Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 21Article 538876

xxxxxxxxxxx of Friday, 21 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais Samia: Maneno basi, tujenge bomba

RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza wote wanaohusika na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania wakamilishe mikataba iliyobaki ili mradi huo uanze.

Aliyasema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam, katika hafla ya utiaji saini mkataba wa nchi hodhi (HGA) wa ujenzi wa bomba hilo kati ya Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) na Serikali ya Tanzania.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais Samia, viongozi wa kampuni za uwekezaji wa mradi huo wakiwemo wa kampuni ya Total, Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),Shirika la Taifa la Mafuta la China (UNOOC) na viongozi wa serikali na wa sekta binafsi.

Mkataba huo kwa upande wa EACOP ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Martin Tiffen na kwa upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani.

“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa pande zote mbili kuhakikisha tunakamilisha majadiliano ya mikataba iliyobaki ili mradi huu uanze kutekelezwa na hatimaye ikifika mwaka 2025 mafuta yaanze kusafirishwa, wananchi wetu wamesikia maneno haya kwa miaka mitano nyuma sasa tuache maneno twende tukatekeleze,” alisema Rais Samia.

Alisema kupitia mkataba huo, Tanzania imeridhia bomba la mafuta lijengwe katika ardhi yake na pia ijengwe bandari ya kupokelea mafuta ghafi, Chongoleani mkoani Tanga.

Samia alisema kilometa 1,147 kupita Tanzania ndani ya mikoa minane na wilaya 24 kutatoa ajira nyingi, hivyo kuchangia deni la kuzalisha ajira zaidi ya milioni saba zinazotarajiwa kuzalishwa na serikali kwa kipindi cha miaka mitano.

Mradi huo unaotarajia kusafirisha mapipa ya mafuta bilioni 6.5 utaongeza mapato mengi kwenye nchi mbili akitolea mfano kwa Tanzania kwamba mbali na gawio la hisa kwa kampuni ya asilimia 15 lakini itapata asilimia 60 ya mapato ya kodi na Uganda itapata asilimia 40.

Samia alisema pia mradi huo utatochea shughuli za utafutaji wa pamoja wa biashara ya mafuta na gesi kwenye eneo la Afrika Mashariki hasa ikizingatiwa kuwa, nchini kuna mategemeo ya kupata mafuta katika Ziwa Eyasi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kwamba muundombinu utakaotumika ni bomba hilo la mafuta.

Samia alisema faida ya tatu ni kwamba Tanzania imefanikiwa kupata gesi hivyo mradi huo wa bomba la mafuta, utatoa njia ya kujenga bomba la gesi kusafirisha bidhaa hiyo nchini Uganda na nchi za jirani.

Faida ya nne kwa mujibu wa Samia mradi huo utasaidia kuwavuta wawekezaji wa kimataifa kwenye ukanda huu na kuondoa taswira ya muda mrefu iliyojengeka kwamba Afrika ni Bara la vita, njaa kutokuwa na mazingira bora ya biashara na uwekezaji, hivyo mradi huo utasaidia kuondoa taswira hiyo mbaya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Museveni aliipongeza Tanzania kwa mwelekeo wa maendeleo ya kiuchumi yanayogusa ukanda mzima wa Afrika Mashariki katika utoaji wa huduma, mambo ambayo alikuwa akiyazungumza mara nyingi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Sasa tumepata uelekeo na tutatumia rasilimali hizi zenye ukomo kama mafuta kuendeleza zisizo na ukomo kama kilimo na huduma. Wakati mafuta yakiisha nchi itakuwa kwenye hatua nyingine. Asante Tanzania leo kusiani mkataba huu na kuonesha ushiriki katika mradi huu,” alisema Museveni aliyehutubia kwa Kiswahili huku akiingiza misamiati mipya ya Kiganda na kumuomba Rais Samia amuunganishe na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita).

Hatua inayofuata sasa

Waziri wa Nishati, Dk

Kalemani alisema kusainiwa kwa mkataba huo kunawezesha kuanza kutekelezwa kwa mradi huo.

Dk Kalemani alizitaja hatua ya kwanza kuwa ilikuwa ni kusaini mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda kupitisha mafuta takribani mapipa bilioni 5.6 nchini Tanzania kwenda nje.

Alisema kazi muhimu za mradi ni tano, ya kwanza ni ujenzi wa bomba lenyewe la urefu wa kilometa 1,443, ya pili ni kujenga maeneo ya vituo vinane kwa nchi zote mbili kusukuma mafuta; viwili Uganda na sita Tanzania ambapo vya Tanzania vinne vitakuwa ni vya kusukuma mafuta na viwili kupunguza kasi ya mafuta.

Kazi ya tatu ni kujenga vituo 29 vya kulainisha vyuma au mabomba ambapo kati ya hivyo, vituo 22 vitajengwa Tanznaia na saba nchini Uganda.

Ya nne ni kujenga vituo 76 vya kufunga valvu, 53 vitakuwa Tanzania na 23 nchini Uganda. Na kazi ya mwisho alisema ni ujenzi wa matangi matano yatakayotumika kuhifadhi mafuta katika bandari ya Tanga.

Join our Newsletter