Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 25Article 544195

Maoni of Friday, 25 June 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Polisi mikoa mingine waige mbinu hii ya Dar

Polisi mikoa mingine waige mbinu hii ya Dar Polisi mikoa mingine waige mbinu hii ya Dar

JUZI Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilitangaza donge la Sh milioni mbili kwa yeyote atakayetoa taarifa sahihi zitakazowezesha kukamatwa kwa majambazi na hasa kupatikana silaha, yaani bunduki au bastola.

Kamanda wa polisi katika kanda hiyo, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Jumanne Muliro alisema lengo la kutangaza donge hilo ni kuchochea moyo wa uzalendo zaidi kwa raia wema kushiriki kupambana dhidi ya vitendo vya uhalifu.

Kimsingi, ni wazi kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa raia na mali zao lipo mikononi mwa Jeshi la Polisi, lakini wananchi pia wana nafasi yao ya kizalendo ya kukataa kushiriki, kuhifadhi wahalifu na mali za uhalifu au kuwalinda na kuwatetea.

Ndiyo maana tunaamini, lengo la polisi kutangaza zawadi hiyo si kulipa ujira kwa watoa taarifa, bali kuwatia shime zaidi kama ilivyo kazi ya zawadi yoyote kwamba ni kuchochea moyo wa ufanisi.

Kamanda Muliro alisema: “Mwenye taarifa zinazohusu jambazi ziwe sahihi na ambazo zitafanikisha kumkamata akiwa na silaha, donge hilo litatolewa palepale baada ya kufanikisha kumkamata mtuhumiwa na si tu mtuhumiwa, bali silaha.”

Sisi tunasema, tangazo la donge hili liwe kichecheo cha utamaduni wa wakazi wa Dar es Salaam na mikoa mingine kuukataa uhalifu ukiwamo ujambazi wa kutumia silaha kwa vitendo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia utoaji wa taarifa sahihi za kuzuia uhalifu na kuwakamata wahalifu na silaha zao.

Tunasema hivyo tukiamini kuwa, mara zote Jeshi la Polisi limekuwa likisisitiza watoa siri wanalindwa na watazidi kulindwa na kwamba, inapotokea ikabainika kuwapo ‘kidudumtu” wanaofichua watoa siri, hao nao wanapobainika lazima wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na kiutumishi.

Ndio maana tunasema, katika mapambano dhidi ya uhalifu, lengo kubwa la raia wema liwe kuzuia na kupambana na uhalifu maana uhalifu mahali popote ni sawa na jiwe linalorushwa kundini maana hakuna ajuaye litamdhuru nani na kwa namna gani.

Tunapoliomba Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendeleza operesheni yake kupambana na uhalifu hadi uishe huku likihidi kuwalinda watoa taarifa, tunaishauri mikoa mingine nayo kuanisha utaratibu huu wa kutoa motisha kwa watoa taarifa zinazowezesha kukamatwa kwa wahalifu na silaha.

Tunalishauri pia Jeshi la Polisi kutangaza zawadi kwa wote wanaotoa taarifa za kuwezesha kuzuia uhalifu na kuwakamata wahalifu hususan majambazi wa kutumia silaha.

Tuna amini hili litawezesha operesheni inayoendelea ya kupambana na uhalifu kuzaa matunda. Hata hivyo, tunashauri kuwa, kutangaza zawadi kufanyike hadharani, lakini wanaopewa zawadi wapewe kwa siri ili wasijulikane.

Ndiyo maana tunasema, polisi katika mikoa mingine waige mbinu iliyotangazwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.