Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 26Article 553822

Maoni of Thursday, 26 August 2021

Columnist: TanzaniaWeb

Ripoti ya NEC Yachochea mahitaji ya Katiba Mpya

Rais Samia akipokea mapendekezo ya katiba kutoka NEC Rais Samia akipokea mapendekezo ya katiba kutoka NEC

Mjadala wa madai ya Katiba mpya unazidi kushika kasi kila kukicha, licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kuomba apewe muda ili aimarishe uchumi kwanza, ripoti ya Uchaguzi Mkuu 2020 ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imechochea madai hayo.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, Agosti 21 aliwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia na kutoa mapendekezo saba ya kufanyiwa kazi, likiwemo la kuanzishwa kwa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo itawapa meno zaidi.

Miongoni mwa hoja za wanaotaka Katiba mpya ni uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, uwepo wake unatajwa utasaidia chaguzi kuendeshwa kwa uhuru na haki.

Tume iliyopo imekuwa ikilalamikiwa kutotenda haki kwa sababu ya muundo wake, uteuzi wa viongozi na watendaji wakuu hufanywa na Rais ambaye wakati mwingine huwa ni mgombea urais.

Muundo huo umekuwa ukiifanya Tume kutoaminika kwa wananchi na chaguzi ambazo wanazisimamia zimekosa mvuto na kuaminika kama ilivyo kwenye baadhi ya mataifa ambayo Tume zao zinafanya kazi kwa uhuru.

Mapendekezo ya NEC ya kutaka ianzishwe sheria inayowatambua na kuwapa mamlaka zaidi imetoa tafsiri kuwa wanataka wajiendeshe kwa uhuru na ufanisi zaidi pasi hofu ya kuingiliwa na viongozi, yanaipa nguvu hoja ya wanaotaka tume huru ya uchaguzi.

Licha ya NEC na viongozi wa Serikali mara kwa mara kupinga kutoa au kupokea maelekezo ya uendeshaji wa uchaguzi, lakini ukweli unabaki kuwa kuna mkanganyiko wa kisheria na tume hiyo haiko huru.

Baadhi ya mapendekezo yanaonyesha wanalenga kuboresha utendaji, kuongeza kuaminika kwa wadau na kupata uhuru zaidi.

Tume imekuwa ikilalamikiwa kuwatumia wakurugenzi wa halmashauri ambao ni makada wa chama tawala na huteuliwa na Rais wa chama tawala kusimamia chaguzi, sasa inapendekeza kuwe na watendaji wake hadi ngazi ya halmashauri.

Kama pendekezo hili litapitishwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika 2025, ingawa inaonekana gharama ndizo zitakuwa kikwazo cha utekelezwaji wake kama alivyodokeza Rais Samia.

Pendekezo jingine ni kuunganishwa sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura namba 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, sura ya 292 ili kurahisisha utekelezaji wa sheria hizo.

Kimsingi mapendekezo ya NEC yanaonyesha taasisi hiyo inavyofanya kazi katika mazingira magumu ambayo pia yanawafanya wasipate uungwaji mkono wa baadhi ya wadau pindi wanapotangaza matokeo ya kuendesha uchaguzi.

Wanaodai Katiba mpya wanataka iweke wazi juu ya Tume huru ya uchaguzi kama ilivyokuwemo kwenye rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2014 ambayo ilipendekeza Bunge lichuje na kupitisha majina ya wateule wa Rais kwenye nafasi husika.

Ipo mifano ya nchi kadhaa za Afrika ambazo Tume zao za uchaguzi zinafanya kazi kwa uhuru. Hilo limewezekana kwa sababu mamlaka ya uteuzi haijaachwa kwa Rais pekee, bali na Bunge limepewa mamlaka ya kuwathibitisha.

Mfano wa Tume hizo ni ile ya Zambia (ECZ) ambayo ilianzishwa mwaka 1996 chini ya Ibara ya 76 ya Katiba ya Zambia, inaundwa na mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wengine wasiozidi watatu ambao wanateuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge.

Tume hiyo imesimamia uchaguzi wa Agosti 12, 2021 nchini humo na kumtangaza kiongozi wa upinzani, Hakainde Hichilema kuwa mshindi katika uchaguzi huo dhidi ya Rais Edgar Lungu, ambaye alilalamikia rafu kwenye uchaguzi huo. Hichilema ameapishwa jana kuwa Rais wa saba wa Zambia.