Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 17Article 579382

Maoni of Friday, 17 December 2021

Columnist: www.tanzaniaweb.com

Ricardo Kaka, Mlokole aliecheza soka na imani yake mkononi

Ricardo Kaka Ricardo Kaka

Siku kama ya leo mwaka 2007, Ricardo Kaka alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia. Nyuma yake walimaliza Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Hotuba yake fupi usiku ule ilivutia zaidi ya tuzo yenyewe. Ilivutia zaidi ya lile bao alilowafunga Manchester United kule Old Trafford. Ilivutia zaidi ya ile pasi yake kwa Hernan Crespo dhidi ya Liverpool.

Baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza Ricardo Kaka alisema, "Nilipokanyaga uwanjani siku ya kwanza nikiwa mvulana wa miaka 15, nilikuwa natamani mambo mawili tu moyoni mwangu"

"Moja ni kuichezea timu ya ndoto zangu na timu inayoshabikiwa na familia yangu, Sao Paolo. Pili ni kupata nafasi ya kuichezea timu ya taifa ya Brazil mechi moja tu"

"Lakini maandiko yanasema! Maandiko yanasema ukiomba kidogo, unapewa zaidi. Tazama leo nimekuwa mchezaji bora wa dunia. Nani alitegemea. Ni Mungu tu ninayemuamini siku zote"

Siku anayotua AC Milan akitokea Brazil katika uwanja wa ndege wa Malpensa waitaliano wengi walimtazama Ancelotti kwa makasiriko wakisema amesajili kijana laini wa kilokole ambaye hatawezana na soka gumu la Kiitaliano.

Mkononi mwake alikuwa ameshika Biblia na shingoni mwake ilikuwa imening'inia rosari na usoni alikuwa na tabasamu kubwa.

Hakuna aliyedhani kwamba mguuni mwake kuna maji, miujiza na uponyaji wa mpira. Kama alivomuamini Mungu, mpira pia ulimuamini yeye.

Ni sababu hii ya imani ilimfanya akatae dili la kwenda Man City kabla ya kupokea ofa ya Real Madrid. Man City walikuwa tayari kumlipa paundi laki tano kwa wiki. Imagine paundi laki tano kwa wiki mwaka 2009??

Lakini Kaka alisema pesa siyo kila kitu. Kwake Mungu ndiyo kila kitu na hasikii amani ya Mungu ndani yake ikimtaka ajiunge na Man City.

Alienda Real Madrid kuchukua pesa ndogo zaidi, hadi leo anaamini kwamba, alifeli Real Madrid kwa mipango ya Mungu.