Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2022 01 10Article 584578

Maoni of Monday, 10 January 2022

Columnist: www.habarileo.co.tz

Rais Samia agusa wengi uteuzi Mawaziri

Samia agusa wengi uteuzi Mawaziri Samia agusa wengi uteuzi Mawaziri

WASOMI na wachambuzi wa masuala ya siasa wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi makini wa mawaziri, manaibu mawaziri na makatibu wakuu na manaibu.

Wamesema kwa mwendo huo hakuna mzembe atakayevumiliwa ndani ya serikali, hali inayoonesha uwepo wa utawala bora katika serikali yake.

Wakati wasomi na wachambuzi wakisema hayo, Waziri Mteule wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula mbali na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini amesema hatorudi nyuma katika kutekeleza ndoto na maono ya Rais Samia ya kusimamia ardhi na kuendeleza makazi nchini.

Dk Mabula aliyasema hayo jana wakati alipozungumza na HabariLEO kuhusu mipango ya wizara hiyo baada ya uteuzi huo ambapo alimshukuru Rais Samia na kumuahidi utendaji uliotukuta, kwa weledi wa hali ya juu ili kufanikisha malengo ya serikali.

Alisema ili kutafsiri kivitendo ndoto na maono ya Rais Samia, wizara pamoja na mambo mengine imeweka mikakati ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yatakayoleta ustawi wa wananchi na serikali kwa ujumla.

Alisema kwa kuwa sehemu kubwa ya ardhi nchini haijapimwa, jambo atakapofanya katika nafasi yake hiyo kwa wizara kutilia mkazo suala la upimaji wa ardhi ambayo hadi sasa asilimia 25 pekee ndiyo iliyopimwa huku 75 ikiwa bado haijapimwa.

“Kipaumbele cha pili kitakuwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi bora ya ardhi ili waweze kunufaika nayo, badala ya kuzalisha migogoro,” alisema.

Alisema amepanga kuwatuma maofisa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kutatengwa siku moja hadi mbili kwa maofisa hao kwenda kutekeleza jukumu hilo ambalo mwisho wa siku litakuwa na msaada mkubwa kwa wananchi na serikali kwa ujumla.

Dk Mabula aliongeza kuwa wizara itahakikisha kuwa maeneo ya mijini yanakuwa na mpango wa matumizi ya ardhi ili kumaliza migogoro na misuguano kuhusu umiliki wa ardhi katika maeneo yote ya mijini.

Aidha, Dk Mabula alisema jambo lingine ni kushirikiana na vyombo vya habari ili kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi kwa kueleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya ardhi nchini na namna zilivyoshughulikiwa na serikali na kuleta ustawi wa maisha ya wananchi.

“Kwa kushirikiana kwa karibu na Kituo cha Uwekezaji tutaimarisha uwezo na utendaji wetu ili kuwapatia kwa wakati wawekezaji wanaohitaji ardhi pamoja na kutatua migogoro kwa haraka zaidi ili kuondoa malalamiko,” aliongeza.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Dk Kaanaeli Kaale alimpongeza Rais Samia kwa kuimarisha baraza lake la mawaziri akisema hiyo ni njia nzuri ya kuwatenga wazembe na wasiokuwa na nia njema ili wasimuangushe.

“Rais Samia anataka watu watakaokuwa na lugha moja ili kuyafikia malengo yake, anataka watu wenye uwezo wa kufanya kazi kama timu moja ili kuyafikia malengo ya serikali katika kuwatumikia wananchi,”alisema.

Aliongeza kuwa Rais Samia kwa weledi wake hawezi kufanya kazi na watu wazembe, wanafiki na wanaofanya kazi kwa ajili ya maslahi yao kwanza kabla ya maslahi ya taifa kwa sababu wanaweza kuleta mgawanyiko mkubwa serikalini.

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Gabriel Mwang’onda alisema rais siku zote akihisi kuwa watendaji wake wanafanya mambo tofauti na anavyotaka hakuna njia nyingine zaidi ya kufanya mabadiliko ili kuondoa wababaishaji wanaokwamisha malengo yake.

Alisema Rais Samia amefanya vizuri kuunganisha baadhi ya wizara ambazo zilikuwa zikifanya jambo moja, akitolea mfano wa iliyokuwa Wizara ya Uwekezaji na Wizara ya Viwanda na Biashara na kuwa moja.

Kwa upande wake Abbasi Mwalimu ambaye ni Mchambuzi wa Siasa na Diplomasia alisema mabadiliko ya mawaziri yanategemea mahitaji ya Rais Samia ambapo anahitaji watu kutekeleza kile anachokitaka na anayekwenda kinyume ndio kama walioachwa katika mabadiliko hayo.

Alisema dira na falsafa ya Rais Samia isipofuatwa badala yake watu wakawa na dira zao na falsafa zinazotofautiana na ya rais, kitakachofuata ni kufanya marekebisho ili watu hao wawapishe watakaofuata dira na falsafa ya rais katika kuongoza nchi.