Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 18Article 558151

Maoni of Saturday, 18 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

SPOTI DOKTA: Mdamu ana nafasi kubwa kurejea tena uwanjani

Gerald Mdamu, akiuguza majeraha nyumbani kwake Gerald Mdamu, akiuguza majeraha nyumbani kwake

Mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mdamu alikuwa miongoni mwa wachezaji waliopata ajali barabarani Julai 9, wakitokea mazoezini katika Uwanja wa TPC mjini Moshi.

Mdamu ambaye alivunjika miguu, kwa mujibu wa gazeti hili inaonyesha akiwa na nyumbani kwake anajiuguza baada ya kuruhusiwa kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), alikokuwa akipatiwa matibabu kwa takriban zaidi ya mwezi mmoja.

Mara baada ya ajali wachezaji majeruhi walipelekwa Hospitali ya KCMC mjini Moshi na hapo ndipo Mdamu alianza kupata matibabu mbalimbali ikiwamo kuwekewa vyuma tiba katika mguu wa kushoto uliopata mivunjiko miwili.

Baadaye aliendelea na matibabu Moi na kulazwa huku akipata nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Mguu wake wa kulia unaonyesha kuwekewa vifaa tiba vyuma mtaani huviita antena katika mfupa wa chini ya goti ambao ni wa ugoko.

Kwa maelezo ya walioshuhudia tukio hilo majeraha ya mguu wa kushoto alipata mivunjiko wazi ya mfupa wa ugoko na mvujiko usio wazi wa mfupa wa nyuma ya ugoko. Wakati kwa mguu wa kulia alipata mvunjiko wa mfupa usio na jeraha la wazi wa paja.

Vilevile alipata majeraha machache ya kichwani, lakini ililazimika madaktari kufanya kazi ya ziada baada ya pia kuonekana figo zilipata tatizo katika ajali hiyo.

Habari iliyotoka Jumatatu katika gazeti hili ndugu yake mmoja alieleza kulikuwa na mpango wa kwenda kutibiwa Sauzi. Hapa nilikutana na maswali kadhaa toka kwa wasomaji wakidhani pengine tatizo lake limekuwa kubwa na imeshindikana kutibiwa Moi.

Kwa uzoefu wangu kufahamu miongozo ya kutoa rufaa kwa wagonjwa kama ingelikuwa hali yake ni mbaya isiyoweza kutibiwa nchini, basi Moi wangeishampa rufaa ya kumpeleka nje ya nchi.

Uamuzi wa kutaka kumpeleka Afrika Kusini pengine ni kutokana ndugu au jamaa wa karibu kuvutiwa na huduma za nchi hiyo kuwa za kisasa zaidi, lakini bado Moi tatizo hilo wanaweza kulimudu kwani wana vifaa na wataalamu wenye uzoefu.

Vilevile nimekutana na swali lingine likiuliza kuwa mchezaji huyo ataweza kupona kabisa na kurudi uwanjani na kucheza kama awali? Jibu ni kuwa anaweza kupona, kurudi uwanjani na kucheza kwani mifupa inavunjika na kuunga na kupona, na kuwa imara kuliko awali.

Kwa wale wanaokumbuka wapo wachezaji duniani waliowahi kupata mivunjiko mibaya ya mifupa wakapona na kurudi tena kucheza kana kwamba hawajawahi kabisa kuvunjika. Wachezaji hao ni pamoja na Djibril Cisse enzi hizo akiwa Liverpool; Aron Ramsey wa Arsenal na Kurt Zouma wa Chelsea.

Ingawa walipata mivunjiko wakiwa katika mchezo, lakini uvunjikaji wao unafanana na wa Mdamu.

Hivyo kama hawa walirudi uwanjani bila shaka hata Mdamu atarudi. Tukio hili linatukumbusha wachezaji kuzingatia ushauri wa madaktari juu ya kutunza afya ya mifupa iliyojeruhiwa.

Mdamu na wengine wafanye hivi mifupa ni tishu ngumu ambayo ndiyo inasaidia mwili kuweza kuweka umbile vizuri kwa ajili ya viungo vingine kujipachika na kujihifadhi.

Mwili wa mtu una takriban mifupa 206, kati ya hiyo 26 ni ya miguuni na 54 ya mikononi ambayo ndiyo inayopata majeraha mara kwa mara kwa wanamichezo.

