Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 22Article 558979

Maoni of Wednesday, 22 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Nilichokiona kwa Yanga Nigeria

Nilichokiona kwa Yanga Nigeria Nilichokiona kwa Yanga Nigeria

Na Oscar Oscar

KUNA tofauti kubwa sana kwa Yanga tunayoiona kwenye magazeti na ile inayocheza uwanjani. Yanga ni kubwa sana ukiisikia.

Yanga ni kubwa sana ukisimuliwa. Unaweza kudhani ni Al Ahly! Unaweza kudhani ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Presha iko juu. Matarajio yako juu.

Ndugu zangu wana Yanga safari bado ni ndefu na imejaa wanyama wakali. Nchi ya ahadi bado iko mbali.

Nimepata nafasi ya kuishuhudia Yanga ikifungwa na Zanaco kwa Mkapa. Nimeiona Yanga ikifungwa na Rivers United kwa Mkapa. Nimeiona pia Yanga ikifungwa na Rivers United nchini Nigeria. Ni timu yenye historia kubwa inayohitaji uvumilivu.

Yanga bado ni ileile kwenye matokeo, lakini inaimarika kiuchezaji. Nimeiona Yanga iliyofungwa na Rivers United nyumbani. Nimeiona tena Yanga iliyofungwa na Rivers United ugenini. Matokeo bado ni yaleyale, lakini kiuchezaji Yanga imebadilika.

Walau Yanga imeanza kutazamika. Walau unaona kuna muunganiko wa timu. Mechi ya Rivers United pale Kwa Mkapa, Yanga ingeweza kufungwa hata goli tatu. Mechi ya juzi nchini Nigeria, Yanga ilistahili kushinda.

Ilitengeneza nafasi nyingi. Yanga waliangushwa mara mbili ndani ya eneo la penalti. Walau kuna kitu kinaanza kuonekana. Yanga wamefanya usajili mkubwa kuelekea msimu mpya, lakini wamekosa maandalizi sahihi. Timu ya mtindo huu huwa haihitaji presha. Ni timu inayotakiwa kupewa muda. Ni timu ambayo inaimarika taratibu. Ukitazama mechi ya Rivers United nchini Nigeria unamuona Bakari Mwamnyeto mpya. Unauona ubora wa Mwamnyeto yule misimu miwili ya pale akiwa na Coastal Union. Jitu la kutisha. komando wa vita. Jenerali aliyeiva.

Alipotakiwa kuruka juu alifanya hivyo. Alipotakiwa kugongana na wababe wa Rivers United alipambana. Kuimarika kwa Mwamnyeto ni ishara nzuri sana ya Yanga kufanikiwa. Timu bora zote duniani zinajengwa na wachezaji bora wa ulinzi kama Mwamnyeto.

Nimemuona Yannick Bangala Litombo. Huyu jamaa ni mtu na nusu. Ni Yaya Toure anayekipiga Jangwani. Ameifanya Yanga kuwa na utulivu mkubwa sana katikati. Fundi wa pasi. Kipande cha mtu. Mapafu ya mbwa. Amemfanya pia Tonombe Mukoko apumue.Amemfanya pia Feisal Salum kuwa huru na kazi ya ushambuliaji.

Ukitazama matokeo bado Yanga ni ileile. Lakini ukiwatazama uwanjani ni watu wanaoimarika kila kukicha. Ni timu inayozidi kukaa sawa. Ni timu inayohitaji uvumilivu. Wanachopitia kwa sasa walitakiwa kukipitia wakati wa maandalizi (pre-season).

Gharama wanayopitia Yanga kwa sasa ni matokeo ya kutokuwa na maandalizi sahihi. Mpira hauna njia ya mkato, Yanga lazima wakubali.

Nimeitazama Yanga Dar es Salaam ikifungwa na Zanaco. Nilikuwepo wakifungwa na Rivers United. Matokea yao bado ni yaleyale lakini hawa jamaa wanaimarika. Yanga inazidi kukaa sawa. Nimemuona Feisal akicheza juu ya Yannick Bangala na Tonombe Mukoko yuko huru zaidi.

Anaendesha timu vizuri. Muda si mrefu tutaanza kumuona akipiga pasi za mwisho. Muda si mrefu tutaanza kumuona akifunga mabao. Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi.

Baada ya kukosa maandalizi mazuri ya mwanzo wa msimu ilikuwa ni lazima Yanga wapitie tabu hii. Nimemuona Jesus Moloko ni winga haswa. Ana kasi. Ana kontro. Siyo muoga. Ni suala la muda tu. Nilimuona pale Dar es Salaam dhidi ya Zanaco. Nimemuona Port Harcourt nchini Nigeria. Ni fundi halisi wa mpira.

Bado Yanga ni kubwa mno unaposimuliwa kuliko unayoiona uwanjani, lakini wanazidi kuimarika. Yanga ni kubwa ukiisoma magazetini kuliko inayoonekana uwanjani lakini ni suala la muda tu.

Muda si mrefu tutaanza kuona soka safi. Muda si mrefu tutaanza kuona burudani. Nimemtazama kocha kwenye mechi za Rivers United nyumbani na Ugenini. Nimemuona kocha amebadilika. Nimemuona Nabi anafanya kazi nzuri. Hakuna kazi ngumu kwenye ukocha kama kufanya mabadiliko ya wachezaji na mfumo wakati mchezo unaendelea.

Mpaka sasa Kocha Nabi hajawa na wachezaji wake wote kwenye mechi hata moja. Wanafungwa na Rivers United kikosini hakuna Khalid Aucho, Djuma Shabani wala Fiston Mayele.

Hawa Wachezaji watatu watakuja kutuonyesha picha nyingine tofauti ya ubora wa Yanga. Hawa watakuja kuongeza nguvu na ubora kikosini. Bado Yanga ni ileile kwa kutazama aina ya matokeo ya timu mpaka sasa, lakini kiuhalisia wanaonekana kuimarika kila kukicha.

Yanga imesajili wachezaji wengi wazuri, lakini bado hawana timu. Kuipata timu siyo kazi ndogo, lakini naona taratibu wanazidi kuimarika.

Maombi yako ni muhimu kwao katika kipindi hiki kigumu. Nchi ya ahadi huwa haifikiki kirahisi. Inahitaji watu wavumilivu na watu wanaoongea lugha moja.

Kwa maoni nitumie kwenye namba: 0658 376417