Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 09Article 569347

Maoni of Tuesday, 9 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SIO ZENGWE: Wakosefu wanapokosoana kuna tatizo, litatuliwe

Mmiliki wa GSM, Ghalib Said Mohammed Mmiliki wa GSM, Ghalib Said Mohammed

Fainali za Kombe la Dunia zitafanyika mwakani nchini Qatar zikikamilisha vita kali ya kampuni mbalimbali kudhamini timu za taifa zinazoshiriki.

Vita kubwa huwa kwa kampuni zinazotengeneza vifaa vya michezo kama Adidas, Puma na Nike, ambazo zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyashika mataifa makubwa katika soka ulimwenguni kama Ufaransa, Ujerumani, Brazil na Cameroon ambao ni wababe wa soka Afrika.

Mara nyingine vita hiyo huingia ndani kwenye timu za mataifa hayo. Ilisemekana mwaka 1994, Nike ililazimisha mshambuliaji nyota ulimwenguni wa wakati huo, Ronaldo de Lima acheze mechi ya fainali licha ya kuwa mgonjwa.

Taarifa zisizo rasmi zilisema Nike ndiyo iliyomtoa Ronaldo, ambaye aliugua degedege, hospitalini na kuhakikisha anacheza mechi ya fainali dhidi ya Brazil lakini ugonjwa ulionekana dhahiri kwa kuwa siku hiyo kilionekana kivuli cha ‘Phenomenon’ na Brazil ikalala 3-0.

Kampuni hizo pia hupambana katika ngazi ya klabu. Inasemekana Adidas ndiyo ilihusika kwa kiasi kikubwa kuhakikisha Paul Pogba anasajiliwa Manchester United baada ya vigogo hao wa Ulaya kutokuwa na mwanasoka nyota wa kuweza kuwauzia jezi na vifaa vingine, hasa kwa vijana.

Hilo halijawahi kuwekwa bayana lakini ubashiri umekuwa mkubwa na Adidas haijitokezi kufafanua.

Hali kadhalika, habari nyingine zinasema Nike ilikorofishana na Manchester United baada ya kuamua kumuuza Christiano Ronaldo kwenda Real Madrid, ambao wanavalishwa vifaa na Adidas. Inasemekana chanzo cha Nike kuondoka United ni mzozo huo.

Hata usajili wa Piere Emerick Aubameyang kwenda Arsenal ulichagizwa na Adidas baada ya klabu hiyo ya London kutokuwa na jina kubwa la kuwauzia vifaa.

Habari hizo zote hazijawahi kuwa rasmi, pengine ni kutokana na sheria na kanuni kali zinazoongoza biashara ya mpira wa miguu maana kuhusika moja kwa moja kwa kampuni inayodhamini kusajili au kuamua nani acheze ni kuibua shaka kibao kwa wasimamizi wa mchezo na washiriki wengine.

Lakini hali huku kwetu inaonekana kwenda tofauti.

Wiki iliyopita kuliibuka mjadala wa GSM kudhamini klabu nyingine mbali na Yanga, baada ya mmiliki wake kutajwa amesaidia klabu kadhaa zilipokwama kifedha.

Viongozi wa Simba hawajazungumza, lakini watu wenye vinasaba vya Mtaa wa Msimbazi wameshazungumza sana kuonyesha hiyo ndio hoja iliyopo upande wao.

Yanga nao wamejibu kwa kuonyesha ushahidi hata kampuni ya Mohamed Dewji aliyewekeza Simba, yaani Mohamed Enterprises, ilidhamini klabu nyingine msimu uliopita na hivyo wanashangaa kwa nini sasa Simba wanalalamika baada ya kuona GSM anaongeza kasi.

Si dhambi kwa kampuni moja kudhamini zaidi ya klabu moja katika ligi moja.

Ni vitu vya kawaida sana na ndio maana nimejaribu kuonyesha hapo mwanzo jinsi kampuni hizo kubwa duniani zinapodhamini timu au klabu zilizo katika ligi moja na kunakuwa hakuna tatizo.

Hata hapa kwetu, Simba na Yanga zinadhaminiwa na SportsPesa na awali zilidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager na hakukuwa na tatizo lolote, achilia mbali haki za televisheni za Azam Media ambazo zinahusu klabu zote kupitia Shirikisho la Soka (TFF).

Pengine tatizo laweza kuwa ushiriki wa wafanyakazi au watu wenye madaraka ya juu katika kampuni hizo, kujihusisha pia na klabu moja katika shughuli zote kubwa, wakati ndio wenye maamuzi makubwa katika kampuni zao.

Kama MeTL inadhamini klabu nyingine zaidi ya Simba, halafu mmiliki wake Mohamed Dewji anakuwa ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba huku akimiliki takriban asilimia 49 za hisa, basi hapo kuna tatizo.

Kama Hersi Said ndiye Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM na ndiye mwenye sauti kubwa baada ya Ghalib, anakuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Yanga na anahusika kwa kiasi kikubwa katika shughuli za uendeshaji, pengine kuliko hata Ofisa Mtendaji Mkuu, basi hapo kuna tatizo.

Wote hao wawili wameona kasoro hiyo ndio maana wanakosoana. Cha msingi ni kwa wasimamizi wa mpira kutambua kuwa hadi hao wakosefu wawili wamefikia hatua ya kukosoa makosa yao wote wawili, basi kuna tatizo ambazo linatakiwa lisimamiwe na mwongozo au kanuni imara itakayozuia harufu hiyo ambayo wakosefu hao wanaiona.