Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 15Article 571486

Maoni of Monday, 15 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

RESPECT: Hili ndilo chama la ubingwa!

RESPECT: Hili ndilo chama la ubingwa! RESPECT: Hili ndilo chama la ubingwa!

KWA misimu minne mfululizo, Yanga imekuwa ikihaha kurejesha heshima yake katika Ligi Kuu Bara.

Ndio, kwa muda wote huo wa miaka minne, Yanga imepoteza ufalme wake iliyokuwa nayo mikononi mwa Simba iliyiobeba ubingwa wa Ligi Kuu misimu yote minne mfululizo.

Rekodi zinaonyesha Yanga ilibeba ubingwa wa mwisho msimu wa 2016 2017 ukiwa ni wa tatu mfululizo kwao na baada ya hapo watani wao waliwanyang’anya na kuendelea kuutetea kibabe kwa misimu hiyo yote na kuwafanya mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani kuwa wanyongeee!

Lile chama lililotwaa ubingwa kwa mara ya mwisho Jangwani bado limeendelea kupata heshima yake, kwani mastaa wengine walioingia na kutoka wameshindwa kuipigania timu na kurejesha taji hilo, japo kwa msimu huu mashabiki wamekuwa na imani kubwa kuwa watapindua meza.

Mwanaspoti linakuletea kikosi hicho ya ubingwa cha Yanga likichobeba ndoo ya Ligi Kuu Bara kwa mara ya mwisho kwa kuifumua Toto Africans bao 1-0 lililowekwa kimiani na Amissi Tambwe dakika ya 82, licha ya mechi ya kukabidhiwa ubingwa ilikubali kichapo cha bao 1-0 toka kwa Mbao FC.

Hapo chini ni kikosi kilichoihakikishia Yanga ubingwa huo wa mwisho pamoja na wachezaji wengine waliokuwa Jangwani msimu huo sambamba na makocha wao, ikieleza sehemu walipo sasa. Endelea...!

BENO KAKOLANYA

Ni kipa aliyekaa langoni katika mechi ya mwisho ya Yanga ya kukabidhiwa ubingwa, akiwa amesajiliwa msimu huo kutoka Tanzania Prisons na ndiye aliyekuwa chaguo la kwanza akisaidiana na Deogratius Munishi ‘Dida’.

Kakolanya sasa anakipiga Simba na ni kipa namba mbili kutokana na kushindwa kumtoa langoni Aishi Manula ambaye tangu amesajiliwa akitokea Azam FC amekuwa akikaa langoni na kufanya vizuri.

JUMA ABDUL

Beki huyo aliyesifika kwa kasi na kupiga krosi zenye macho, alisajiliwa Yanga akitokea Mtibwa Sugar na kuwa mhimili imara wa klabu hiyo naye alikuwa katika mechi hiyo iliyowapa ubingwa Yanga na kwenda kuidhinishwa rasmi jijini Mwanza katika mechi dhidi ya Mbao na kupoteza 1-0, ambapo katika mechi hiyo ya CCM Kirumba alisimama Hassan Kessy katika nafasi hiyo ya beki wa kulia.

Kwa sasa Abdul anaichezea klabu ya DTB iliyopo Ligi ya Championship iliyomsajilia akitokea Zambia alikoenda kucheza soka la kulipwa msimu uliopita alipoachana na Yanga.

HAJI MWINYI

Ndiye aliyekuwa beki wa kutumainiwa Yanga na kupewa jina la beki wa kumwaga maji kutokana na krosi zake zilizokuwa zinatengeneza mabao tangu ameondoka Yanga hana maisha mazuri kwenye timu za Bara.

Mwinyi sasa amerudi visiwani na anakipiga katika klabu ya KMKM timu ambayo imemlea tangu alipoanza kucheza soka na kumpatia ulaji Yanga ambayo iliachana naye baada ya mkataba wake kuisha.

KELVIN YONDANI

Alikuwa beki panga pangua kikosi cha kwanza cha Yanga na kufanikiwa kupewa uongozi ndani ya timu hiyo kutokana na heshima yake na kucheza kwa muda mrtefu ndani ya timu hiyo akiwa na kiwango bora.

Yondani ameondoka Yanga msimu uliopita baada ya mkataba wake kuisha na kushindwa kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya sasa anakipiga Polisi Tanzania ambapo pia amejijengea ufalme beki ya kati kutokana na uwezo wake.

VICENT BOSSOU

Beki huyo mwili jumba aliyesajiliwa kutoka Togo, ndiye aliyesimama kwenye mechi hiyo ya Toto, lakini katika mechi ya Jijini Mwanza, alimpisha nahodha wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Beki huyo kisiki alisimama imara akipokezana na mabeki wenzake wa kati katika msimu huo akiwamo Andrew Vincent ‘Dante’ na Cannaravo na aliisaidia timu kuwa imara eneo la nyuma.

Kwa sasa yupo klabu ya Pattani FC ya Thailand iliyomsajili baada ya kuondoka Jangwani mara baada ya kumaliza mkataba wake.

NADIR HAROUB ‘CANNAVARO’

Alikuwa beki kitasa akisaidiana na Yondani kuzuia mashambulizi ya washambuliaji na alimudu nafasi hiyo hadi alipoamua kustaafu kucheza soka na kupewa umeneja wa timu kwa muda na baadaye kuondolewa.

Canavaro sasa ni meneja wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ akiongoza baadhi ya wachezaji ambayo alishawahi kucheza nao amekuwa mhimili mkubwa kwenye timu hiyo kutokana na kuwa na wakati mzuri kuwashauri na kumuelewa kutokana na kutambua ukubwa wake kwenye soka.

