Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 28Article 581671

Maoni of Tuesday, 28 December 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SIO ZENGWE: Hivi Simba ishaanza kuendeshwa kisasa?

Viongozi wa Simba SC Viongozi wa Simba SC

Tanzania ina uasili wake na utamaduni wake ambao ni muhimu kuuzingatia kila unapofanya mabadiliko au mageuzi makubwa ya namna yoyote ile.

Ukiwa na klabu ndogo inajiendesha vizuri kama taasisi ya kisasa, si rahisi kuambukiza ustaarabu au utamaduni huo kwa klabu nyingine kutokana na udogo wake. Ni dhahiri kuwa haitaweza kuwa na ushawishi wa kuigwa na wengine.

Lakini klabu kama Simba na Yanga zikifikia hatua ya kujiendesha kisasa, zikawa na vyombo vyake huru kama sekretarieti imara, bodi inayopanga na kuelekeza na wana hisa wenye ufahamu mpana, haitachukua mwaka kwa klabu nyingine kufuata aina hiyo ya uendeshaji.

Kwa hiyo, kwetu sisi, mabadiliko au mageuzi makubwa ya uendeshaji taasisi za michezo, yanaweza kufanikiwa tu iwapo yataanzia kwenye klabu hizo kubwa mbili zinazowagawanya Watanzania takriban nusu kwa nusu, ukiachana na siasa zao za nani ana mashabiki wengi.

Wakati huu ambao Simba wameshafanikiwa kufanya mageuzi ya kimaandishi kwenye katiba yake, huku Yanga ikionekana kujongea uelekeo huo, kila hatua inafuatiliwa kuona kama kweli Simba imeshaanza kuendeshwa kisasa baada ya safari ya takriban miaka minne ya mageuzi ya kimaandishi.

Simba sasa ina bodi ya wakurugenzi inayoongozwa na Salim Abdallah, maarufu kwa jina la kibniashara la Try Again, ambaye alipendekezwa na Mohamed Dewji, kama mwanahisa mwenye asilimia 49 za umiliki, huku ikiwa na wakurugenzi kutoka upande wa Mo na wa klabu.

Simba pia ina sekretarieti inayoongozwa na Barbara Gonzalez, anayesimamia shughuli za kila siku za klabu hiyo.

Pia ina timu ya soka iliyo chini ya Pablo, ambaye kwa kawaida anatakiwa awe na mamlaka kwa timu nyingine zote zilizo chini ya kikosi cha kwanza.

Pia ina mkutano mkuu wa wanachama ambao kama wana hisa wanatakiwa kushikilia asilimia 51 ya umiliki wa klabu hiyo.

Lakini kama wiki moja na zaidi nimesikia kitu ambacho hakionyeshi kwamba taasisi hiyo inaendeshwa kisasa kama inavyotakiwa.

Kwa kawaida bodi ya Simba, ambayo hujumuisha wawakilishi wa wanahisa, ndiyo hutakiwa kupanga na kuelekeza (plan and direct) kama kazi kubwa za bodi yoyote ile ya kisasa. Na hupanga kutokana na kuwa na taarifa nyingi kutoka kwa mkuu wa sekretarieti na vyombo vinghine vilivyo chini yake pamoja na zinazotoka katika mazingira yanayoizunguka klabu.

Baada ya kupanga ndipo huelekeza na hivyo kazi kubwa ya mkuu wa sekretarieti na kubuni mbinu na mikakati ya kutekeleza mipango ya bodi kama inavyoelekezwa.

Lakini juzi, kwa kutumia akaunti binafsi ya Instagram, Mohamed Dewji alitangaza kuwa amepokea mapendekezo mengi kutoka kwa watu mbalimbali wanaotaka Simba ijenge uwanja wake. Na akasema amekubaliana na mapendekezo hayo na akaahidi kuchangia Sh2 bilioni katika mpango huo.

Tamko lake kwenye Instagram likawa kama mpango uliopelekwa mbele ya bodi ya wakurugenzi kwa lengo la kutengenezewa mkakati wa utekelezaji kwamba ujengwe uwanja wa gharama ya Sh30 bilioni.

Na kesho yake wajumbe wa bodi wakaanza kuimba wimbo wa ujenzi wa uwanja, wakionyesha kuvutiwa na mapendekezo ya rais huyo wa heshima na wengine hata kudai kuwa mpango huo ulishakuwepo muda mrefu.

Mo anaweza kuwa alitoa pendekezo mtandaoni, lakini bodi ya wakurugenzi ilipaswa kuzingatia mambo mengi kabla ya kujitokeza hadharani na sifa kibao kwa mwekezaji huyo.

Suala la uwanja si suala la pesa peke yake.

Baada ya ripoti ya Lord Taylor wa England kulazimisha klabu ziondoe sehemu za kusimama kwa ajili ya kuongeza usalama viwanjani, Arsenal ilipata shida sana. Kuweka viti kulipunguza idadi ya mashabiki na mpango wa kupanua uwanja haukukubaliwa na manispaa.

Ikajaribu kupendekeza inunue uwanja wa Wembley, lakini ikakataliwa. Ikakubaliwa kuutumia kwa mechi zake za Ligi ya Mabingwa za kuanzia msimu wa mwaka 1999 hadi 2000.

Ilipoona kila kitu kimeshindikana ndipo ikapendekeza kununua eneo la viwanda na jalala lililopo kaskazini mwa London. Iliandika mchanganuo mkubwa na ndipo ilipokubaliwa na ujenzi ukaanza mwaka 2004. Baadaye Emirates wakawekeza fedha katika ujenzi na hivyo ukaenda vizuri hadi ulipokamilika mwaka 2006.

Suala la fedha halikuwa tatizo kwa Arsenal, bali andiko la kuweza kushawishi mamlaka zikubali kutoa eneo la ujenzi wa uwanja.

Yanga walijenga uwanja Kaunda, lakini leo si sehemu ambayo wanaweza kusema watauendeleza au kuupanua kwa kuwa si eneo rafiki kimazingira.

Hatutarajii Simba nayo ianze ujenzi wa uwanja ambao baada ya miaka kumi tu, ionekane uko sehemu isiyofaa..