Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 20Article 579778

Maoni of Monday, 20 December 2021

Columnist: www.tanzaniaweb.com

Nyuma ya Pazia: Haishangazi, bishoo Auba hakuzaliwa kuwa nahodha

mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang

Baada ya kila kitu walichokiona katika miguu yake, maneno yaliisha katika midomo yao wakaamua kumjengea mnara katika mji wao wa Florence. Heshima kwake. Gabriel Omar Batistuta aliwaingia watu wa mji wa Florence katika mioyo yao kiasi hiki.

Aliwafungia mabao 168 katika mechi 269. Wakamgeuza mungu mtu. Mpira ulipoisha miguuni na akilini akaondoka, lakini huku nyuma katika mji wa Florence wakamuenzi kwa kumjengea mnara. Inatokea mara chache katika maisha ya mwanadamu wa kawaida. Batistuta alikuwa mmoja wao.

Kilichonishangaza ni kwamba wakati uleule anacheza soka Batistuta aliwahi kufanya mahojiano fulani mahala pale Italia. Akadai kwamba mchezo wa soka sio mchezo unaomfurahisha. Sio mchezo anaoupenda. Alikuwa anacheza tu kama kazi yake. Asingepoteza muda wake kukaa mbele ya televisheni kutazama soka.

Baada ya Batistuta kunishangaza nikagundua kitu. Walikuwepo wachezaji wengi wa aina yake. Benoit Assou-Ekoto aliwahi kusema hivyo. Kipa wa Barcelona, Marc-Andre Ter Stegen aliwahi kusema hivyo. Tofauti na fikra zetu kwamba wachezaji wetu ni mashabiki kama sisi. Hapana.

Katika orodha hii nimemuongeza Pierre-Emerick Aubameyang. Hajawahi kutamka hivyo, lakini namuona hivyo. Majuzi Arsenal wamemvua unahodha. Kinachonishangaza sio kumvua, kinachonishangaza ni kwanini hata walimpa unahodha wenyewe. Kuna vigezo vya unahodha, lakini Auba hana.

Alizaliwa na kipaji kikubwa cha kufunga, basi. Na wala hakupewa kipaji cha kuhangaika uwanjani au kujihangaisha. Kipaji chake cha kufunga kimempa maisha. Katika soka kufunga ni miongoni mwa kazi ngumu zaidi. Auba anaijua vyema kama kipaji na ametumia kipaji hiki kupata maisha. Kuishi uzunguni mwa London, kuishi uzunguni mwa Paris, kuendesha kila aina gari zuri unalolifahamu. Kuanzia Bugatti hadi Ferrari.

Hata hivyo, ninapotazama lugha yake ya mwili akiwa ndani na nje ya uwanja nagundua kwamba Auba ni bishoo tu anayekula maisha kwa sababu ya kipaji. Hauwezi kumlaumu kwa sababu kuna watu ambao ni wagumu lakini hawawezi kufunga kama yeye. Kwanini Arsenal walimpa unahodha? Sielewi.

Ni kweli ukipiga tathmini ya wakati Auba anapewa unahodha na Unai Emery unagundua kwamba alikuwa mchezaji staa zaidi kikosini. Mchezaji mwenye thamani zaidi kikosini. Alikuwa pia mchezaji mwenye haiba zaidi kuliko wenzake. Hata hivyo hakuwa na sifa ya unahodha.

Achilia mbali kufunga, hauwezi kumkuta Auba anafokea makosa ya wenzake. Hauwezi kukuta Auba anapewa kadi ya njano kwa kumfokea mwamuzi wala mchezaji wa timu pinzani. Hauwezi kumuona Auba anatoa jasho lake la mwisho kwa ajili ya timu. Anacheza tu kwa sababu muda wowote atakufunga kutokana na kipaji chake alichopewa na Mwenyezi Mungu. Mengine hayamuhusu.

Auba anaweza kuwa nahodha wa timu ya taifa. Siku hizi ni rahisi kuwa nahodha wa timu ya taifa hata kama hauna sifa yoyote ya kuwa nahodha. Ukiwa staa mkubwa kuliko wengine wote basi moja kwa moja unakuwa nahodha hata kama hauna sifa za unahodha. Mpaka sasa siamini kama kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wana sifa za unahodha.

