Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2022 01 11Article 584908

Maoni of Tuesday, 11 January 2022

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SIO ZENGWE: Bashungwa bado uko michezo, hujaondolewa kabisa

Innocent Bashungwa Innocent Bashungwa

Wakati mabadiliko ya baraza la Mawaziri yakitangazwa mwishoni mwa wiki, moja ya maeneo niliyokuwa nikisubiri kwa hamu ni michezo, utamaduni na Sanaa kama litapata mabadiliko.

Hii ni kwa sababu nimekuwa nikitegemea mambo makubwa kutoka kwa Innocent Bashungwa, ambaye alikuwa Wazirti wa Utamaduni, Michezo na Sanaa. Kila nilipomsikia akizungumzia michezo, sikuona alipokosea Zaidi ya kuona upeo wake mpana katika masuala hayo.

Hata alipozungumzia utamaduni, niliona dhahiri kuwa hakuwa akibahatisha. Alikuwa akizungumzia mambo anayoyajua na jinsi ambavyo haoni yakifanyika humu ndani.

Niliona akili ya kiubunifu zaidi katika kufuatilia maendeleo ya michezo, kuikuza na kuoanisha michezo na burudani, vitu ambavyo ni nadra sana kusikia kutoka midomoni mwa wanasiasa.

Lakini, kama alikuwa na ndoto ya kutekeleza yale masuala ya kibunifu aliyokuwa nayo akilini mwake, muda ulikuwa mfupi sana kwake kuyatekeleza katika Wizara ya Utamaduni, Michezo na sanaa.

Lakini Rais Samia Suluhu Hassan hajamtupa mbali. Amempeleka Wizara ya Tamisemi, ambayo ni kubwa Zaidi na ina masuala mengi yanayoangaliwa na kufuatiliwa kwa karibu na wananchi wengi. Elimu, afya, usafiri, makazi na mengine mengi ni miongoni mwa masuala ambayo atayashughulikia kwa kiwango fulani kwenye wizara hiyo mpya.

Lakini hataacha kabisa michezo, utamaduni na Sanaa kwa sababu amepelekwa sehemu ambayo masuala hayo ndiyo yanatakiwa yawekewe nguvu zaidi kwa kuwa huko katika serikali za mikoa na mitaa ndiko ambako ni chimbuko la michezo, utamaduni na sanaa.

Chini yake wapo maofisa utamaduni, ambao wanasimamia pia michezo na Sanaa katika ngazi ya mikoa na wilaya. Chini yake ziko shule za msingi na sekondari, ambako watoto wanatakiwa wapewe mafunzo ya msingi ya michezo, utamaduni na sanaa.

Chini yake wako walimu ambao wakipewa nyenzo sahihi za kufundisha kanuni za msingi za michezo na Sanaa, wanaweza kuwa wasanii au wanamichezo wakubwa hapo baadaye.

Ni ajabu kwamba mchezaji anayefikia ngazi ya kucheza ligi daraja la kwanza au Ligi Kuu, hajui kanuni za msingi za mchezo huo na hivyo kocha wa klabu hizo za juu analazimika kutumia muda mwingi kumfundisha mambo hayo badala ya kujikita zaidi katika mbinu.

Leo hii tuinasikia wasanii ambao mashairi ya nyimbo zao ni kama mazungumzo ya kawaida. Hayana usanii wala maono, hayana misemo wala methali na cha zaidi wala mafumbo. Ni bora liende.

Na sasa wanajihami kwa kusema hivi ndivyo watu wanavyotaka, kumbe ni kutokuwa na misingi imara ya fasihi na utunzi wa nyimbo ambao zamani tulifundishwa vyema darasani, tukifuatilia kwa makini ustadi wa watu kama Shaaban Robert na Andanenga katika mashairi.

Wakati fulani pia walimu kutoka chuo kama cha Malya walikuja shuleni na kutufundisha kanuni za msingi za michezo kama soka, mpira wa wavu na netiboli kwa wasichana. Leo hawa hawaonekani.

Hivi ni vitu ambavyo vinatakiwa vifundishwe kutoka ngazi ya chini kabisa ambako Mheshimiwa Bashuingwa amepelekwa kusimamia.

Ule ubunifu ambao Bashungwa alikuwa akiuzungumzia katika mahojiano yake na vituo mbalimbali vya redio na televisheni, hauwezi kufa kwa sababu tu amehamishwa kutoka Wizara ya Utamaduni, Michezo na Sanaa.

Bado mambo hayo ni moja ya majukumu yake katika wizara mpya na hivyo, matarajio ni kuona akianza kutekeleza moja ya mambo aliyokuwa akiyawaza kwa kujanzia ngazi ya wilaya ili hapo baadaye tupate wanamichezo waliopikwa sawasawa badala ya hawa wa kufundisha ukubwani.

Cha msingi ni kukaa na watu sahihi, wenye fikra sahihi na maono ili kujua mtasukumaje gurudumu la maendeleo ya utamaduni, michezo na Sanaa huku masuala mengine muhimu katika wizara hiyo yakisonga mbele bila kukwamishwa na jitihada hizo.

Wako watakaosema tuweke nguvu katika michezo ya shule za sekondari, wako watakaosema kwa kuwa uko Tamisemi basi utaweza kusimamia vizuri Kombe la Taifa na wengine watakuja na mawazo mengi.

Lakini inabidi tatyhmini ya kina ifanyike. Kazi Kwako.