Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 22Article 543745

Maoni of Tuesday, 22 June 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SIO ZENGWE: Kichekesho cha waandishi na uchaguzi TFF

SIO ZENGWE: Kichekesho cha waandishi na uchaguzi TFF SIO ZENGWE: Kichekesho cha waandishi na uchaguzi TFF

OKTOBA mwaka 2019, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF), Wilfred Kidao alitangaza mpango wa chombo hicho kufanya mabadiliko makubwa katika muundo na masuala mengine.

Alidokeza baadhi ya mambo kuwa ni ukubwa wa mkutano mkuu kupungua kutoka wajumbe 129 hadi 87, Kamati ya Utendaji kupungua kutoka wajumbe 13 wa kuchaguliwa hadi sita na idadi ya wapiga kura kupungua kutoka wanne kwa kila mkoa hadi wawili.

Alikuwa akizungumzia mabadiliko ambayo yangefanywa na mkutano mkuu mapema mwaka uliofuatia.

Huu ndio ulikuwa mwisho wa vyombo vya habari kuripoti kuhusu mabadiliko hayo makubwa na yaliyogusa sehemu nyingi. Vyombo vya habari havikuibua mijadala yoyote kuhusu mabadiliko hayo na kama yana chembechembe za kutaka kulinda viongozi waliopo madarakani kwa kuwaminya wanaotaka kuingia, hasa walio nje ya chombo hicho.

Ungetemea wadau mbalimbali wa soka, viongozi wa zamani, watu waliowahi kugombea na wanasheria kuhojiwa maoni yao kuhusu mabadiliko hayo, lakini habari zilizotawala zikawa ni zile za uwezo na udhaifu wa washambuliaji wa klabu za Simba na Yanga na ule uchambuzi wa ‘box-to-box midfielders wa klabu za Ulaya.

Yaani matukio yalitawala vyombo vya habari kuliko mambo muhimu yanaoufanya mpira uende uwanjani, uendelee au udumae, ufurahishe au kuchukiza.

Si redio, si televisheni, si magazeti mitandao ya kijamii iliyolipa suala hili umuhimu mkubwa. Lilionekana kama ni tukio la mara moja na kuachiwa lipite. Hata Mkutano Mkuu wa TFF ulipokaa pale kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mapema mwaka jana, hakukuonekana mshawasha wa waandishi kutaka kujua kwa kina jinsi mabadiliko yale yalivyopita na yanamaanisha nini ili wawataarifu wadau wa mpira kwamba chombo hicho kimefanyiwa mageuzi makubwa.

Kazi ya msingi ya vyombo vya habari ni kutaarifu, kuelimisha na kuburudisha. Angalau suala la kuwepo mabadiliko lilitaarifiwa kwa kiwango kidogo, lakini halikuelimishwa kwa wadau ili unapofika uchaguzi au wakati muhimu wa kuonekana malengo ya mabadiliko hayo, wahusika wafanye maamuzi sahihi.

Hivyo, kama mabadiliko ya katiba yaligusiwa tu na kuonekana hayangeathiri kwa kiasi kikubwa uchaguzi, hasa kwa watu walio nje ambao wanataka kuingia ndani, isingekuwa rahisi mtu kuanza kupekuwa kujua mabadiliko hayo kwa kina kwa kuwa hajaona mijadala mikubwa ikichambua kila kipengele cha mabadiliko hayo.

Kichekesho ni pale waandishi wanapojivua jukumu lao la kutaarifu na kuelimisha na kuwasukumia wagombea ambao wanalaumu sharti la idadi ya wadhamini wa wagombea urais kuwa wanachama watano, muda mfupi wa kuwatafuta na hata sharti la kuzuia mwanachama mmoja kudhamini wagombea wawili, huku katiba ikiwa haijaweka ukomo katika idadi ya wadhamini, kana kwamba ni uchaguzi wa kisiasa kama ilivyo katika vyama ambako wagombea urais hudhaminiwa na wanachama wengi wawezavyo ingawaje tofauti ni kwamba wanaowadhamini si wale wanaoenda kupiga kura katika mikutano yao ya maamuzi kama ilivyo kwa TFF.

Nimefuatilia mijadala mingi ya redio, magazeti na televisheni na kote nimeona lawama zinarushwa kwa wagombea kwamba hawakuwa makini na kwamba kama wangekuwa makini wangeshatafuta kanuni na katiba na kujua wanatakiwa wafanye nini, au wangeshaanza mikakati mapema ya kujijengea mazingira ya kudhaminiwa, kitu ambacho kingeweza kutafsiriwa na walioshika madaraka kuwa ni kuanza kampeni mapema.

Waandishi na watangazaji hawakutakiwa kufikia kiwango cha chini cha kujenga hoja kiasi hicho, bali kujirudi na kuona walikosea sehemu fulani katika wajibu wao kwa jamii—kutaarifu na kuelimisha.

Hivyo kicheko na kejeli kwa wagombea kingegeuziwa kwa waandishi wa habari kutokana na udhaifu huo mkubwa wa kutoelimisha umma kuhusu mabadiliko makubwa kama hayo. Hatutakiwi kuwa na ujasiri wa kuwadhihaki wagombea katika kitu ambacho hata sisi hatukukifanya kwa weledi. Katiba ina mabadiliko mengi sana ambayo yanaweza kuibua mijadala mizito iwapo vyombo vya habari vitafanya kazi yao kwa lengo la kusaidia maendeleo ya soka.

Kama vyombo vya habari havitaona umuhimu huo, basi kicheko, dharau, kebehi na dhihaka dhidi ya wanaolalamika sasa kuhusu ubovu wa mabadiliko ya katiba, haina budi kutugeukia sisi waandishi kwa kutochukua hatua stahiki, wakati stahili kutekeleza Wajibu wetu kwa jamii.