Wamepewa katika nchi zao kwa sababu wamekuwa mastaa zaidi. Zamani hali hii haikuwepo. Ndio maana Dunga alikuwa nahodha mbele ya Romario na Bebeto pale Marekani mwaka 1994 wakati Brazil wakichukua Kombe la Dunia kwa njia ya matuta.

Katika klabu utamaduni wa manahodha asilia unapaswa kudumishwa. Labda ndio maana Jordan Henderson ni nahodha Liverpool zaidi ya Mohammed Salah. Labda ndio maana pale Real Madrid, Sergio Ramos alikuwa nahodha mbele ya Ronaldo. Hata leo pale Liverpool kama Henderson akiondoka basi Virgil Van Dijik atapaswa kupewa kitambaa mbele ya Salah na Sadio Mane.

Turudi kwa Auba. Majuzi alifanya kosa lake la tatu Arsenal kama nahodha. Alipewa ruhusa ya kwenda kwao Ufaransa kumchukua mama yake ambaye ni mgonjwa. Alipaswa kurudi Jumatano, yeye akarudi Alhamisi. Jumatano aliyopaswa kurudi yeye aliposti picha mitandaoni akichorwa tattoo mkononi.

Haya yote anayafanya huku fomu yake ikiwa mbovu. Siku hizi hafungi sana. Hili ndio jambo ambalo nadhani limewakasirisha zaidi mashabiki wa Arsenal kiasi cha kusimama nyuma ya Mikel Arteta na watu wengine waliochukua uamuzi wa kumvua unahodha. Kwa siku za karibuni Arsenal inabebwa na watoto kina Bukayo Saka na Emile Smith Rowe kuliko Auba.

Achilia hili la unahodha, lakini Arsenal wenyewe wanaonekana pia kuachana na Auba mwenyewe. Tangu aongezewe mkataba mpya ambao unampatia Pauni 350,000 kwa wiki haonekani kuwa bize uwanjani. Pesa inaingia, maisha yanataka nini zaidi? Kuna kitu bora zaidi ya pesa?

Nini hatima yake? Sifahamu sana. Nataka tu kujua kama Auba atafanya kama kile ambacho Mesut Ozil aliwafanyia Arsenal. Ozil aliongezewa mshahara mkubwa nafasi yake ikapotea klabuni kwa sababu ya uvivu wake akaamua akae benchi tu, huku akila kuku. Auba anaweza kufuata njia hii pia.

Kwanza ana mkataba na Arsenal, lakini pili mshahara wake ni mkubwa. Klabu inayomtaka inabidi imnunue halafu pia imlipe mshahara kama ule anaolipwa na Arsenal au zaidi. Kidogo pana ugumu hasa kipindi hiki ambacho wakubwa wapo hoi kiuchumi. Nasikia Xavi Hernandez anamtaka pale Catalunya, lakini itabidi apambane kwanza kurekebisha vitabu vyake kwa kuuza wachezaji kabla hajavamia kariba ya kina Auba.

Vinginevyo Auba anaweza kuwa amepigwa kibao mgongoni. Anaweza kurudi na kupambania heshima yake. Hapo katika kuipambania nimesema lakini sina uhakika sana. Kama nilivyosema hapo juu, Auba anajua tu kufunga, lakini sina uhakika kama huwa anang’ata sana meno anapokuwa ndani au nje ya uwanja.

Mwisho wa siku vyovyote ilivyo kila mmoja anaweza kuishi bila ya mwenzake. Tunakoelekea Arsenal wameonyesha wanaweza kuishi bila ya Auba. Wameshinda vizuri tu katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Southampton na West Ham ambao ni wagumu kwa sasa. Na hata wakiwa na Auba walikuwa wanafungwa tu. Lakini hata Auba pia anaweza kuishi bila ya Arsenal. Popote alipo anaweza kufunga tu kwa sababu amezaliwa kwa ajili hiyo. Tatizo labda linarudi palepale tu katika mshahara. Wakubwa wengi kwa sasa hawamudu kutoa Pauni 350,000 kwa wiki kwa urahisi, hasa baada ya matatizo ya Uviko-19.

Haishangazi kuona kuna mastaa wengi wakubwa wanatazamiwa kuwa huru katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto. Sio kwa bahati mbaya, klabu zimechemsha kuwaongezea mikataba ya bei mbaya. Tafuta orodha ya wachezaji ambao wanaweza kupatikana bure mwishoni mwa msimu ujao. Hautaamini.