Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 16Article 571789

Maoni of Tuesday, 16 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SIO ZENGWE: Tunamshusha, kumpandisha Pablo kwa ajili gani?

Pablo Franco Martin Pablo Franco Martin

Wiki tuliyoimaliza ilikuwa ya kuwekana sawa kati ya mashabiki na wachambuzi baada ya kutolewa taarifa kuwa kocha mpya wa Simba, Pablo Franco aliwahi kuwa msaidizi katika klabu ya Real Madrid ya Hispania mwaka 2018.

Suala hilo lilianza baada ya wachambuzi kama kawaida yao ya kupenda ukwanza kusema hii ni mara ya kwanza kwa kocha wa klabu za Tanzania kumpata kocha kutoka moja ya ligi kubwa Ulaya na hasa klabu kubwa kama Real Madrid, ambayo mimeshatwaa ubingwa wa Ulaya mara 13.

Hapo ndipo wengine walipoingia mitandaoni kusaka taarifa sahihi kama kweli Mhispania huyo aliwahi kuifundisha Real Madrid na baadhi kuibuka na taarifa kuwa hajawahi hata kuingia katika orodha ya waajiriwa.

Waliweka orodha ya makocha wasaidizi waliokuwa chini ya Julen Lopetegui, ambaye alimrithi Zinedine Zidane mwaka 2018 na Solari Santiago aliyemrithi mikoba Lopetegui, lakini halikuwepo jina la Pablo.

Lakini mitandao ya Wikipedia na Transfer Market, ambayo taarifa zake haziaminiki sana, ilionyesha kuwa mwaka huo Pablo alikuwa msaidizi Real Madrid. Hata hivyo, mtandao kama Wikipedia hueleza bayana kuwa taarifa zake si za kuaminika na unaruhusu watu kurekebisha au kuongeza taarifa zaidi kuhusu jambo fulani kama wanazo.

Katika akaunti yake ya Linkedin, Pablo ameeleza kuwa kati ya mwaka 2018 na 2019 alikuwa mchambuzi wa Real Madrid wa timu pinzani. Yaani kama Real Madrid inacheza na Sevilla, kazi yake inakuwa ni kuangalia Sevilla inatumia mipira gani kutafuta mabao—krosi, pasi mpenyezo, au mipira mirefu, inajihami vipi na ni imara sehemu gani au dhjaifu sehemu gani.

Hata hivyo, mtu mwingine akaibuka na taarifa zake zinazoonyesha kuwa kipindi hicho kuna kocha mwingine ndiye aliyepewa jukumu hilo la kuchambua timu pinzani.

Ukiangalia sana mijadala hiyo utabaini kwamba ama inataka kumkuza Pablo kufikia kiwango cha juu sana, ili Simba ionekane imecheza karata bora au kumshusha hadi chini sana ili Simba ionekane imepigwa change la macho.

Binafsi naona tatizo kubwa la kwanza ni hilo la kutaka kukuza au kushusha kitu bila ya sababu za maana, bila ya kujihoji kwamba mwishowe itasaidia nini.

Ni muhimu sana kumchambua mtaalamu kama huyo anapopewa timu, lakini historia yake huko nyuma hubakia kuwa historia tu, kinachofuata mbele chaweza kuwa tofauti kabisa na ilivyokuwa huko nyuma.

Wapo makocha wengi ambao historia yao haikuonyesha mafanikio yoyote na hawakuwahi hata kufundisha klabu kubwa, lakini walipopata nafasi walionyesha uwezo mkubwa.

Chukulia mfano wa Carlos Alberto Perreira ambaye kabla ya kuiongoza Brazil kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1994, hakuwa amefundisha taifa kubwa kwa mafanikio zaidi ya kupewa nafasi ya kuifundisha Brazil kwa muda mfupi mwaka 1983. Aliwahi kuifundisha Kuwait, Fluminance, Ghana, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia.

Yuko Claudio Ranieri ambaye alifundisha klabu kubwa kadhaa Ulaya bila ya kutwaa ubingwa lakini akiziongoza klabu kadhaa kupanda daraja. Uwezo wake wa kukaribia ubingwa ulisababisha apachikwe jina la “Nearly Man” kutokana na kazi alizofanya Italia, Hispania, England na Ufaransa. Lakini aliporejea England 2014, aliiongoza Leicester City kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza.

Kama viongozi wa Leicester wangeangalia historia yake huko nyuma, wasingempa jukumu hilo kubwa ambalo pengine walidhani lisingewezekana la kuiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa.

Kuna mazingira mengi ambayo huweza kusababisha kocha asipate mafanikio sehemu fulani alizopitia na hivyo kuonekana bure, kumbe kuna mazingira tofauti yanayoweza kumjengea nafasi ya kutekeleza kikamilifu uwezo wake.

Kwa hiyo, sioni kama kuna tatizo kubwa kwa Pablo labda kama uhariri wa taarifa za Wikipedia na Transfer Market ulifanywa kwa njama zake aonekane kuwa aliwahi kuwa Real Madrid, kitu kitakachomaanisha kuwa si mtu safi na hivyo kuna tatizo na weledi wake.

Kitu kikubwa ni uwezo wake, mbinu na falsafa zake. Kama viongozi wa Simba walizingatia vitu hivyo na wanaamini kuwa ndivyo vitakavyoisaidia timu, historia yake huko nyuma kwamba aliwahi kufundisha klabu kubwa, au hajawahi kutwaa kombe au amekuwa akifundisha klabu ndogo, si muhimu.

Muhimu ni uwezo, falsafa na mbinu zake za mchezo. Karibu Pablo.