Mifupa ndiyo inamuwezesha mwanamichezo kufanya kila kitu wakati wa kucheza au kufanya mazoezi. Hii ni kutokana na misuli inayojipachika katika mifupa na kutengeneza umbile la miili. Wakati misuli inapovutika na kujirefusha ndipo mwili huweza kufanya matendo mbalimbali ikiwamo kutembea, kukimbia na kuruka.

Ugumu wa mfupa ndiyo unaowezesha ubongo, moyo na mapafu kuwa salama kutokana na mwili kuipa hifadhi na kuwa kama ngao.

Vilevile ndani ya mifupa hutengenezwa seli zote za mwilini, kuhifadhi na kudhibiti madini mbalimbali ambayo ni muhimu kwa shughuli za mifumo ya mwili.

Mifupa hupata majeraha mbalimbali ikiwamo kuvunjika, kuteguka, kumomonyoka na kushambuliwa na magonjwa mbalimbali, hivyo kuweza kuathiri utendaji wake.

Wanamichezo wako katika hatari zaidi ya kupata mivunjiko ya mifupa kwa sababu wanatumia nguvu nyingi. Wanakumbana kimwili wakati wa kucheza na huku wakipata ajali za kimichezo.

Mwanamichezo anaboreshaje mifupa inapopata majeraha? Jibu ni rahisi - ni lishe mchanganyiko. Mienendo na mitindo rafiki kwa majeraha ya mifupa.

Mambo yafuatayo yameonekana kusaidia kuboresha uimara wa mifupa wakati wa kipindi cha uuguzi wa majeraha ya mifupa kwa wanamichezo. Ulaji milo kamili na virutubisho vya ziada ni muhimu katika uponaji na ukuaji wa mifupa kwani husheheni vitamini, madini na protini ambavyo vinahitajika katika ujenzi wa mifupa bora.

Mjeruhiwa ale zaidi mboga za majani, matunda na protini inayopatikana katika minofu ya samaki na nyama au jamii ya kunde. Pia anywe maji mengi takriban glasi 8-10 au lita 1.5-3 kwa siku. Maji ndiyo yanayosaidia shughuli zote za mwili na pia kuupa mwili madini yanayoimarisha mifupa.

Uzito wa mwili ni lazima udhibitiwe kwa kuzingatia maelekezo ya lishe toka kwa wataalamu lishe za wanamichezo. Muhimu kuepuka ulaji wa vyakula vya sukari, wanga na mafuta mengi.

Vilevile epuka matumizi ya tumbaku na vilevi ikiwamo pombe kwani hudhoofisha mwili na hatimaye kuingilia ukuaji wa mifupa kwa kuwa sumu za tumbaku hunyausha mishipa ya damu, hivyo kuzuia damu kwenda kwa wingi katika eneo lenye mfupa wenye jeraha.

Kwa aliyevunjika na kupewa matibabu ikiwamo ya bila upasuaji na upasuaji atahitajika kupumzika muda mwingi ili kuepukana na mtikisiko.

Kama ni mifupa ya mkono au mguu iliyovunjika, unyanyuaji wa vitu vizito au ukanyagio mguu inahitajika kuepukwa kwani unapoupa shinikizo la uzito mfupa uliovunjika kabla ya kupona vizuri unaweza kusababisha kutounga vyema.

Dhibiti matumizi holela ya dawa za maumivu ikiwamo zenye steroid na zinazofifisha mapigo ya kinga ya mwili kwani huathiri ukuaji na uimara wa mifupa. Epuka mambo ambayo yanaweza kukupa msongo wa mawazo, kwani hali hiyo inashusha kinga ya mwili ambayo ni muhimu kipindi cha uponaji.

Uimara wa mifupa ni muhimu kwa mwanamichezo, hivyo muhimu kushikamana na mambo haya ni kuzingatia ushauri wa daktari na mtaalamu lishe za wanamichezo.

Kuhusu Mdamu, muda wa kurudi uwanjani bado na pengine msimu huu na ujao kumuona itakuwa vigumu kuwa timamu kwa haraka. Hata hivyo hakuna kinachoshindikana chini ya jua. Tumuombee apone na kurudi tena kuutumikia mchezo wa soka.