Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 11Article 537190

xxxxxxxxxxx of Tuesday, 11 May 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SIO ZENGWE: Manchester na Glazer, Simba na Mohamed Dewji

WAKATI tunasoma nadharia za maendeleo, tulikutana na moja ya “modernisation” ambayo inataka jamii zilizonyuma kimaendeleo, kuanza kuchukua usasa ili zilingane na nyingine zilizoendelea.

Na kuchukua huko usasa hakumaanishi kufanya juhudi zenu wenyewe, bali kuiga waliokwishafanikiwa kwa kuwa tayari wameshapitia mambo mengi hadi kufikia maendeleo na hivyo wana mbinu za kupambana na changamoto za njiani.

Kwa kiasi kikubwa nadharia hiyo ndio inatumika karibu sehemu nyingi duniani, ukiacha zile nchi zenye mrengo tofauti kuhusu maendeleo kama Russia, China na nchi nyingine za Asia.

Kwa hiyo, Tanzania haiwezi kukaa pembeni katika suala hilo. Katika michezo hivi sasa kuna moto wa mabadiliko ya uendeshaji klabu, kwa upande wa Yanga, huku Simba kukiwa na mabadiliko katika umiliki wa klabu.

Wakati mchakato wa Simba ukionekana kukwamia FCC, Ulaya kumeibuka vurugu ambazo zinaibua changamoto zitakazosaidia klabu za kwetu kujifunza wakati zikiendelea na mabadiliko.

Manchester United, Arsenal, Liverpool, Manchester City, Chelsea na Tottenham zilisaini mpango wa kuanzishwa kwa mashindano mapya ya European Super League, sambamba na Real Madrid, Barcelona na Atletico Madrid za Hispania, Juventus, Inter na AC Milan za Italia.

Lakini mzozo uliotokea ndani ya saa 24, ukihusisha mashabiki, wachezaji, vyama vya soka na serikali ulisababisha mpango huo kufa hata kabla ya kuanza.

Lakini kifo chake kimetonesha kidonda cha muda mrefu kwa mashabiki ambao klabu zao zilinunuliwa na matajiri, hasa wa Marekani.

Liverpool, Arsenal na Manchester United zinamilikiwa na matajiri au kampuni za Kimarekani na zote ziko katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki, wakitaka watu wenye hisia na kujali utamaduni wa soka, ndio wamiliki.

Mzozo mkubwa zaidi ulitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati mashabiki wa Man United walipovamia uwanja wa Old Traford kupinga kitendo cha wamiliki kuhusika katika mpango huo wa kuanzisha Super League, wakisema wameweka mbele zaidi maslahi ya kifedha kuliko utamaduni wa michezo ambao mafanikio hupatikana mchezoni, na si wa kuhakikishiwa. Manchester inamilikiwa na familia ya Glazer, ambayo kama mchezo ilianza kununua hisa kidogokidogo hadi 2005 ilipokamata asilimia kubwa za hisa na kukamilisha mpango huo mwaka 2010.

Sasa mashabiki, kama ilivyo kwa Arsenal na Liverpool, wanataka familia ya Glazer iachie hisa hizo ili ziende kwa mtu anayejali utamaduni wa kimichezo. Mashabiki wameshaiandikia bodi kutaka kuwepo na mabadiliko katika chombo hicho kwa kumuingiza mjumbe ambaye ataweka mbele maslahi ya michezo badala ya biashara (planetfootball.com).

Na barua nyingine imeandikwa na mashabiki kwenda kwa wadhamini wa klabu hiyo kuwatahadharisha kuwa wanaweza kujikuta katika hali ngumu iwapo wataendelea kuiunga mkono familia ya Glazer.

“Kama washirika wa kibiashara wa familia ya Glazer nyinyi ni walengwa wa shutuma kutoka kwa mashabiki kote duniani kwa sababu jumla ya pauni 279 milioni kwa mwaka mnazolipa, hazitaelekezwa katika kuwekeza katika kikosi ili kiweze kupambana na klabu bora ambazo United iko chini yake. Hazitaelekezwa katika kuikarabati Old Trafford au uwanja wa mazoezi, ambavyo vyote sasa vimepitwa na wakati na kugeuka kuwa alama ya Glazer kutovipa kipaumbele,” inasema barua hiyo iliyonukuliwa na ESPNA.

“Fedha zenu za udhamini zitatumiwa kulipa madeni na malipo ya gawio. Kuiunga mkono familia ya Glazers hakuisaidii klabu. Kunaendeleza uhusiano wa kinyonyaji.”

Kwa sasa United ina wadhamini 23 kote duniani, zikiwemo kampuni kubwa za Chevrolet, Adidas, DHL na Marriott Hotels huku TeamViewer ikitarajiwa kuchukua nafasi ya Chevrolet kifuani kwa dau la pauni 235 milioni (ESPNA). Mashabiki hao wanasema watagomea bidhaa za wadhamini hao, kuzishusha hadhi na kutumia bidhaa za wapinzani wa kampuni hizo.

Kwa kifupi mashabiki hao wanataka familia ya Glazer iachane na umiliki wa klabu ya Manchester United ili irudi katika utamaduni wake wa kawaida na kuweka mbele maslahi ya mchezo wa mpira wa miguu.

Join our Newsletter