watoto watatu, kochi lipo palepale kama kisiki cha mti, saa ya ukutani tangu imetundikwa mpaka imeshikana na ukuta, mapazia yaleyale na kama yanabadilishwa basi rangi ni zilezile, hali hii humfukuza mwanamume ndani ya nyumba na kumfanya arudi kuja kulala tu, na huu ndio mwanzo wa kuchokana na kuichoka nyumba.

Kwa familia nyingi mume ndiye anatoa pesa ya kununua vitu vya kubadilisha nyumba lakini mbinufu na kudai hizi pesa mara nyingi anapaswa kuwa mwanamke.

Usafi wa mwili na mavazi

Moja miongoni mwa mambo yanayokera kwa wanandoa ni uchafu wa mmoja wao. Uchafu ni sifa isiyovumilika. Wakati wanaume wana tatizo la kutooga vizzuri na ‘kujiswafi’ kila eneo, baadhi ya wanawake hudhani kuwa manukato, vipodozi ndio usafi.

Utakuta anapitisha masiku bila kuoga kikamilifu, bali anapitisha pitisha maji na sabuni tu katika maeneo fulani, kisha kujijaza manukato, lotion na mafuta mengine, bila kuelewa kuwa, anapokuwa karibu zaidi na mumewe harufu ya asili hujitokeza na kuleta mchanganyiko wa harufu mbaya.

Hali kama hii si rahisi kwa mwanaume mstaarabu kuizungumzia kwa mkewe, atakaa nayo na atavumilia, lakini mwisho wake ni kumchoka mke huyu.

Wanaume nao hudhani kuwa kwao wanaume ndio wamepewa kibali cha kuwa wachafu. Kwa mfano wanaume wengi huona ni jambo la kawaida kunuka jasho, na wengine wana matatizo sugu ya kunuka miguu na maeneo ya kokwa zao.

Huu ni uchafu ambao hauvumiliki kwa mwanamke msafi. Aidha baadhi ya wanaume hawana vionjo katika mavazi yao, na jinsi wanavyojiweka, jambo ambalo linaweza kumsababishia mke maudhi, na hata kujihisi aibu kunasibishwa na mume wake!

Kufanya Ibada kwa pamoja.

Nguzo muhimu na mhimili wa maisha ya ndoa ni kumcha Mwenyezi Mungu. Kwa waislamu, swala za usiku humkurubisha mja karibu zaidi na muumba wake, hivyo mume na mke kuhimizana kufanya ibada hii pamoja huwazidishia imani na mapenzi baina yao na kuifanya ndoa yao kuwa imara zaidi.

Ni vema wanandoa pia wakaweka katika kalenda yao ya mwezi au miezi kwa mujibu wa nafasi zao kufanya matendo ya kiibada kama kutembelea ndugu wa nasaba, kutembelea majirani, kutembelea wagonjwa hospitali, kutembelea vituo vya watoto yatima na kujitolea au kutoa msaada kwenye taasisi zinazotoa msaada kwa jamii zilizotatizika

Ibada hizi zitawazidishia imani yao na kuwafanya wawe karibu na Mwenyezi Mungu na wawe pia karibu na ndoa yao.

Itaendelea…

Mwandishi wa makala haya ambaye ni mmoja wa mashehe waliobobea katika saikolojia ya mahusiano na malezi ya watoto anapatikana kupitia +255 784 448 484 – [email protected]

Join our Newsletter