Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 07 07Article 545818

Maoni of Wednesday, 7 July 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Ni nini kiini cha umasikini wa wachimbaji wadogo

Ni nini kiini cha umasikini wa wachimbaji wadogo Ni nini kiini cha umasikini wa wachimbaji wadogo

UCHIMBAJI mdogo wa madini katika siku za karibuni ni miongoni mwa sekta ambayo imegeuka kimbilio kubwa kwa vijana ili kujipatia kipato.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa, ingawa wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kwenye kazi hizo, vijana wengi wameshindwa kujikomboa na umasikini na kubakia watumwa wa kazi hizo, miaka hadi miaka, hali inayoibua maswali ya nini kifanyike ili uchimbaji mdogo uwe jukwaa la ukombozi wa kiuchumi kwa vijana.

Mtazamo wa vijana migodini

Mussa Elikana (27), mchimbaji mdogo katika mgodi wa madini ya dhahabu wa Kasi Mpya uliopo kata ya Mwazimba wilayani Kahama anasema ameanza kufanya kazi migodini tangu mwaka 2017 na hadi sasa amepita kwenye migodi minne. Lakini anakiri kwamba maisha ya migodini ni magamu na hajafanikiwa lolote.

Anasema aina ya uchimbaji wanaofanya ni mgumu kuwa ni wa kubahatisha na hivyo kupata hata gramu moja ya dhahabu ni mtihani mkubwa.

Hata hivyo anasema mafanikio makubwa anayojivunia tangu aanze shughuli za migodini ni kuweza kununua ng’ombe saba na kiwanja kimoja lakini ameshindwa kujenga nyumba.

“Mimi nazama ndani, ila kwa sasa hivi tuseme tu kwa ujumla huwezi kuzama ndani kwa ajili ya kutafuta hela kubwa, tunatafuta hela ya matumizi tu, yaani kwa sasa hivi tunapiga tu ya mabosi unalipwa hela, kwa mfano mfuko unalipwa Sh 3000, basi unapata ya matumizi, kwa siku unaweza kupata elfu 50 hadi elfu 70,” anasema Elikana.

Elias Makenzi (31), anasema changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu ya fedha kwa wachimbaji wengi wadogo ambapo taasisi za kifedha zinapaswa kuwageukia na kuwasadia namna ya kujikwamua kiuchumi pamoja na kuwapatia motisha jinsi gani ya kujiwekea akiba kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

“Unakuta, kwa mfano kwenye machimbo hapa, hakuna taasisi ya kifedha hata moja, ambayo inawasaidia wachimbaji kufungua akaunti, kwa hiyo tunabaki saa nyingine ukipata pesa tunajisahau, tunatumia yote na hiyo inakuja kuleta shida huko mbele. Unaweza ukapata tatizo kwenye uchimbaji ukakosa pesa kwa sababu ulikuwa huweki akiba,” anasema.

Marry Charles (30) ni mwanamke anayemiliki mashimo maarufu kama maduara pamoja na mwalo wa kuchenjulia dhahabu katika mgodi wa Tambarare uliopo wilayani Kahama.

Anakiri kuwa starehe zilizopita kiasi ndiyo kikwazo kikubwa cha mafanikio ya vijana wengi wanaofanya kazi machimboni ikiwemo kwenye mgodi huo

“Wakipata pesa wanasahau wanafanya kazi ngumu, halafu hizo kazi ngumu wanazozifanya wanashindwa kutambua wanapopata pesa badala ya kufanya maendeleo wao wanajikita kwenye starehe zaidi kuliko miradi ya maendeleo,” anasema Marry.

Anaongeza kuwa, kwenye migodi mingi ikiwemo mgodi wa Tambarare biashara ya ngono imekuwa ikiwafanya vijana wengi kutumia pesa nyingi wanayoipata. Anaishauri serikali kuingilia kati kudhibiti biashara hiyo kwani mbali na kuwa kikwazo cha maendeleo kwa vijana pia inachochea mambukizi ya virusi vya ukimwi.

Mtazamo wa watu wazima migodini

Adrian Magoma (58), ni mkazi wa Bunda mkoani Mara ambaye ameamua kusafiri kuja Kahama kutafuta maisha kwenye machimbo hayo ya dhahabu anasema chimbuko kubwa la umaskini wa wachimbaji unatokana na mifumo kandamizi kwenye maeneo ya migodi.

Anasema yeye anamiliki mashimo ya kuchimba lakini gharama za kuhudumia mashimo ikiwemo kununua na kufunga matimba, kulipua miamba, kumwaga maji kwa mashine za umeme, ni kubwa zaidi ikilinganishwa na mapato halisi ya migodi.

Adrian anatolea mfano kwenye maduara anayomiliki akisema kwa kila mifuko 100 ya mchanga unaosadikika kuwa na dhahabu, asilimia 30 wanachukua wamiliki wa leseni, asilimia tatu wanachukua vibarua wanaozama mashimoni, kuna tozo ya serikali, tozo ya vijiji na kiasi kinachobaki ndiyo wanagawana wawekezaji walio na hisa.

