Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2022 01 07Article 583915

Maoni of Friday, 7 January 2022

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SPOTI DOKTA: Ligi za ulaya na mapumziko ya kijanja

Ligi za ulaya na mapumziko ya kijanja Ligi za ulaya na mapumziko ya kijanja

Tukiwa ndani ya wiki ya kwanza Januari 2022 tuliona ligi kubwa tano za Ulaya zikiendelea na utamaduni wa mapumziko ya kijanja ya kati ya Desemba na Januari. Ni kawaida kwa ligi kubwa za Ulaya ikiwamo La Liga, Bundesliga, Series A na Ligue 1 kuwa na mapumziko ya kijanja majira ya baridi kali kipindi cha Desemba na Januari.

Kwa mara ya kwanza utamaduni huo umetua katika Ligi Kuu ya Scotland wakiufanya kwa kuanza mapumziko wiki hii mpaka mwishoni mwa mwezi huu. Ligi nne za awali zimekuwa na utamaduni huo kwa muda mrefu wa kutoa mapumziko haya wakati wa majira ya baridi Desemba hadi Januari kipindi cha sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Wakati ligi hizi kubwa zikifanya hivyo Ligi Kuu ya England (EPL) wao hawana mapumziko ya kupisha majira ya majira ya baridi kali. Tumeshuhudia katika EPL michezo kadhaa ikichezwa siku ya Boxing Day na Mwaka Mpya.

Unaambiwa mapumziko ya kijanja ambayo EPL hawana huwanufaisha wanasoka wanaocheza katika ligi nne kubwa za Ulaya kwani yanawapa mwanya wa kutunza nguvu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi. Vilevile huwapa nafasi kujumuika na familia zao katika sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, hivyo kuwapa ari hatimaye hujituma kusaidia mafanikio ya klabu hizo.

Kocha wa Manchester City, Pep Gurdiola anayakumbuka mapumziko hayo alipokuwa na Klabu ya Buyern Munich akisema kuwa siku 30 za kupumzika kwa Bundesliga ziliwapa nguvu mpya wachezaji. Kuanza kwa mapumziko kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu ya Scotland kumekupokewa kwa shangwe na klabu zinazoshiriki.

Aliyewahi kuwa kocha wa Liverpool na Leicester City, Brendan Rodgers ambaye sasa anaifundisha Celtic ya Scotland amenukuliwa akisema kuwa uamuzi huo unaipa nguvu timu yake na wanaukaribisha kwa mikono miwili.

MAPUMZIKO YA KIJANJA

Bundesliga ndiyo iliyokuwa inaongoza kutoa mapumziko marefu ambayo ni siku 30. Michezo ya mwisho ilichezwa Desemba 19, 2021 na itaendelea kesho - siku ya Ijumaa Januari 7, 2022. Wakati kule Hispania mechi za mwisho za Desemba walikomea Desemba 22 na kuanza tena baada ya mwaka mpya.

Ufaransa ambako kuna Ligue 1 mechi za mwisho zilikomea Desemba 22 na zitaendelea kesho Januari 7 na kwa Italia (Serie A) walikomea mechi zao Desemba 22 na leo zitaendelea. Ni kawaida mapumziko hayo ya kijanja kuibua mjadala hasa pale timu za England zinazoshiriki EPL zinapoboronga katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa.

Moja ya sababu kubwa inayotolewa na ligi hizo kubwa ni kutokana na kipindi hicho kuwa na baridi kali kiasi cha kuwafanya wachezaji kuwa katika mazingira magumu ya kiuchezaji. Kipindi hicho hali ya hewa katika nchi za Ulaya ambako ndiko zipo huwa ni mpaka kufikia chini ya nyuzijoto -3.

Inaelezwa kutokana na wachezaji hao kutoka katika maeneo mbalimbali baadhi yao wamekuwa wakiathiriwa na hali ya hewa ya baridi kali kiasi cha kushindwa kucheza kwa kiwango cha juu. Kitabibu ni kweli kabisa kucheza kipindi cha baridi kali huwa na madhara ya kiafya ambayo yanaweza kujitokeza ikiwamo kupumua kwa shida, udhaifu viungo na kukamaa misuli.