THABANI KAMUSOKO

Ni kiungo ambaye alikuwa fundi ndani ya kikosi na kutengeneza timu ambayo ilikuwa inagongeana pasi hadi kuwafanya mashabiki mitaani watambe kuwa wanatimu nzuri ya kampa kampa tena alidumu kikosini na kuisaidia timu hiyo kutwaa mataji mawili mfululizo.

Baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili alirudi nchini kwao na sasa anakipiga katika klabu ya Zesco United, huku akiitumikia pia timu ya taifa lake la Zimbabwe.

JUMA MAHADHI

Ni moja ya mawinga ambao walitua Jangwani kwa mkwara mwingi akitokea Coastal Union na kupokezana nafasi hiyo na mkali wao, Simon Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa Morocco.

Winga huyo alicheza vizuri kwenye mchezo huo ambao Tambwe ndiye aliyefunga bao pekee lililoihakikishia Yanga ubingwa licha ya kudhibitishwa mwisho wa ligi Yanga wakibeba kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Simba.

Kwa sasa Mahadhi anakipiga Geita Gold baada ya msimu uliopita kukipiga Ihefu iliyoshuka daraja hadi Championship.

HARUNA NIYONZIMA

Baada ya kutwaa taji la mwisho la Ligi akiwa Yanga aliondoka na kuhamia kwa wapinzani wao Simba na baadaye kurudi tena lakini hajachukua muda kaondolewa kikosini.

Niyonzima sasa amerudi nchini kwao ambapo anakipiga katika timu ya AS Kigali akiungana na aliyekuwa beki wa kati wa Yanga Lamine Moro.

AMISSI TAMBWE

Desemba 16 alijiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja akitoka kwa watani zao Simba ambao walimuacha kwa madai kuwa kiwango chake kimeisha na amemaliza msimu akiwa na timu hiyo kwa kuibuka kuwa mfungaji bora.

Sasa anakipiga DTB ligi daraja la kwanza (Champion Ship) anakiwasha huko na ndiye anayeongoza kwa upachikaji wa mabao akiwa ameingia kambani mara nanae kwenye michezo sita waliyocheza.

OBREY CHIRWA

Ulikuwa ni msimu wake wa kwanza akisajiliwa kutoka timu ya FC Platinum za Zimbabwe aliingia na neema kwa kuingia tu na kutwaa taji ambalo lilikuwa la mwisho kwa Yanga hadi sasa ambapo Simba ni mtetezi akitwaa mara nne mfululizo.

Chirwa sasa anakipiga Namungo akisajiliwa akitokea Azam FC ambapo alisaini mkataba wa mwaka mmoja baada ya kumaliza uongozi haukuwa na mpango wa kumuongeza mpya.

GEOFREY MWASHIUYA

Mwashiuya alitua Yanga 2015 akitokea kwao Mbozi katika timu ya Kimondo iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza kwa kandarasi ya miaka mitatu alikiwasha ndani ya timu hiyo na kuwafunika Deus Kaseke na Juma Mahadhi ambao ndio walikuwa wanacheza nafasi hiyo.

Hakuchukua muda ndani ya Yanga akatoka na kujiunga na Singida United, Kagera Sugar na Mbeya City.

AKIBA

Deogratius Munishi (hana timu kwa sasa), Hassan Kessy anakipiga KMC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa sasa ni Meneja wa Taifa Stars, Matheo Anthony kwa sasa anakipiga KMC, Deus Kaseke bado yupo Yanga, Emmanuel Martin anakipiga kwa sasa Dodoma Jiji na Justine Zulu, kiungo huyo wa alipotoka Yanga alirudi timu yake ya zamani Red Arrows kisha kutua Nakambala Leopards alipo hadi sasa.

WENGINE KIKOSINI

Ally Mustafa ‘Barthez’, kipa huyu aliyesajiliwa kutoka Simba, alikuwa miongoni mwa makipa wa Yanga msimu huo kwa sasa ni kocha wa makipa wa Mbeya Kwanza, baada ya kuzidakia timu kadhaa ikiwamo Ndanda na Singida United mara alipoachwa na Yanga.

Donald Ngoma straika huyo alipoondoka Yanga alienda Azam na sasa amerejea FC Platinum ya kwao Zimbabwe, Oscar Joshua aliyechezea mechi ya mwisho ya Yanga ndani ya msimu huo jijini Mwanza na kupasuka mbele ya Mbao FC, amestaafu soka kwa sasa, Pato Ngonyani, kiungo huyo mkabaji anayemudu pia beki ya kati alipoondoka Yanga alitua Polisi Tanzania msimu uliopita kabla ya sasa kukipiga Mbeya City, Said Juma ‘Makapu’ anakipiga Polisi Tanzania kwa sasa akijiunga msimu huu baada ya kutemwa Jangwani. Mbuyiu Twite, beki huyu wa kulia naye alikuwa sehemu ya kikosi hicho cha ubingwa wa msimu huo, kabla ya kutimka zake umangani kucheza soka la kulipwa.

MAKOCHA

George Lwandamina, huyu ndiye aliyeipa timu hiyo ubingwa huo wa mwisho akimpokea Hans Pluijm, aliyebadilishiwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi kabla ya kutimkia Singida United na baadaye Azam.

Lwandamina aliyetua Jangwani kipindi hicho akitokea Zesco United akitoka kuifikisha timu hiyo nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa sasa yupo Azam FC iliyomrejesha nchini akitokea Zambia.

Wakati Lwandamina akiibebesha Yanga ubingwa huo wa mwisho na kuifikia nusu fainali ya Kombe la ASFC na kutemeshwa ubingwa na Mbao kwa kufungwa bao 1-0 lililotokana na kujifunga kwa beki wa kati Andrew Vincent ‘Dante’, msaidizi wake alikuwa ni Juma Mwambusi pamoja na Noel Mwandila.