Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 07 13Article 546844

Maoni of Tuesday, 13 July 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SIO ZENGWE: Hatutarajii kumuona Mzee Mpili ndani ya Yanga TV

SIO ZENGWE: Hatutarajii kumuona Mzee Mpili ndani ya Yanga TV SIO ZENGWE: Hatutarajii kumuona Mzee Mpili ndani ya Yanga TV

KUTAYARISHA vipindi vya televisheni ni moja ya kazi ngumu na inayogharimu fedha nyingi kwa kuangalia gharama zinazoambatana na utayarishaji, vifaa na vitu vingine.

Mbali na gharama hizo, liko tatizo la kuwapata watu sahihi kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu zinazohitajika katika vipindi hivyo na hali kadhalika taarifa nyingine muhimu ambazo baadhi ya wahusika wanaweza kuzizuia kutoka bila ya sababu za maana.

Pia vingine vinahitaji kuwalipa wale ambao watapoteza muda na mali zao kwa ajili ya kushiriki katika vipindi kutokana na ukweli kwamba ushiriki wao huongeza thamani ya kipindi.

Hivyo si ajabu kuona vituo vyetu vya televisheni vimejaa vipindi vya nje ambavyo baadhi vina maudhui ambayo hayaendani kabisa na utamaduni wetu, hapa sina maana ile pekee ya tabia na vitendo vichafu vinavyohubiriwa kila mara dhidi ya utamaduni wa kigeni, bali mambo mengi.

Mfano, ili uchekeshwe na kichekesho cha Mmarekani, ni lazima uwe unafahamu utamaduni na mambo ya Kimarekani ili uweze kupata mantiki na baadaye kucheka. Mfano kipindi cha vitimbi cha “Perfect Strangers” ni vigumu kumchekesha kila mtu duniani, isipokuwa kwa wale wanaoelewa utamaduni wa taifa hilo na mengine yanayolingana nalo katika masuala ya kijamii na hata kisiasa na kiuchumi.

Kwa hiyo vituo vyetu vimejaa vipindi vya aina hiyo kwa sababu ya gharama zinazoambatana na utayarishaji na hata stadi za kuviandaa.

Kwa hiyo kuna wakati unakutana na vipindi vilivyoandaliwa humu nchini ambavyo unahisi viko chini ya kiwango na hivyo badala ya kuangalia, unajikuta unakosoa kila kitu hadi kipindi kinaisha.

Hapo labda mtayarishaji hakupata watu wa kutosha kujaziliza maudhui aliyokusudia, hakuweza kufika sehemu zinazotakiwa au hana stadi za kutosha kumuwezesha kuandaa kipindi kilichojaa maudhui yanayolingana na mada aliyoilenga.

Si ajabu basi kukuta mtu kama Mzee Mpili anapewa muda mwingi katika redio na televisheni, eti aeleze alifanikishaje ushindi wa Yanga wa bao 1-0 dhidi ya Simba wakati hakuingia uwanjani kucheza. Aeleze eti hao ‘watu wake’ ni kina nani, wakati anayemhoji anaelewa fika kwamba huyo anayemuhoji hajashiriki kwa chochote kufanikisha ushindi huo.

Hivyo mtu anayekaa kuangalia kipindi hicho, atakosoa mwanzo hadi mwisho, akijua kabisa kuna mpango wa kuhamisha juhudi zilizofanywa na wachezaji na kocha na kuzihamishia kwa mtu ambaye hajahusika kwa lolote katika mechi. Kipindi kama hicho hakitazamiki, hakisikiliziki na habari zake hazisomeki bila ya kukosolewa mwanzo-mwisho.

Na niliangalia mjadala mmoja, watetezi wa vipindi kama hivyo eti wanasema “jamii ya siku hizi ndiyo inapenda mambo hayo”, halafu mwingine katika mjadala huohuo akahoji “ina maana vyombo vya habari siku hizi havitengenezi ajenda?

Kwa hiyo unajiuliza mbona hao watu wawili wako kwenye jamii moja inayoitwa ya “siku hizi” halafu wanatofautiana? Na kama ukifuatilia mjadala mzima wa suala hilo, utaona wengi wanaponda mtu kama Mzee Mpili kupewa muda hewani kama huo, licha ya kwamba wote ni wa ‘jamii ya siku hizi’ inayopenda vitu visivyo na kichwa wala miguu.

Wiki tuliyoimaliza jana kampuni ya Azam Media ilisaini mkataba wa Sh34.8 bilioni za haki za televisheni na klabu ya Yanga, mkataba ambao utadumu kwa miaka kumi, huku ukifanyiwa uchambuzi baada ya miaka mitano.

Mkataba huo utahusu maudhui yanayohusu klabu hiyo kama shughuli zake za kimichezo, yaani mechi za kirafiki, mazoezi, shughuli za maendeleo ya soka kama program za vijana na wanawake na hata Wiki ya Wananchi ambayo huandaliwa kila mwaka kwa ajili ya kufungulia msimu.

Maana yake, Yanga itatakiwa iwe makini kuandaa shughuli zake za mwaka ili zitakaporushwa na Azam Sports ziwe na thamani inayolingana na mzigo uliowekwa. Mechi za kirafiki za kujiandaa na msimu ziwe ni halisi zinazoipima Yanga na zinaoweka thamani kwa mtazamaji na mmiliki wa haki za televisheni.

Hata shughuli za Wiki ya Wananchi ni lazima ziwe zile zilizopangiliwa kiasi cha kuwapa Azam nafasi nzuri ya kutayarisha vipindi vilivyo na thamani kwa mtazamaji.

Maana yake ni kwamba ni lazima idara ya habari ya Yanga ipange kwa umakini shughuli zake, huku ikipendekeza mbinu za utekelezaji wa mikakati mikubwa ya klabu kwa jinsi ambayo itakuwa na mvuto unaoweza kuifanya Azam itafutwe kwa hamu na watazamaji.

Vipindi viwe siriaz.