Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 19Article 552478

Maoni of Thursday, 19 August 2021

Columnist: TanzaniaWeb

Ni kweli Katiba sio hitaji la Wananchi?

Uhitaji wa Katiba Mpya Uhitaji wa Katiba Mpya

Vuguvugu la madai ya Katiba mpya limeanza kushika kasi, lakini katikati ya vuguvugu hilo kumejitokeza kundi ambalo linajaribu kuuaminisha umma kuwa hakuna mwananchi wa kawaida anayeihitaji isipokuwa ni wanasiasa.

Kundi hilo limeamua kuvaa miwani myeusi katikati ya giza totoro na kwa vyovyote vile haliwezi kuona wala kukumbuka kuwa maoni pekee tuliyonayo hadi sasa ni ya wanaotaka Katiba mpya na aina ya Katiba na hatuna waliosema hawataki.

Tena maoni haya yalikusanywa chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 8 ya mwaka 2011 na marekebisho yake ya 2012 yaliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa na mamlaka ya kisheria kukusanya maoni nchi nzima.

Tume hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba ilikusanya maoni kwa miezi mitano kuanzia Julai hadi Desemba 2012 na ilifanya mikutano 1,942 ambayo ilihudhuriwa na wananchi 1,365,337 ambao kati yao, 333,537 walitoa maoni yao.

Si hivyo tu, Januari 2013 Tume ilikusanya maoni kutoka makundi mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa, taasisi za Serikali, taasisi za dini, wakulima, wafugaji, wafanyakazi na Asasi za kiraia na kwa ufupi makundi 160 yalikutana na Tume.

Ni kutokana na maoni hayo, ndipo tulipata rasimu ya pili ambayo ilipelekwa Bunge la Katiba na ikapatikana Katiba Inayopendekezwa ambayo kwa sehemu kubwa naweza kusema haikubeba maoni ya wananchi, bali maslahi ya wanasiasa.

Sasa wiki iliyopita nilipomsikia Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo akisema hakuna mwananchi anayetaka katiba mpya nilishangaa sana nikajiuliza msingi wa kauli hiyo unajengwa kwa kuegemea utafiti upi?

“Wapi umeona wananchi wamebeba mabango wamesema wanataka katiba mpya. Tuambiane ukweli. Zaidi ya sisi wanasiasa. Na sisi wanasiasa katika katiba mpya tunataka mambo mawili matatu"

“Kwanza tunataka Tume Huru ya Uchaguzi, niambie mwananchi gani Tume huru inampelekea unga, inampelekea ugali. Tunataka tutengeneze loop hole (mwanya) wa sisi kushika madaraka. Full stop (mwisho). Hakuna kingine,”

Lakini kiongozi huyo wa juu CCM hakuishia hapo, akasema kingine kikubwa wanachotaka (hao wanasiasa) ni demokrasia na uhuru wa kuendesha mambo yao na kwamba hayo ndio makubwa.

Ukifanyia tathmini kauli ya Chongolo na kurejea kilichojitokeza katika Bunge Maalumu la Katiba ambapo mambo ya msingi kabisa waliyoyataka yalinyofolewa, unajiuliza nani walikuwa wengi ndani ya Bunge lile zaidi ya wajumbe wa CCM

Ukisoma ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya Mei 2018. imebainisha wazi kuwa mpasuko ndani ya Bunge la katiba ulichangiwa na uwepo wa idadi kubwa ya wanasiasa ambao waliteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge hilo. Sasa kwa vile Chongolo anasema vuguvugu la sasa ni la wanasiasa wenye agenda zao za madaraka, basi tuachane na vuguvugu hili turudi kuanzia pale kwenye rasimu ya pili kwa sababu katiba inayopendekezwa ina maslahi ya wanasiasa.

Tuifumue sheria ya mabadiliko ya Katiba, tuwaondoe wanasiasa kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, badala yake tutengeneze mfumo ambao rasimu ile ya pili itakwenda kupigiwa kura na wananchi ya Ndiyo au Hapana.

Ninasema hivyo kwa sababu tume ya Warioba haikulenga katiba ya vikundi au vyama vya siasa, bali iliandaa Katiba ya nchi ikiegemea maoni ya wananchi ambayo baadaye yalivurugwa katika Bunge Maalumu kwa maslahi ya wanasiasa.

Hakuna ubishi na ambaye halioni hili basi nitatilia shaka uzalendo wake, kuwa hoja ya Katiba mpya imeanza kuligawa taifa letu katika vipandevipande na kuibua chuki ambayo inaanza kutishia amani na umoja wa kitaifa.

Kuahirisha kuandika Katiba mpya ni sawa na kumpa panadol mgonjwa wa saratani ukiamini ni tiba.

Tusisubiri hadi vuguvugu hili la Katiba mpya likafikia kama wenzetu Kenya walipopitia wakapata Katiba mpya 2010 ambapo wapo walilopoteza maisha na wala hakuna sababu ya kutumia nguvu kuzima moto wa Katiba mpya.

Mwaka 1917 huko Urusi, Jeshi lililokuwa na vifaa vya kisasa lilizidiwa na nguvu ya umma na ndio maana nimetangulia kusema tusisubiri vuguvugu hili likaingia hatua nyingine kwa vile kulizuia itakuwa kama ni kuzuia mafuriko kwa mikono.