“Leo unaweza kupata milioni 30, lakini katika mzunguko wote na mgawanyo unajikuta una faida ya shilingi laki tano tu, zingine zote zinapita, kwa hiyo unakuta yale mahitaji yote unayohitajika kuyafanya yanakwamia njiani,” anasema.

Leopord Petro (57) mwenyeji wa Biharamulo Mkoani Kagera anamaani kwamba kiini cha umasikini wa wachimbaji wadogo ni ukosefu wa mitaji na vifaa vya kutendea kazi huku maisha magumu waliyonayo yakisababishwa na kipato kidogo cha pesa na matumizi yakiwa ni makubwa.

“Nawashauri vijana ni bora waendelee na masomo tu maana mgodini ni sehemu moja mbaya sana. Ubaya wake pesa haipatikani vizuri ya kuweza kukidhi mahitaji yao, na pesa zenyewe zinapatikana kwa shida,” anaeleza.

Naye John Wiliam (49) anasema vijana wengi wanaofanya kazi kwenye machimbo hawafikii mafanikio ya kiuchumi kutokana na kutokuwa na malengo na kujisahau wanapopata pesa kutokana na mazoea ya kupata pesa za mara kwa mara pasipo matarajio na kuishia kutumia pesa nyingi kwenye starehe.

Anasema kazi za mgodini zina tija iwapo utazifanya kwa malengo kwani kwake yeye toka ameanza kuzifanya miaka mitatu iliyopita imemsaidia kupata mafanikio kadhaa ikiwemo kununua kiwanja na kujenga nyumba na ameweza kutoa mahitaji ya shule ya watoto kwa wakati.

“Vijana wanaokimbilia kuja migodini kwanza kabisa wawe na malengo, wasikimbilie kuja tu huku kula starehe, huku starehe zipo na pesa ipo ya mara kwa mara sasa unakuta wakati mwingine vijana wanabweteka, wanaona kwamba anapochukua pesa leo anajua na kesho ipo atapata, vijana wanapokuja wawe na mpangilio kabisa naenda kutafuta hiki,” anasema.

Ushauri mtaalamu wa uchumi.

Mtaaluma wa Masuala ya Uchumi Dk Lulu Olang' anasema ili kukabliana na changamoto hiyo kitu cha kwanza kuna haja ya kuwapatia elimu na njia za kumudu mtu pesa wanazopata na pia anashauri watu kujaribu kutotegemea shughuli moja ya uzalishaji hususani shughuli za uchimbaji pekee, badala yake kuwekeza kwenye mianya tofauti.

Anaongeza, ni lazima watu waweke mipango endelevu jinsi gani ya kujikwamua kichumi na kuweza kupiga hatua zaidi za maendeleo hata baada ya kuacha kazi za uchimbaji, na ni vyema vijana wajifunze kufanya utafiti na kujua aina ya uwekezaji wanaokusudia kuufanya ili kujua kama wana uwezo na muda wa kusimamia badala ya kuanzisha biashara kwa kufata mkumbo.

“Fanya utafiti hata ule mdogo, muda wangu unaruhusu kufanya hiyo biashara, kwa sababu unaweza kujikuta kwa mfano wewe upo machimboni miezi mitatu, minne, umeweka mtu kule anakuangalizia matikiti, siku mbili tatu shamba limeliwa halafu baadaye utakuja uanze kulalamika zaidi hujapata kitu, kwa sababu hukufanya utafiti kujua kama muda unaruhusu” anasema Dk Lulu.

Msaada wa Shirika la FADev

Evans Rubara ni Meneja wa Programu na Tafiti wa Shirika la Kuendeleza Wachimbaji Wadogo (FADev), anasema ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kupiga hatua shirika hilo linatoa elimu ya utunzaji taarifa za mapato, matumizi, na faida ambazo zinaweza kuwasaidia kupata mikopo na pia wanasaidia akina mama kupata ruzuku ili waweze kufanya shughuli za kijasiriamali tofauti na shughuli za mgodini.

“Tunatumia nafasi hii kuwapatia hayo mafunzo ambayo yatawasaidia kujua jinsi gani ya kuweka taarifa tofauti, umuhimu wa kuweka akiba kidogo kidogo, umuhimu wa kujua wamezalisha kiasi gani, wameuza kiasi gani, wamepata kiasi gani, wametumia kiasi gani, na faida yao inayobaki ni kiasi gani, je fedha ambayo wameitumia kama mtaji imerudi ama haijarudi, anasema Evans”

Anaongeza kuwa shirika hilo pia limekuja na mradi mahususi kwa ajili ya akina mama kwa kuwapatia mitaji, vifaa na mafunzo yatakayowasaidia kuendesha shughuli zao kibiashara zaidi.

Anasema kwa kushirikiana na Shirika la Women in Law and Development in Africa (WiLDAF), pi wanatoa elimu ya kuwasaidia kujikinga na ukatili wa kijinsia ambao pia umekuwa kikwazo cha kiuchumi kwa wanawake migodini.