Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 17Article 551872

Maoni of Tuesday, 17 August 2021

Columnist: www.mwananchi.co.tz

Panda shuka ya uswahiba wa Uhuru Kenyatta, Ruto

Panda shuka ya uswahiba wa Uhuru Kenyatta, Ruto Panda shuka ya uswahiba wa Uhuru Kenyatta, Ruto

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Naibu Rais, William Ruto wamepata kuwa kielelezo cha ‘ndoa’ imara ya kisiasa. Hata hivyo, dhahiri shahiri ndoa yao inaelekea kuvunjika, wakati Taifa la Kenya likijielekeza kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti mwakani.

Ni kama uswahiba wa Uhuru na Ruto unashikiliwa na uzi mwembamba. Uhuru ni Rais, Ruto naibu rais. Kwa namna ambavyo hali imeshakuwa, wachambuzi wengi wa siasa Afrika Mashariki, wanaamini ingekuwa hekima kubwa kwa Ruto kujiondoa, kuliko kung’ang’ania ofisi, maana hana maelewano na bosi wake.

Hivi karibuni, Ruto alikuwa afanye ziara nchini Uganda, lakini safari yake ilifutwa na mamlaka iliyo juu yake. Bila shaka ni Rais Uhuru. Pamoja na hilo, Ruto amebaki ofisini. Hali hiyo ndio inasababisha akumbushwe kilichotokea nchini humo mwaka 1966.

Oktoba 1966, aliyekuwa Makamu wa Rais wa kwanza Kenya, Jaramogi Oginga Odinga, alizuiwa kusafiri kwenda Uganda, alipokuwa Uwanja wa Ndege wa Embakasi, siku hizi unaitwa Jomo Kenyatta International Airport. Baada ya kuzuiwa, Jaramogi aliamua kusafiri kwa basi, lakini akiwa Busia, msafara wake ulisimamishwa na kupekuliwa kwa saa mbili.

Jaramogi, alikuwa kwenye safari moja na aliyekuwa mwanasiasa mahiri, kijana, Tom Mboya, ambaye wakati huo naye alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba. Kwa kitendo hicho, Jaramogi aliamua kujiuzulu umakamu wa rais, kwa kile alichoona kwamba hakuwa kwenye maelewano na Rais Kenyatta.

Agosti 2, mwaka huu, Ruto, alizuiwa Uwanja wa Ndege wa Wilson, alipokuwa anasafiri kwenda Uganda. Alipofika uwanjani kwa ajili ya safari, aliambiwa hawezi kuondoka mpaka ruhusa itolewe na kiongozi wake, Uhuru. Ruto alingoja uwanjani kwa saa 5 na dakika 30 bila majibu kutoka kwa Uhuru, mwisho safari ikaahirishwa.

Wachambuzi wa siasa za Kenya, wanapendekeza kuwa Ruto alipaswa kujiuzulu kama Jaramogi, baba yake Raila Odinga, ili kulinda heshima yake na hadhi ya kiti cha naibu rais. Kuendelea kubaki ofisini kunatafsiriwa kuwa Ruto anaona cheo cha naibu rais ni kitamu kuliko heshima na utu wake.

Pamoja na mtikisiko ambao Ruto anakutana nao kisiasa hivi sasa na kuashiria mwisho kwa ndoa ya kisiasa kati yake na Uhuru, hata hivyo, mpaka kufikia wakati huu ni dhahiri Uhuru na Ruto wamepenya hatua kubwa. Na wametoka mbali.

Jinsi walivyovuka pamoja muhula mmoja wakiwa imara na walivyoanza muhula wao wa pili kuelekea mwaka 2022, ilitoa tafsiri kwamba ama ni waaminifu sana au waliweza kudhibiti maneno na vitendo vyenye matokeo ya kuwafarakanisha.

Uhuru na Ruto walishinda urais wa Kenya Machi 4, 2013. Walimaliza muhula wao wa kwanza salama na kuingia mwenye Uchaguzi Mkuu Kenya Agosti 8, 2017. Hata baada ya Mahakama Kuu kutengua matokeo ya ushindi wao, walishikamana na kushinda tena uchaguzi wa marudio Oktoba 26, 2017.

Novemba 28, 2017, Uhuru na Ruto walikula kiapo cha uaminifu kuiongoza Kenya, Uhuru kama Rais na Ruto kama Naibu Rais, ikiwa imepita miaka minne ya ushirikiano wa pamoja kama kiongozi mkuu wa nchi na msaidizi wake namba moja, tangu walipoapa Aprili 9, 2013.

Huko nyuma, sababu iliyoonekana kuwabeba Uhuru na Ruto ni kila mmoja kutambua nafasi yake na kumheshimu mwenzake. Uhuru kumheshimu Ruto kama msaidizi na mshirika wake kiutawala, vilevile Ruto kutambua hadhi na mamlaka ya Uhuru kama Rais, pasipo kuingiliana.

Ni sababu hiyo Uhuru na Ruto hawakuwa wakionekana kama washirika wa madaraka peke yake, bali marafiki walioshibana. Daima walicheka wakiwa pamoja, kugonganisha mikono na kutajana kwa furaha kudhihirisha namna ndani yao kulivyo na urafiki kuliko kuunganishwa na vyeo.

Uhuru na Ruto walipanda madaraja ya kisiasa kupitia chama cha Kenya African National Union (Kanu) ambacho kilizaliwa Mei 14, 1960 kisha kuongoza mapambano ya kudai uhuru wa Kenya na kufanikiwa Desemba 12, 1963.

Kanu iliboreshwa kutoka Kenya African Union (Kau) ilichozaliwa mwaka 1947. Kabla ya kuwa Kau, chama hicho kilijulikana kama Kenya African Study Union (Kasu) kuanzia mwaka 1942. Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta alipojiunga na Kasu kisha kuchaguliwa kiongozi, aliliondoa neno “Study” hivyo kubakisha Kenya African Union (Kau).

Uhuru alizaliwa Oktoba 26, 1961, ikiwa ni takriban miaka miwili kabla ya Kenya kupata uhuru. Hivyo wakati Kenya inapata uhuru hakuwa na ufahamu wowote. Ruto alizaliwa Desemba 21, 1966, kwa hiyo wakati Kenya inafikisha miaka mitatu na siku tisa, ndipo Ruto alizaliwa.

Ruto pia ni mwanasiasa aliyejitengeneza mwenyewe. Alitokea familia ya kimasikini. Akasoma katika mazingira magumu akiuza karanga, kuku na bidhaa nyingine ndogondogo, yote hayo alifanya kuhakikisha anatimiza malengo yake ya kielimu na kimaisha kwa jumla.

Alisoma chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya na kupata shahada ya kwanza na ya uzamili katika mchepuo wa Sayansi ya Mimea (Botany). Mwaka 1990 akiwa na umri wa miaka 24, Ruto alianzisha kampuni ya masuala ya utalii aliyoiita, African Venture Tours and Hotels.

Itaendelea kesho