Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 25Article 565678

Maoni of Monday, 25 October 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SIO ZENGWE: Tulipata nafasi nne Afrika bila ya Ligi Bora

SIO ZENGWE: Tulipata nafasi nne Afrika bila ya Ligi Bora SIO ZENGWE: Tulipata nafasi nne Afrika bila ya Ligi Bora

KWA jinsi tunavyotumia vibaya mitandao ya kijamii, sakata la Jumamosi la Biashara United kushindwa kwenda Libya kumalizia mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, limeongezea mizaha iliyojazana huko badala ya kustua wapenzi halisi wa mchezo wa soka.

Mizaha ni mingi na Biashara imekamilisha safari za klabu tatu kuondolewa mapema katika michuano ya klabu ya Afrika, ikiwa ni mwanzo wa mwaka ambao Tanzania ilipata nafasi nyingine ya kuwakilishwa na klabu nne.

Kwa mara ya kwanza ilikuwa miaka mitatu iliyopita wakati Simba ilipofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na hivyo kuchangia pointi nyingi katika kibubu cha Tanzania, kitu kilichoipandisha juu nchi na kuiwezesha kuwa na sifa ya kuwakilishwa na klabu nne kwenye michuano ya Afrika.

Mwaka uliofuata Simba ilitolewa raundi ya awali na akina Luis Miquissoni, wakati Yanga ikaondolewa katika raundi ya kwanza na kupata nafasi ya kujaribu kuingia hatua ya ligi ya Kombe la Shirikisho, lakini haikufua dafu; ikaangukia pua.

Mwaka huu, Yanga imeondolewa katika raundi ya awali baada ya kupangiwa na River Plate ya Nigeria; ikifungwa bao 1-0 katika kila mechi, huku Azam na Biashara zikijitutumua hadi ya raundi ya kwanza baada ya kupangiwa wapinzani hafifu.

Jumamosi, Biashara ilishindwa kwenda Libya kumalizia mechi ya marudiano, licha ya kuwa na mtaji wa ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza, wakati Azam iliondolewa na timu tajiri ya Pyramids baada ya kufungwa bao 1-0 nchini Misri. Jijini Dar es Salaam, Azam ililazimishwa sare ya bila kufungana.

Kwa hiyo, hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho haitakuwa na timu ya Tanzania, labda ni Simba tu ambayo ilikuwa ikitarajia kukamilisha safari yake ya kufuzu jana baada ya kushinda ugenini kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza.

Kuondolewa kwa timu tatu za Tanzania kunastua, hasa katika kipindi hiki ambacho wengi tunajivuna kuwa ligi yetu ni moja ya ligi bora barani Afrika kwa sasa, ikivuta wanasoka kutoka sehemu mbalimbali Afrika.

Wengi wanaweza kuchukulia kimzaha kuondolewa kwa Biashara kwamba huenda ni kosa la viongozi kutojiandaa mapema, au kuondolewa kwa Yanga, viongozi hawakuwa wamejipanga mapema, hasa baada ya ITC za Khalid Aucho, Djouma Shaban na Bangala kutopatikana mapema kuwahi mechi na Wanigeria.

Au wakachukulia kuondolewa kwa Azam kwamba kulitokana na kupangiwa moja ya timu bora Afrika, ambayo hadi sasa haina taji lolote la kuifanya iogopewe kama kigogo Afrika, licha ya kuwa katika mchakato wa kuandika historia.

Swali ni; je, tulistahili nafasi nne? Ni kweli ligi yetu ni kati ya ligi bora Afrika? Ubora unatokana na nini?

Pengine haya ni maswali ambayo inatupasa kujiuliza na kutafuta ukweli halisi.

Binafsi naona ubora wa ligi hauwezi kutokana na Simba kufurukuta kushinda nafasi na kutuongezea pointi katika kibubu chetu kilichoko Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambalo huziongezea nchi idadi ya klabu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kutokana na pointi inazokusanya ndani ya miaka mitano.

Hadi sasa bado hatujajenga utamaduni wa kudhibiti wa uwazi wa taarifa za kifedha za klabu zetu.

Katika nchi zote ambazo zimeendelea kisoka, au zina ligi bora, afya ya klabu haitokani na kiasi cha fedha alizonazo kiongozi au mdhamini wake, bali fedha zilizoko klabuni.

Taarifa za kifedha za klabu husaidia kutoa picha ya afya ya klabu, si tu ya kuiwezesha kushiriki ligi ya ndani, bali inapotokea hatari ya kuwepo fedheha kama hiyo iliyosababishwa na Biashara.

Shirikisho la Soka (TFF) lisingekuwa na wasiwasi na Biashara kama lingekuwa linajua uwezo wake wa kifedha. Wenzetu, klabu ikianza kutetereka huwekwa chini ya usimamizi kuangalia kama itajimudu kwa muda fulani na kukionekana hakuna dalili hushushwa daraja.

Labda utauliza, “na Yanga je?” Utayari wa kifedha wa klabu hufanikisha mambo mengine yote. Yaani kama tatizo ni ITC, ilikuwaje hadi dakika za mwisho ndipo ukimbilie Fifa kuomba iingilie kati? Kuna tatizo la kifedha katika suala zima la Yanga kushughulikia ununuzi wa wachezaji hadi kukamilisha usajili mzima.

Labda Azam kunaweza kuwa na tatizo kidogo la kiufundi au kiutawala kwa kuwa walishamaliza kila kitu. Mzigo ulikuwa kwa mwalimu na wachezaji kuthibitisha thamani yao.

Lakini usisahahu suala la wachezaji nyota na tegemeo watatu waliolazimika kukaa nje katika mechi hizo mbili dhidi ya Pyramids.

Kwa hiyo hakuna haja ya kuchekana au kufanya mizaha baada ya timu tatu kuondolewa mapema katika michuano ya Afrika.

Ni lazima kwanza tukubali kuwa kuna kosa sehemu fulani na baada ya hapo litafutwe suluhisho.

Binafsi tulipewa nafasi nne kabla hatujawa na ligi bora inayostahili kutambuliwa zaidi Afrika.