Vilevile inaelezwa kwamba kutopumzika Desemba hadi Januari kwa EPL ni chanzo cha kutofanya vizuri kwa klabu zao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwani wachezaji wanakuwa wamechoka na kuwa majeruhi. Tafiti zilizowahi kufaywa zinazonyesha uwepo wa idadi kubwa ya majeruhi EPL majira ya baridi kali Desemba kuendelea.

Ligi zinazopumzika hasa kipindi cha Desemba hadi Januari kwa nchi za Ulaya ambacho baridi huwa kali huku ikiambatana na theluji huwa na faida ya kutunza utimamu wa mwili wa mchezaji.

FAIDA ZA MAPUMZIKO

Kwa ujumla mapumziko ya kijanja kipindi cha Desemba hadi Januari huwafanya wachezaji kutunza nguvu, kuepukana na majeraha na kuwa na ari kutokana na kujumuika na kufurahi na familia zao. Kwa kawaida misuli imeundwa kwa bunda la nyuzi zenye uwezo wa kunepa au kuvutika kama ‘rubber band’.

Kufanya mazoezi misuli huvutika mara nyingi na pengine kupitiliza kuwango chake. Jambo hilo ndilo linalosababisha mpaka misuli kuchanika na kusababisha majeraha makubwa. Ili kulinda afya ya mwili wa mchezaji yapo mambo yanayohitajika ili mwili uweze kusahihisha na kujikarabati kwa ajili ya kuponyesha majeraha ambayo ni kama haya mapumziko ya kijanja.

Kupumzika kuna maana kuwa ni kile kipindi ambacho mwili haufanyi shughuli yoyote ni hali ya kutulia pasipo misuli kujishughulisha. Unapofanya mazoezi au shughuli misuli hufanya kazi huku ikitumia sukari ya mwilini katika kuwezesha misuli kujikunja na kukunjuka ili kufanya mambo mbalimbali ikiwamo kutembea, kukimbia na kuruka.

Kipindi hiki hutokea mabadiliko mengi ikiwamo tishu za misuli kuvunjikavunjika, kupungua kwa sukari iliyohifadhiwa katika misuli na mwili kupoteza maji. Wakati wa kupumzika ndipo mwili unapopata nafasi ya kusahihisha upungufu wa maji na sukari na kukarabati tishu za misuli zilizopata madhara au kujeruhiwa.

Hivyo, bila mwili kupata mapumziko ya kutosha ina maana mwili utaendelea kupata athari katika tishu za misuli.

Hapa tunapata picha wale wachezaji wa ligi kubwa za Ulaya zinazopumzika kipindi cha baridi ya Desemba na Januari wanafaidika katika kutunza utimamu wao wa mwili. Wengi huwa na kawaida kwenda kupumzika katika maeneo yenye kuvutia na mandhari nzuri wakiwa na familia zao.

Klabu ya Bayern Munich chini ya Guardiola ilikuwa na programu ya mazoezi kwa kuwapeleka nchi za Uarabuni kama vile Dubai ambako kuna hali ya joto na mazingira ya kuvutia. Changamoto kubwa kwa ligi hizo kwa sasa ni janga la Uviko-19 kwani kuna ongezeko la visa kwa wachezaji na viongozi kuugua.

Hali hiyo ya baadhi ya klabu kuuguliwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye maambukizi ya corona imetishia kwa baadhi ya michezo kuwa na uwezekano wa kuahirishwa.

Pia imeshuhudiwa wiki hii supastaa wa kimataifa kutoka nchini Argentina, Lionel Messi amelazimika kujitenga baada ya kubainika kupata maambukizi ya Uviko-19, hivyo atakosa mechi kadhaa zitakazoanza.

Tusubiri kuona kama mapumziko haya ya kijanja yataendelea kuwapa faida ligi kubwa za Ulaya zenye utamaduni wa kupumzika kipindi cha Desemba hadi Januari.